Facebook Comments Box

Tuesday, October 9, 2012

MAJAMBAZI YAKAMATWA KWA CCTV BAADA YA KUIBA KWENYE M-PESA




JANET JACKSON NDANI YA HIJJAB



Pop star Janet Jackson mwenye umri wa miaka 46 ambae ni mpenzi wa zamani wa producer Jermain Dupri anaolewa mwaka 2013 na tajiri bilionea wa kiarabu Wissam Al Mana na inaaminika kwamba Janet itabidi abadili dini na kuwa muislam

YANGA WALALA TENA MZUNGU WA NNE

HISTORIA ya wachezaji wa Yanga kulala mzungu wa nne imejirudia tena Bukoba, baada ya kulala kwa kubanana katika kitanda kimoja kama ilivyokuwa Mbeya, licha ya kufikia katika Hoteli ya Smart, yenye hadhi kubwa.

Hali kama hiyo ilijitokeza wakati timu hiyo ikijiandaa kucheza na Prisons, Mbeya, huku aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet akianika ukweli ambao baadaye ulimponza na kufukuzwa.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wachezaji alisema, mambo ni yale yale kama ilivyokuwa Mbeya.

“Mambo kama ya Mbeya, hoteli ni nzuri, lakini wachezaji tumelala wawili wawili katika hoteli, pamoja na kupata huduma nzuri lakini tatizo lilikuwa ni hilo,” alisema mmoja wa wachezaji hao.

Hata hivyo wachezaji wanatarajiwa kurejea kwa usafiri wa basi, badala ya ndege maalumu ya kukodi ya Kampuni ya Precision Air, iliyotumika kwenda Kagera kwa ajili ya mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Kagera, uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Habari zilizopatikana kutoka kwa kiongozi mmoja, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, zinasema wachezaji hao watarejea kwa usafiri huo baada ya mchezo wao dhidi ya Toto African, ambao utachezwa keshokutwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Wachezaji hao wanatarajiwa kuondoka mjini Mwanza Ijumaa, baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Toto African, kwa basi maalumu walilopewa na wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania TBL kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.

Hata hivyo, gazeti hili liliweza kuongea na mkuu wa msafara, Mussa Katabaro, ambaye alisema anachojua yeye ni kwamba timu yao itarejea kwa ndege kama ilivyokuja.

Wakati huo huo, uongozi wa Kagera Sugar uliondoa mabango ya wadhamini wa Yanga, Kampuni ya Bia Tanzania, kutokana na kuwa wenyeji wa mchezo huo.

Kagera Sugar ambao ndio wenyeji wa uwanja huo kupitia kwa mratibu wake Mohamed Hussein, ilikataa katu katu mabango hayo kuwekwa katika uwanja huo, kwa kuwa wao ndio wa miliki wake.

MATUMLA NDANI YA MKASI NA SALAMA JABR





VURUGU ZA UVCCM MARA NDIO HIZI




UDA KULITEKA SOKO LA TANZANIA BAADA YA KUPATA MUWEKEZAJI

 
Picture
Viongozi wa Kampuni ya Simon Group na wengine Wakielekea kuzindua mabasi15 waliyowekeza UDA.
KAMPUNI ya Usafiri jijini Dar es Salaam (UDA) imejipanga kuteka soko la usafiri nchini ifikapo mwezi Machi mwaka 2013.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena alipokuwa akipokea mabasi 15 kutoka kampuni ya Tata Africa ya India ikiwa ni sehemu ya mabasi 30 yanayotarajiwa kuingizwa nchini ifikapo Desemba mwaka huu.

Kisena alisema kampuni ya Simon Group iliyowekeza katika shirika la UDA imejipanga kuwa kampuni kubwa barani Afrika kwa mtaji wa Dola25 milioni (sawa na Sh375 bilioni)  utakaowezesha kupatikana kwa mabasi 300 ifikapo mwezi Machi mwakani, “Simon Group imejipanga kuwa kampuni kubwa Afrika ifikapo Machi mwakani na tuna mpango wa kununua mabasi 300 kwa mtaji wa Dola25 milioni,” alisema Kisena.

Aliongeza kuwa kati ya mabasi hayo kutakuwa na mabasi ya wanawake, mabasi ya wanafunzi, mabasi ya binafsi, mabasi ya mikoani na mabasi yatakayosafiri barani Afrika, “Mazingira mabovu ya sasa ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam mara kwa mara yamekuwa yakisababisha udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake, bila shaka wengi wenu mtakumbuka vizuri kisa cha Maumba. Tunataka kukomesha udhalilishaji huo kwa wanawake ili wasafiri kwa uhuru na raha mstarehe,” alisema Kisena.

Kuhusu mabasi ya wanafunzi, alisema yatakuwa matano kila barabara kuu jijini Dar es Salaam na yatafanya kazi hiyo tu.

Kuhusu mabasi ya binafsi (Executive class), alisema yatakuwa na nauli ya juu lakini yatatoa huduma kama vile televisheni, vinywaji, magazeti na kiyoyozi, “Tunataka tuwahamasishe watu wasitumie tena magari yao binafsi. Unajua kwa mwezi mtu hutumia katiya Sh800,000 hadi Sh1milioni kununua mafuta ya gari, hela ambayo ni nyingi mno. Lakini kwa kutumia usafiri huu, inawezekana kubana matumizi,” alisema.

Akizungumzia mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) alisema kuwa wanatarajia kushinda zabuni ya kuuendesha kwa kuwa kampuni hiyo haina mshindani katika usafirishaji nchini, “Kwa sasa Dart inajengwa barabara ya Morogoro na barabara itakamilika mwaka 2014. Kwa sasa tutaendesha mradi huo kabla Dart haijaanza na kwa barabara nyingine baada ya hapo. Kwa kuwa sasa UDA haina mpinzani katika sekta ya usafirishaji nchini, naamini tutashinda zabuni ya kuendesha,” alisema. Aliongeza kuwa mradi huo unatarajia kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 1,500.
Picture
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group,Robert Kisena (wa pili kulia) Wawekezaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA akipokea mfano wa funguo kutoka kwa Meneja wa Biashara wa TATA Afrika Holding Tanzania Ltd,Srinivas Nemalapuri (wa pili kushoto) kulia ni Mkurugenzi wa Simon Group, Leonard Rubuye na kushoto Kaimu Meneja Biashara,Sarvan Keshri. ikiwa ishara makabidhiano ya mabasi 15 katika awamu ya kwanza, hafla hiyo ilifanyika kwenye Ofisi za UDA Dar es Salaam.
Picture
Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group,Robert Kisena (wa nne kushoto) akiwaongoza viongozi wengine ndani ya Basi la UDA.



Thursday, October 4, 2012

BAADA YA RAFU MBAYA YA BOBAN, YONDANI AANZA MATIBABU MUHIMBILI (MOI)



Mlinzi wa kati ya timu ya Young Africans, Kelvin Yondani
























Mlinzi wa kati wa kutumainiwa wa klabu ya Young Africans na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Kelvin Yondani anaendelea vizuri mara baada ya kuanza kupata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha mifupa MOI jijini Dar es salaam.
Daktari wa timu ya Young Africans Dokta Suphian Juma, amesema Yondani alipata mshtuko katika mfupa wake mkubwa, baada ya kuchezewa vibaya na kiungo wa timu ya Simba Haruna Moshi 'Boban'.
Dr Suphian anatoa wasi wasi wapenzi na washabiki wa Young Africans, kwamba Yondani anaendelea vzuri na anatazamiwa kurudi dimbani baada ya wiki mbili. 'Unajua Yondani baada ya kukanygwa na Boban alipata mshituko katika mfupa wake mkubwa mguuni, hivyo anapata matibabu ya kumrejesha katika hali yake ya kawaida.
Katika hali ya kushangaza mwamuzi wa mchezo huo wa watani wa jadi, Mathew Akrama alishindwa kumonyesha kadi nyekundu Boban kwa mchezo mbaya uliopelekea Yondani kutolewa nje na kushidwa kuendelea na mchezo.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyowakutanisha watani wa jadi wakongwe Afrika Mashariki iliishia kwa sare ya mabao 1-1, mabao yaliyofungwa na Amri Kiemba Simba dakika ya 4 na Said Bahanunzi aliyesawazisha kwa upande wa Young Africans dakika ya 67.
Young Africans leo imeendelea na mazoezi katik uwanja wa shule ya sekeondari ya Loyola kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya timu ya Kagera Sugar, mchezo utakaofanyika siku ya jumapili katika uwanja wa kaitaba mjini Bukoba.

RAFU MBAYA YA BOBAN YAMPELEKA YONDANI HOSPITALI


Yondan wa pili kutoka kulia waliosimama katika kikosi cha Yanga jana
BEKI Kevin Yondan wa Yanga hajaamka mazoezini leo, kutokana na kuumizwa vibaya na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga wapo Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo hivi sasa wakifanya mazoezi, lakini Yondan anajiandaa kwenda hospitali kufanyiwa uchunguzi wa maumivu yake.
Habari kutoka Yanga, zimesema kwamba tangu jana beki huyo anasikia maumivu makali na hatima yake itajulikana baada ya vipimo hivyo.
Yanga jana ilitoka nyuma na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02 usiku.
Habari kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba wachezaji waliahidiwa asilimia ya 60 ya mgawo wa timu kutokana na mapato ya milangoni na asilimia 20 ya kiwango hicho kuongezwa na Friends of Simba, lakini kwa sare hiyo, ahadi hiyo imeota mbawa.
Hata hivyo, uongozi wa Simba unafikiria kuwapa ‘kifuta jasho’ wachezaji wake kwa angalau kulinda hadhi ya klabu kwa kutokubali kufungwa na wapinzani wao hao wa jadi jana.
Yanga ambao walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso, ndio waliohaha kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la kiungo Amri Kiemba.  
Hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba dakika ya pili.
Simba walicheza vizuri kipindi chote cha kwanza wakigongeana pasi za uhakika na kuwazidi kasi uwanjani wapinzani wao, wakati Yanga pamoja na kuzinduka baada ya kufungwa bao, lakini makosa yalikuwa mengi.
Pasi zao zilikuwa nyingi hazifiki, walikuwa wanapokonyeka mipira kirahisi, wanazidiwa nguvu na wapinzani wao katika kugombea mipira na hata mashambulizi yao hayakuwa ya mpangilio, zaidi ya kuonekana kubahatisha zaidi.
Katika kubahatisha huko, Mbuyu Twite alifumua shuti zuri dakika ya 38 kutoka wingi ya kulia, ambalo lilitoka nje sentimita chache.    
Kabla hata ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika, kocha Mholanzi Ernie Brandts alimtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Frank Domayo ili kuimarisha safu ya kiungo, ambayo ilionekana kuzidiwa na Simba inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick.
Kipindi cha pili, Yanga walianza na mabadiliko, kocha Ernie Brandts akimtoa kiungo Nizar Khalfan na kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu, ambaye alikwenda kuongeza nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Angalau, kipindi cha pili Yanga walionekana kucheza vizuri na kupeleka mashambulizi yenye uhai langoni mwa Simba, ingawa safu imara ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi ilikuwa kikwazo.
Katika dakika ya 63, beki Paul Ngalema aliunawa mpira katika harakati za kuokoa na refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani kiufundi na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Katika dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso, aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’. Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari refa alikwishapuliza filimbi na kumpa kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na hasira za kitoto.
Pamoja na Yanga kubaki pungufu, waliendelea kucheza vema na mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili. Refa Akrama alishindwa kuumudu mchezo na maamuzi yake mengi yalikuwa chungu kwa Yanga, mfano Haruna Moshi ‘Boban’ alipomchezea rafu mbaya beki Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake ikachukuliwa na Juma Abdul alimpoza kwa kadi ya njano.
Hakumchukulia hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana kupoteza muda tangu mwanzo, na alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.
Alipingia Abdul alikwenda kucheza beki ya kulia na Mbuyu Twite akahamia katikati kucheza na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Simba, Milovan alisema kwamba ulikuwa mchezo mzuri na Yanga walicheza vizuri, lakini timu yake ilicheza vizuri na anajivunia. Alisema Yanga imeimarika tofauti na ilivyokuwa awali na kwamba hizo ni dalili Ligi Kuu msimu huu itakuwa ngumu.
Kwa upande wake, kocha wa Yanga, mwanzoni hawakucheza vizuri, lakini baadaye walitulia na kucheza vizuri. “Hii ni mechi ya kweli ya upinzani, unaweza kuona rafu na kadi nyingi,”alisema Brandts.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 13, ndani ya mechi tano na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, wakati Yanga imefikisha pointi nane na kubaki nafasi ya tano, kwani Coastal Union imetoa sare ya 2-2 na JKT Oljoro mjini Arusha na kufikisha pointi tisa.   
SIMBA: Juma Kaseja, Nassor Chollo, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Shomary Kapombe, Jonas Mkude/Haruna Moshi, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Edward Christopher/Daniel Akuffo na Mrisho Ngassa.
YANGA: Yaw Berko, Mbuyu Twite, Stefano Mwasyika, Nadir Cannavaro, Kevin Yondan/Juma Abdul, Athumani Iddi, Simon  Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza/Frank Domayo na Nizar Khalfan/Didier Kavumbangu.


KIBONZO CHA LEO




HUU NDIO UDHAIFU MWINGINE WA TFF

Pichani ni sehemu ya paa la chumba cha habari cha chama cha mpira wa miguu Tanzania (TFF),ambacho kinatumika kukutana na Wanahabari wa vyombo mbalimbali kuhusiana tasnia ya michezo kwa madhumuni ya kuihabarisha jamii.Kwa wanahabari za Michezo naamini kabisa mtakubaliana na mimi kuhusiana na hali iliyopo ndani ya ofisi hiyo,ambayo kimsingi nayo una umuhimu wake mkubwa,lakini imetelekezwa kama hivyo.
Chombo cha kutoa ubaridi ambacho kiliwekwa angalau kupunguza joto la Daslam ofisini humo,lakini kwa sasa ndege wamepata mahala pa kujipumzikia na kuzaliana,lakini sio ishu.
Taa nazo ziko hoi zinaning'inia tu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa watu.
Baadhi ya Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakisubiri wahusika wa TFF, kukutana na Wanahabari hao kwa ajili ya kuwapa taarifa mbalimbali za michezo, ili jamii ihabarishwe.
Dude la kuwekea Maji ya Kunywa ambalo sijui kwa mara ya mwisho lilitumika lini,kwani limejaa vumbi, haliangaliwi tena.



HII NDIO MBINU MPYA YA KUTOROSHA MADINI

WIZARA ya Nishati na Madini imegundua ‘madudu’ katika sekta ya madini, ikiwamo utoroshaji wa madini ya tanzanite kwa punda na ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na kampuni za migodi nchini.

Kutokana na hilo, imefanya marekebisho ya mifumo ya ulipaji kodi iliyowezesha kulipwa kwa baadhi ya madeni na imetangaza Mtanzania yeyote, ikiwamo mfanyakazi wa mgodi atakayetoa taarifa za utoroshaji wa madini, atapewa asilimia 30 ya thamani ya mzigo utakaokuwa umetoroshwa.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza katika uzinduzi wa Kitabu cha Ripoti inayohusu Haki za Binadamu katika Kazi, Biashara, Mazingira, Ardhi, Ulinzi na Haki ya Mlaji.

Hafla hiyo iliandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na yeye alikuwa mgeni rasmi.

Akizungumza kabla ya uzinduzi wa ripoti hiyo iliyoelezea ukiukwaji mkubwa wa haki za wafanyakazi katika kampuni za madini nchini na uharibifu wa mazingira uliobainika, Masele alikubaliana nayo na kueleza jinsi Serikali ilivyojipanga kukabiliana na kadhia hiyo.

“Kuna ‘madudu’ mengi na makubwa yanafanyika, rasilimali za nchi hii zinatoroshwa na kuyeyuka, tumegundua kule Manyara madini pekee yanayopatikana Tanzania tu ulimwenguni kote-tanzanite yanatoroshwa kwa punda, hii haiwezekani kukaa kimya, wezi wa mali zetu ni Watanzania wenyewe, tubadilike,” alisema Masele na kuongeza: “Kuna watu wanapewa asilimia 10 ya madini yanayotoroshwa, tumegundua hilo pia sasa tumesema mwananchi au mfanyakazi atakayegundua utoroshaji na kutoa taarifa kwetu, tutampa asilimia 30 ya fedha ambayo ni thamani ya mali aliyookoa”.

Akisisitiza ukwepaji kodi, alisema: “Tena nitoe onyo kwa kampuni zinazokwepa kodi na kukiuka haki za binadamu hasa katika sekta inayosimamiwa na wizara yetu, waache mara moja maana kuna mapinduzi makubwa yanafanyika sasa na hatutasita kuyafutia leseni mara moja”.

Masele alisema walibaini kampuni zote za madini nchini zikikwepa baadhi ya kodi kupitia uandikaji wa nyaraka zao na sasa wamezibaini na kuanza kulipa madeni hayo.

Alitoa mfano kampuni ya Barrick katika ukokotoaji wa hesabu, ilibainika kuwa na deni la zaidi ya Sh bilioni 5.6 na hadi sasa imelipa Sh bilioni 2.3; nyingine ni TanzaniteOne inayodaiwa zaidi ya dola za Marekani milioni 2.5.

“Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) ilikuwa inadaiwa zaidi ya dola milioni 1.4 ambazo sasa imeanza kuilipa Halmashauri ya Geita, niseme tu kuna mapinduzi makubwa na tunaamini Watanzania wako nyuma yetu hatuogopi,” alisema Masele.

Kuhusu TanzaniteOne, alisema leseni yake imekwisha tangu Agosti na Serikali imesitisha kuipa leseni nyingine mpaka mpango wa kurejesha asilimia 50 ya hisa serikalini ili kuondoa umiliki binafsi uliopo sasa na masuala mengine ya utendaji vitakapokaa vizuri.

Alisema katika kuhakikisha kuna usimamizi mzuri wa kodi na rasilimali za madini, mafuta na gesi nchini, Wizara inafanya mapinduzi makubwa katika taasisi zake kwa kufumua Bodi, kupanga mifumo na kuongeza nguvu ya kiutendaji ya rasilimali watu.

Masele alisema miongoni mwa Bodi zitakazofumuliwa ni pamoja na ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ili kuongeza usimamizi katika sekta ya madini, pia itafanya marekebisho makubwa ya utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC).

Alisema lengo la wizara ni kutekeleza malengo ya kiuchumi ya mwaka 2020 hadi 2025 ya nchi kuwa katika uchumi wa kati kwa kutumia rasilimali zake hasa madini, gesi na mafuta na kusisitiza kuwa hawataacha kuwachukulia hatua wezi wa rasilimali, waharibifu wa mazingira na ardhi.

Alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wanaharakati wa haki za binadamu, kwamba Serikali inawatambua na haipingi kukosolewa, lakini kwenye pongezi ipewe, huku akiwahakikishia kuwa utafiti wao ni moja ya zana za kuendeleza utendaji unaoendelea hivi sasa katika sekta mbalimbali.

Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwa kuonesha matumaini mapya kwa wananchi, hasa usalama wao katika maeneo ya kazi kwenye migodi na kampuni za uwekezaji.

Kuhusu ripoti ya utafiti, Kijo- Bisimba alisema utafiti ulifanyika nchi nzima na kugundua ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wafanyakazi wa migodini, ujira mdogo na usalama kazini, uharibifu wa mazingira na ardhi.

“Ilizoeleka katika nchi nyingi, kwamba walaumiwa wa ukiukaji wa haki za binadamu ni Dola, lakini sasa hali hiyo imebadilika, sekta binafsi inashiriki katika ukiukaji wa haki za binadamu kupitia mifumo yao ya utendaji na kukwepa kulipa kodi,” alisema Dk Kijo-Bisimba.

Akitoa takwimu, Wakili na Mratibu wa Uwajibikaji wa Kampuni na Mazingira wa LHRC, Flaviana Charles alisema wafanyakazi asilimia 15.77 waliohojiwa walikiri kuwapo na ukiukwaji wa haki za binadamu migodini na ujira mdogo, hakuna haki ya kujumuika (kuwa na vyama vya wafanyakazi).

“Pia asilimia 28.22 ya kampuni hazina sera ya kuzuia ajira kwa watoto na asilimia 4.62 ya kampuni hazishirikishi wananchi kuchukua ardhi ya uwekezaji, pia watu hawajui haki zao wanapouziwa bidhaa bandia,” alisema Charles.

LHRC waliiomba Serikali kuhakikisha pia kuwa familia 20 zinazoishi katika mahema Geita zilizopisha mradi wa GGM, zinajengewa nyumba. Naibu Waziri Masele alisema tayari GGM imekubali kujenga nyumba hizo.

Kwa mujibu wa LHRC, utafiti huo ni wa kwanza wao kuufanya nchini kuhusu masuala ya haki za wafanyakazi, mlaji, ardhi, mazingira na ulinzi.



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU