Facebook Comments Box

Tuesday, December 16, 2014

RASMI: YANGA WAMTIMUA MAXIMO

Pita hivi: askari akimuelekeza maxio Maximo uwanja wa ndege
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,

Baada ya kuchapwa mabao 2-0 na mahasimu wao wa soka Simba SC katika mchezo wa ‘ Hisani Nani Mtani Jembe’ siku ya Jumamosi iliyopita, klabu ya Yanga SC imeamua kufikia maamuzi magumu ya kumfuta kazi kocha Marcio Maximo na ni wazi Mholanzi, Hans Van De Pluijm atachukua nafasi hiyo. 

Hii ni mara ya pili kwa Yanga kumfukuza kazi kocha wao mara baada ya kufungwa na Simba. Ikumbukwe mwaka uliopita, Mholanzi, Ernie Brandts aliondoshwa baada ya kufungwa mabao 3-1 katika Mtani Jembe.

Tofauti na ilivyokuwa kwa Brandts ambaye aliifundisha Yanga kwa mwaka mmoja na kuisaidia kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/13, Maximo yeye amefukuzwa baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo tisa ndani ya miezi mitatu. 

Yanga imepoteza michezo miwili kati ya saba ya ligi kuu msimu huu, Maximo ambaye alianza vizuri klabuni hapo kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii, alipoteza mchezo wa kwanza tu wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Yanga imeshinda michezo minne msimu huu, lakini hadi l,igi inasimama katika raundi ya saba hakuna mtu alikuwa na shaka kuhusu uwezo wa Maximo. Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa
ya Tanzania, Taifa Stars amechokwa haraka sana na mashabiki, wapenzi, wanachama na viongozi wa klabu yake kutokana na kiwango kidogo cha uchezaji. Mifumo yake ya ufundishaji imekosa mvuto, lakini kitendo cha kufungwa kidhaifu na Simba kimeshindwa kuvumilika.

COUTINHO, JAJA, EMERSON WAMPONZA?

Ndiyo sababu kubwa, ukitoa mbinu zake, Maximo alikuwa akiwakumbatia zaidi wachezaji raia wa Brazil, Andrey Coutinho, Geilson Santos ( ambaye aliomba mwenyewe kuachwa baada ya michezo saba), kwa Emerson Oliveira siwezi kuzungumzia kwa sababu mchezaji huyo wa nafasi ya kiungo alicheza katika kiwango cha kawaida wakati alipoichezea Yanga kwa mara ya kwanza.

Jaja alifunga mara mbili dhidi ya Azam, ila alikosa makali katika ligi kuu kiasi cha kufunga bao moja tu katika michezo saba ya ligi kuu. Alishindwa kumudu presha ya mashabiki wa Yanga ambao hawakuwa wakipendezwa na kiwango chake huku uchezaji wake wa taratibu ukiwaboa wengi.

Maximo aliwanyima nafasi washambuaji kama Said Bahanunzi, Jerry Tegete, Saimon Msuva, Hussein Javu na Hamis Kizza hata pale wachezaji hao wa Kibrazil waliposhindwa kufanya vizuri.
Kuwang’ang’ania wachezaji hao na kuwanyima nafasi wale wenye uwezo kumewakera . Brandts aliondolewa baada ya kufungwa 3-1 licha ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili zaidi, yeye aliondolewa kwa kuwa alipingana na uamuzi wa viongozi kuwasajili baadhi ya wachezaji ambao hakuwataka wakati ule.
Brandts ndiye mwalimu aliyeifanya Yanga kucheza mchezo mzuri wa kupasiana na ndiye aliyeimarisha kiwango cha wachezaji kama, Saimon Msuva, Frank Domayo ( yuko Azam FC kwa sasa), Juma Abdul, Oscar Joshua na wengineo lakini kwa Maximo imekuwa ni tofauti,
wachezaji wengi wameshuka viwango na
ameshindwa kuwaimarisha wachezaji ambao ‘ wanasua-sua’. 

Yanga wamefanya uamuzi sahihi kwa kumuondoa Maximo na Coutinho.

Ahsante: Shaffih Dauda


Monday, December 15, 2014

BREAKING NEWS: HAMIS TAMBWE ASAJILIWA NA YANGA

Hamis Tambwe akisaini

 Akihojiwa na kipindi cha sports bar cha clouds tv Hamis Tambwe amekubali kuwa amesaini Yanga



MWANAMUZIKI MKONGWE WA BENDI YA TABORA JAZZ AFARIKI DUNIA


 Shem Karenga wapili kutoka kushoto waliosimama.

 Shem Ibrahim Karenga, mkongwe wa muziki wa dansi Alizaliwa mwaka 1950, Bangwe, Kigoma na kupata elimu ya msingi katika shule ya kimishionari ya Kihezya kuanzia mwaka 1957 hadi mwaka 1964.

“Kiukweli, nilianza kujifunza muziki tangu nikiwa shuleni kwa sababu mimi nimesoma shule ya Wamishionari, sasa kule tulikuwa tukifundishwa fani hiyo,” ndivyo anavyoanza kusema Karenga.

Karenga anasema kuwa, baada ya kumaliza shule huku shetani muziki akiwa kampanda kichwani, mwaka 1964 alijiunga na bendi ya Lake Tanganyika Jazz ambayo maskani yake yalikuwa mjini Kigoma.
 
Anakumbuka kuwa, aliingia Lake Tanganyika akiwa mwimbaji na mcharazaji wa gitaa la besi, ambako pia alikuwa na ujuzi wa kutengeneza gitaa kwa kutumia vifaa vya kuokoteza. Akiwa na Lake Tanganyika Jazz, aliyodumu nayo kwa miaka minane, alianza pia kujifunza vyombo vingine vya muziki kama vile; Drums, Kinanda, gitaa la Rithym na la Solo’.
 
“Mwaka 1972, aliitwa kwenye bendi ya Tabora Jazz kama mwanamuziki mwenye kipaji cha utunzi, mwimbaji na mpigaji wa gitaa la Solo, alijiunga na Tabora Jazz akiwa na vibao vyake Dada Asha na Lemmy alivyovitungia Lake Tanganyika, ambavyo vilimpa umaarufu mkubwa alipo vipakua hapo Tabora Jazz'.
 
 Anasema, Tabora jazz walimchukua akiwa Mtaalam wa muziki, ambako hata hivyo alipokuwa na bendi hiyo alikuwa akijiendeleza zaidi kwa masomo ya jioni kwenye shule ya Sekondari ya Milambo, Tabora pamoja na kusoma vitabu mbalimbali vya muziki.

Katika bendi ya Tabora Jazz ambako alikuwa pia kama Kiongozi wa bendi, Karenga alikutana na wakali wengine wa muziki kama vile Kassim Kaluona na Athuman Tembo ambao kwa sasa ni marehemu pamoja na Salum Muzila.

Kutokana na sababu binafsi ambazo hakutaka kuziweka wazi, mwaka 1983 alijiengua kutoka Tabora Jazz na kusimama kabisa kujihusisha na muziki, ambako kilichofuatia ilikuwa ni kifo cha bendi hiyo.

“Mwaka 1990 aliondoka Tabora na kutua jijini Dar es Salaam alipokutana na Baraka Msilwa katika mwaka huohuo na kuniomba nijiunge na MK Beats ili kuiongezea nguvu,” anasema Kalenga.

Ndani ya MK Beats iliyokuwa ndugu na bendi nyingine iliyotamba vilivyo enzi hizo, MK Group, Karenga alikutana na wakali kama Malik Star, Sisko Lulanga, Fungo Shomari na Bwami Fanfan.

Baada ya kujiunga na MK Beats iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Tukunyema’, Karenga aliisuka vema na kuinyanyua vilivyo hasa kwa vibao moto wa kuotea mbali vilivyozitetemesha vikali bendi nyingine
zote za wakati huo.

Mwaka 1995, MK Beats ilisambaratika, ambako mwaka uliofuata, yaani 1996 alianzisha bendi ya Tabora Jazz Star kwa kushirikiana na mtu aliyemtaja kwa jina la Ibrahim Didi.

“Bendi ya Tabora Jazz Star ndio niliyo nayo hadi sasa nikiwa Mkurugenzi Msaidizi, ambako nafasi ya Mkurugenzi Mkuu imeshikiliwa na Didi mwenyewe,” alisema Karenga.

Akizungumzia anavyouona ushindani wa kimuziki akiwa na bendi yake hiyo ya Tabora Jazz Star, Karenga alisema kwa upande wake mambo si mazito sana kwa kuwa ana mashabiki wake wa tangu huko nyuma.

Kwa upande wa mafanikio, Karenga anasema ukiondoa nyumba nzuri aliyoiporomosha nyumbani kwao Kigoma, anashukuru kuona ana marafiki wengi na anaishi atakavyo akiwa anamudu vema kuitunza familia yake.

Ushauri alioutoa kwa wanamuziki na mashabiki wa dansi ni kuwa, wasibabaike kwani muziki huo ni wa kudumu, ambako hata hivyo alisikitika kuona kuna uhaba mkubwa wa vijana warithi wa miondoko hiyo
kwa sasa.

“Unajua, sisi tulirithi dansi kutoka kwa baba, kaka na wakubwa zetu wengine, lakini ni masikitiko makubwa kuona vijana wetu wa sasa wanarithi muziki hewa wa Bongo Fleva,” alisema.

Alisema, sababu ya kuuita muziki wa Bongo Fleva kuwa hewa ni namna wasanii wake wanavyopora midundo na ala kutoka nje huku wakijidai kuwa ni mtindo mpya wa muziki hapa nchini.

Mkongwe huyo aliyebainisha siri yake ya kukubalika katika muziki kuwa ni bidii na juhudi za dhati kwenye fani hiyo, alisema anavutiwa na wasanii wote wanaofanya vema katika sanaa.

Kama ilivyo kwa wakongwe wengine wengi wa muziki, Karenga alifaulu kuwarithisha muziki watoto wake wawili wa kiume ambao ni Ramadhan na Mussa waliowahi kuwika vilivyo katika bendi ya TOT Plus.

“Mussa ni mwimbaji na rapa mahiri, ambako kaka yake, Ramadhan ni mcharazaji wa gitaa kiongozi, Solo,” anasema Karenga, baba wa watoto sita.

Watoto wengine wa Karenga ambao hawakubahatika kurithi kazi yake ya muziki ni Tausi, Biata pamoja na Rehana.




BREAKING NEWS: PRUIJM KUREJEA KUINOA YANGA

kocha Mdachi Hans Van Der Pruijm huenda akarejea nchini kuifundisha tena YANGA,kutoka chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kinasema kocha huyo wa zamani wa klabu hiyo huenda akawasili usiku wa leo kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya awali.

Mwishoni mwa juma hili kwenye mchezo wa NANI MTANI JEMBE Yanga ilifungwa na mtani wake wa jadi Simba mabao 2-0 huku timu hiyo inayonolewa na Mbrazil Marcio Maximo ikionyesha kiwango cha kawaida kwenye mchezo huo ikilinganishwa na kipindi cha mdachi huyo.
AHSANTE: SHAFFIH DAUDA


Friday, December 12, 2014

KIIZA ATUPWA NJE YANGA

Hamisi Kiiza "Diego "
Taarifa za kuaminika ambazo tumezipa hivi punde, klabu ya Yanga ipo mbioni kukatisha mkataba na mshambuliaji Hamis Kiiza raia wa Uganda.

Mmoja wa watu ambao wanashughulika na usajili wakati akiongea na mtandao huu amesema

‘’Tutakaa chini kuzungumza na Kiiza ili kuangalia namna ya kuachana kwa amani,baada ya Mliberia kufuzu vipimo vya afya hatuna jinsi lazima tuliondoe jina la Kiiza kwenye usajili wetu,kilisema chanzo hicho ‘’

Yanga inalazimika kupunguza mchezaji mmoja wa kigeni hasa baada ya mshambuliaji Kpah Sean Sherman kufuzu vipimo vya afya na kuwa mbioni kusaini mkataba na klabu hiyo.

Hivi karibuni Yanga ilimsainisha kiungo Emerson toka nchini Brazil mkataba wa mwaka mmoja, ukiachana na Kiiza wachezaji wengine wa kigeni ndani ya klabu ya Yanga ni Mbuyu Twite,Haruna Niyonzima, Kpah Sean Sherman na wabrazil Courtinho na Emerson.

Ikumbukwe Idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa na timu ni watano.


Thursday, December 11, 2014

DAVIDO AMWAMBIA DIAMOND AWE NA SHUKRANI

DAVIDO AND DIAMOND
Huhitaji kujifikiria mara mbili kuamini kuwa Davido na Diamond haziivi tena kwa sasa!

Yote yalianza baada ya Davido kutweet ‘N they cheat again, Lol’ baada ya Idris kutangazwa mshindi wa Big Brother Hotshots. Tweet hiyo ikimfanya Davido atukanwe matusi ya kila aina kutoka kwa Watanzania.

Usiku huo huo, Diamond alishinda tuzo za TFA (The Future Awards) za Nigeria na kuandika:

Thanks God, we have cheated another one on The.Future Awards Africa in Lagos Nigeria… #SameDay.#SameNight Thank you Allah.”

Ujumbe huo moja kwa moja ukaashiria kuwa jibu kwa.Davido ambaye matusi kutoka Tanzania yaliendelea kumsakama.

Baadaye, Davido anayeaminika (na huo ndio ukweli) kuwa msanii aliyesaidia kumtambulisha Diamond kimataifa, aliandika ujumbe kwenye Twitter. unaoshiria kumlenga Diamond.

An ungrateful stone will eventually fall… I will always be grateful to pple that have helped me climb this tall ladder of success,” alitweet Davido.

Tweet hiyo ilimaanisha: Jiwe lisilo na shukrani hatimaye huanguka… Nitakuwa mwenye shukrani siku zote kwa watu walionisaidia kuipanda ngazi ya mafanikio.”

Hata hivyo naye Diamond alitumia siku ya Uhuru wa Tanganyika jana kutoa nasaha zake kuhusiana na mikwaruzano baina ya wasanii wa Afrika kwa kuandika:

Badala ya wasanii kuwa ndio mfano bora wa kuweka karibu nchi zao na kujenga Afrika yenye upendo na amani…eti wao ndio wanakua chanzo cha kutenganisha nchi zao. Namna hii kweli tutajenga Afrika? Anyway, Happy Independence day Tanzania.”

 Thanks: BongoClan


Tuesday, December 9, 2014

BREAKING NEWS: KUNA MAPIGANO KATI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI DUMILA

Abiria wakishirikiana na polisi kuzima moto uliowashwa barabarani

Polisi wa kutuliza ghasia wakielekea kwenye tukio
Yametokea mapigano kati ya wakulima na wafugaji dumila mkoani morogoro. Magari yamesimama hayaendi morogoro na wala ya morogoro hayaendi dodoma.

Polisi wa kutuliza ghasia (FFU)  wameelekea huko kutuliza ghasia hizo.

kwenye moshi ndio eneo la mapigano

Foleni ya magari iliyosababishwa na mapigano hayo

 



DANNY MRWANDA ASAINI YANGA KWA MKATABA WA MWAKA MMOJA

Mchezaji Danny Mrwanda amesaini kuitumikia klabu ya Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja. Mkataba huo umesainiwa jana usiku.
Danny Mrwanda akiweka saini katika mkataba



Friday, December 5, 2014

MWANAFUNZI KCMC ATUPA KICHANGA KWENYE PIPA LA TAKA

MWANAFUNZI wa mwaka wa kwanza shule ya viungo KCMC mjini Moshi  mkoani Kilimanjaro, Rachel Malima (22), amewekwa chini ya uangalizi maalumu wa madaktari baada ya kujifungua na kumtelekeza mtoto kwenye pipa la kuhifadhia takataka katika vyoo vya hospitali hiyo.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Ofisa Uhusiano wa hospitali ya KCMC, Gabriel Chiseo, alikiri kutokea kwa tukio hilo juzi baada ya mwanafunzi huyo kushikwa uchungu wa kujifungua.

Alibainisha kuwa, Malima alifika hospitalini hapo akiwa na wenzake na kupokelewa na wahudumu wa mapokezi na kuwekwa mapumziko wodini kabla ya muda mfupi kuomba kwenda msalani kujisaidia na kuruhusiwa.

Alieza kuwa, baada ya kufika msalani ndipo alipojifungua mtoto huyo na kumweka katika pipa la takataka na kutokomea kusikojulikana.

Inaelezwa kuwa, mara baada ya kuondoka mmoja wa wafanya usafi hospitalini hapo, aliingia msalani kwa ajili ya kuhakiki usafi na ndipo alipokuta choo kikiwa kimetapakaa damu na alipofungua pipa la takataka alikuta kichanga kikiwa na mfuko wa uzazi (Placenta), kinatupa tupa mikono na miguu na mdomoni kimesokomezwa taulo ya kike (Pad), ili sauti isisikike.

Chiseo, alisema jitihada za kumtafuta na kumkamata zilifanyika na hivi sasa yupo chini ya uangalizi maalum wa madakatari wa hospitali hiyo kwa ajili ya kumjenga kisaikolojia ili aweze kuhojiwa sababu ya kufanya hivyo.

“Hivi sasa Malima yupo chini ya uangalizi maalum, mtoto anaendelea vizuri  lakini pia bado tukio hilo halijaripotiwa polisi ila lipo chini ya kitengo cha uastawi wa jamii wa hospitali ambao watajua ni nini kitafuata baada ya Malima kupata nafuu,” alisisitiza Ofisa Habari huyo.

Kukamatwa kwa mwanafunzi huyo, kulitokana na jitihada za mashuhuda wa tukio hilo na uongozi wa KCMC, ambao walimwona Malima akiingia hospitalini hapo akiwa na baibui na alitoka akiwa anachechemea huku akiwa amesaidiwa mkoba na mtu ambaye hadi sasa hajafahamika.

CHANZO: TANZANIA DAIMA



Saturday, November 29, 2014

HAYA NDIO MAAZIMIO YA BUNGE JUU YA ESCROW

MAAZIMIO YA BUNGE KUHUSU HOJA YA TAARIFA MAALUM YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI 

MAALUM KUHUSIANA NA MIAMALA ILIYOFANYIKA KATIKA AKAUNTI YA ‘ESCROW’ YA TEGETA

PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL

_____________________________________

 

1.    KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi Maalum wa Malipo yaliyofanyika katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (‘CAG’) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (‘TAKUKURU’) imeonesha kwamba kwamba Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira (VIP), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (‘TANESCO’) walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda kwa makampuni ya Pan African Power Solutions Ltd. (‘PAP’), na VIP Engineering & Marketing (‘VIP’);

KWA KUWA, kwa sababu ya kuhusika kwa watu hao na miamala iliyofanyika kwenye Akaunti ya Escrow imeliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya fedha za umma zinazotokana na kutokulipwa kwa kodi mbali mbali za Serikali na kushindwa kwa TANESCO kukokotoa upya kiwango cha malipo ya gharama za uwekezaji (‘capacity charges’) wa IPTL;

KWA KUWA, mabilioni ya fedha yaliyotolewa kwenye Akaunti ya Escrow yametumika kuwapa kile kinachoonekana kuwa ni rushwa baadhi ya viongozi na maafisa wa serikali kama vile Mawaziri, Majaji, Wabunge, Wenyeviti wa Kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.

NA KWA KUWA, vitendo vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria makosa mbali mbali ya jinai kama vile uzembe, wizi, ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, TAKUKURU, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na Taarifa Maalum ya Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea;

2.    KWA KUWA, vitendo vya kijinai wanavyhohusishwa navyo viongozi wa umma na maafisa wa ngazi za juu serikalini vinakiuka pia maadili ya viongozi wa umma na kuwanyima viongozi na maafisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao;

3.    KWA KUWA, katika watu walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge kama vile Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO;

NA KWA KUWA, Bunge na/au Kamati zake za Kudumu zina uwezo na mamlaka, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, ya kuwawajibisha viongozi hawa wa Kamati kwa kuwavua nyadhifa zao;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka, na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao Wenyeviti tajwa wa Kamati husika za Kudumu za Bunge;

4.    KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba katika watu waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania;

KWA KUWA, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (‘Katiba’) imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia nidhamu ya Majaji;

KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Majaji;

NA KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji au Majaji husika wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania;

5.    KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. ilishiriki kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwa njia haramu kutoka katika Akaunti ya Escrow na kupelekwa katika akaunti zilizofunguliwa na PAP katika benki hiyo;

KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba akaunti za PAP  katika Stanbic Bank Tanzania Ltd. zimekwishafungwa baada ya fedha zote zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kumalizika na Akaunti ya ya VIP katika Mkombozi Commercial Bank imebakiza kiasi fulani cha fedha;

NA KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba kuna uwezekano fedha zilizotolewa kutoka kwenye akaunti za PAP na VIP zilipelekwa katika benki nyingine;

NA KWA KUWA, vitendo vya Stanbic Bank (Tanzania) Ltd., na benki nyingine kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwenye Akaunti ya Escrow ni vitendo vya jinai kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi ziitaje Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. na benki nyingine yoyote itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (institutions of money laundering concern);

6.    KWA KUWA, vitendo vya wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, hujuma ya uchumi na ufisadi vimeongezeka, kushamiri na kushirikisha viongozi wa kisiasa na maafisa wa serikali pamoja na wafanya biashara wakubwa;

KWA KUWA, kwa mujibu wa sheria iliyoiunda, TAKUKURU inashughulikia vitendo vya aina zote za rushwa zikiwemo rushwa ndogo ndogo (petty corruption) na rushwa kubwa na ufisadi (grand corruption) na matumizi mabaya ya madaraka;

NA KWA KUWA, kwa sababu ya majukumu yake mapana kisheria, TAKUKURU inaelekea kuelemewa katika vita ya kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa letu kiuchumi, kijamii na kisiasa;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya Sheria iliyoiunda TAKUKURU kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa;

7.    KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha jinsi ambavyo TANESCO imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya Shirika hilo;

KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba TANESCO itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo wa IPTL;

HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.

8.    KWA KUWA, kwa miaka mingi mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya TANESCO na makampuni binafsi ya kufua umeme imeisababishia TANESCO hasara ya mabilioni ya fedha na hivyo kutishia uhai wake wa kifedha;

KWA KUWA, Bunge lilikwishaazimia kwamba serikali iwasilishe mikataba husika Bungeni au kwenye Kamati zake kwa lengo la kuliwezesha Bunge kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri serikali;

NA KWA KUWA, Serikali haijatekeleza Azimio hilo la Bunge hadi sasa;

HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.

Imewasilishwa leo hii tarehe 28 Novemba, 2014.

------------------------------------------------------

ZITTO ZUBERI KABWE (MB)

MWENYEKITI

KAMATI YA PAC



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU