Facebook Comments Box

Thursday, December 11, 2014

DAVIDO AMWAMBIA DIAMOND AWE NA SHUKRANI

DAVIDO AND DIAMOND
Huhitaji kujifikiria mara mbili kuamini kuwa Davido na Diamond haziivi tena kwa sasa!

Yote yalianza baada ya Davido kutweet ‘N they cheat again, Lol’ baada ya Idris kutangazwa mshindi wa Big Brother Hotshots. Tweet hiyo ikimfanya Davido atukanwe matusi ya kila aina kutoka kwa Watanzania.

Usiku huo huo, Diamond alishinda tuzo za TFA (The Future Awards) za Nigeria na kuandika:

Thanks God, we have cheated another one on The.Future Awards Africa in Lagos Nigeria… #SameDay.#SameNight Thank you Allah.”

Ujumbe huo moja kwa moja ukaashiria kuwa jibu kwa.Davido ambaye matusi kutoka Tanzania yaliendelea kumsakama.

Baadaye, Davido anayeaminika (na huo ndio ukweli) kuwa msanii aliyesaidia kumtambulisha Diamond kimataifa, aliandika ujumbe kwenye Twitter. unaoshiria kumlenga Diamond.

An ungrateful stone will eventually fall… I will always be grateful to pple that have helped me climb this tall ladder of success,” alitweet Davido.

Tweet hiyo ilimaanisha: Jiwe lisilo na shukrani hatimaye huanguka… Nitakuwa mwenye shukrani siku zote kwa watu walionisaidia kuipanda ngazi ya mafanikio.”

Hata hivyo naye Diamond alitumia siku ya Uhuru wa Tanganyika jana kutoa nasaha zake kuhusiana na mikwaruzano baina ya wasanii wa Afrika kwa kuandika:

Badala ya wasanii kuwa ndio mfano bora wa kuweka karibu nchi zao na kujenga Afrika yenye upendo na amani…eti wao ndio wanakua chanzo cha kutenganisha nchi zao. Namna hii kweli tutajenga Afrika? Anyway, Happy Independence day Tanzania.”

 Thanks: BongoClan


Tuesday, December 9, 2014

BREAKING NEWS: KUNA MAPIGANO KATI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI DUMILA

Abiria wakishirikiana na polisi kuzima moto uliowashwa barabarani

Polisi wa kutuliza ghasia wakielekea kwenye tukio
Yametokea mapigano kati ya wakulima na wafugaji dumila mkoani morogoro. Magari yamesimama hayaendi morogoro na wala ya morogoro hayaendi dodoma.

Polisi wa kutuliza ghasia (FFU)  wameelekea huko kutuliza ghasia hizo.

kwenye moshi ndio eneo la mapigano

Foleni ya magari iliyosababishwa na mapigano hayo

 



DANNY MRWANDA ASAINI YANGA KWA MKATABA WA MWAKA MMOJA

Mchezaji Danny Mrwanda amesaini kuitumikia klabu ya Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja. Mkataba huo umesainiwa jana usiku.
Danny Mrwanda akiweka saini katika mkataba



Friday, December 5, 2014

MWANAFUNZI KCMC ATUPA KICHANGA KWENYE PIPA LA TAKA

MWANAFUNZI wa mwaka wa kwanza shule ya viungo KCMC mjini Moshi  mkoani Kilimanjaro, Rachel Malima (22), amewekwa chini ya uangalizi maalumu wa madaktari baada ya kujifungua na kumtelekeza mtoto kwenye pipa la kuhifadhia takataka katika vyoo vya hospitali hiyo.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Ofisa Uhusiano wa hospitali ya KCMC, Gabriel Chiseo, alikiri kutokea kwa tukio hilo juzi baada ya mwanafunzi huyo kushikwa uchungu wa kujifungua.

Alibainisha kuwa, Malima alifika hospitalini hapo akiwa na wenzake na kupokelewa na wahudumu wa mapokezi na kuwekwa mapumziko wodini kabla ya muda mfupi kuomba kwenda msalani kujisaidia na kuruhusiwa.

Alieza kuwa, baada ya kufika msalani ndipo alipojifungua mtoto huyo na kumweka katika pipa la takataka na kutokomea kusikojulikana.

Inaelezwa kuwa, mara baada ya kuondoka mmoja wa wafanya usafi hospitalini hapo, aliingia msalani kwa ajili ya kuhakiki usafi na ndipo alipokuta choo kikiwa kimetapakaa damu na alipofungua pipa la takataka alikuta kichanga kikiwa na mfuko wa uzazi (Placenta), kinatupa tupa mikono na miguu na mdomoni kimesokomezwa taulo ya kike (Pad), ili sauti isisikike.

Chiseo, alisema jitihada za kumtafuta na kumkamata zilifanyika na hivi sasa yupo chini ya uangalizi maalum wa madakatari wa hospitali hiyo kwa ajili ya kumjenga kisaikolojia ili aweze kuhojiwa sababu ya kufanya hivyo.

“Hivi sasa Malima yupo chini ya uangalizi maalum, mtoto anaendelea vizuri  lakini pia bado tukio hilo halijaripotiwa polisi ila lipo chini ya kitengo cha uastawi wa jamii wa hospitali ambao watajua ni nini kitafuata baada ya Malima kupata nafuu,” alisisitiza Ofisa Habari huyo.

Kukamatwa kwa mwanafunzi huyo, kulitokana na jitihada za mashuhuda wa tukio hilo na uongozi wa KCMC, ambao walimwona Malima akiingia hospitalini hapo akiwa na baibui na alitoka akiwa anachechemea huku akiwa amesaidiwa mkoba na mtu ambaye hadi sasa hajafahamika.

CHANZO: TANZANIA DAIMA



Saturday, November 29, 2014

HAYA NDIO MAAZIMIO YA BUNGE JUU YA ESCROW

MAAZIMIO YA BUNGE KUHUSU HOJA YA TAARIFA MAALUM YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI 

MAALUM KUHUSIANA NA MIAMALA ILIYOFANYIKA KATIKA AKAUNTI YA ‘ESCROW’ YA TEGETA

PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL

_____________________________________

 

1.    KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi Maalum wa Malipo yaliyofanyika katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (‘CAG’) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (‘TAKUKURU’) imeonesha kwamba kwamba Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira (VIP), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (‘TANESCO’) walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda kwa makampuni ya Pan African Power Solutions Ltd. (‘PAP’), na VIP Engineering & Marketing (‘VIP’);

KWA KUWA, kwa sababu ya kuhusika kwa watu hao na miamala iliyofanyika kwenye Akaunti ya Escrow imeliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya fedha za umma zinazotokana na kutokulipwa kwa kodi mbali mbali za Serikali na kushindwa kwa TANESCO kukokotoa upya kiwango cha malipo ya gharama za uwekezaji (‘capacity charges’) wa IPTL;

KWA KUWA, mabilioni ya fedha yaliyotolewa kwenye Akaunti ya Escrow yametumika kuwapa kile kinachoonekana kuwa ni rushwa baadhi ya viongozi na maafisa wa serikali kama vile Mawaziri, Majaji, Wabunge, Wenyeviti wa Kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.

NA KWA KUWA, vitendo vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria makosa mbali mbali ya jinai kama vile uzembe, wizi, ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, TAKUKURU, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na Taarifa Maalum ya Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea;

2.    KWA KUWA, vitendo vya kijinai wanavyhohusishwa navyo viongozi wa umma na maafisa wa ngazi za juu serikalini vinakiuka pia maadili ya viongozi wa umma na kuwanyima viongozi na maafisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao;

3.    KWA KUWA, katika watu walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge kama vile Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO;

NA KWA KUWA, Bunge na/au Kamati zake za Kudumu zina uwezo na mamlaka, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, ya kuwawajibisha viongozi hawa wa Kamati kwa kuwavua nyadhifa zao;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka, na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao Wenyeviti tajwa wa Kamati husika za Kudumu za Bunge;

4.    KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba katika watu waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania;

KWA KUWA, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (‘Katiba’) imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia nidhamu ya Majaji;

KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Majaji;

NA KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji au Majaji husika wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania;

5.    KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. ilishiriki kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwa njia haramu kutoka katika Akaunti ya Escrow na kupelekwa katika akaunti zilizofunguliwa na PAP katika benki hiyo;

KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba akaunti za PAP  katika Stanbic Bank Tanzania Ltd. zimekwishafungwa baada ya fedha zote zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kumalizika na Akaunti ya ya VIP katika Mkombozi Commercial Bank imebakiza kiasi fulani cha fedha;

NA KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba kuna uwezekano fedha zilizotolewa kutoka kwenye akaunti za PAP na VIP zilipelekwa katika benki nyingine;

NA KWA KUWA, vitendo vya Stanbic Bank (Tanzania) Ltd., na benki nyingine kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwenye Akaunti ya Escrow ni vitendo vya jinai kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi ziitaje Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. na benki nyingine yoyote itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (institutions of money laundering concern);

6.    KWA KUWA, vitendo vya wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, hujuma ya uchumi na ufisadi vimeongezeka, kushamiri na kushirikisha viongozi wa kisiasa na maafisa wa serikali pamoja na wafanya biashara wakubwa;

KWA KUWA, kwa mujibu wa sheria iliyoiunda, TAKUKURU inashughulikia vitendo vya aina zote za rushwa zikiwemo rushwa ndogo ndogo (petty corruption) na rushwa kubwa na ufisadi (grand corruption) na matumizi mabaya ya madaraka;

NA KWA KUWA, kwa sababu ya majukumu yake mapana kisheria, TAKUKURU inaelekea kuelemewa katika vita ya kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa letu kiuchumi, kijamii na kisiasa;

HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya Sheria iliyoiunda TAKUKURU kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa;

7.    KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha jinsi ambavyo TANESCO imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya Shirika hilo;

KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba TANESCO itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo wa IPTL;

HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.

8.    KWA KUWA, kwa miaka mingi mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya TANESCO na makampuni binafsi ya kufua umeme imeisababishia TANESCO hasara ya mabilioni ya fedha na hivyo kutishia uhai wake wa kifedha;

KWA KUWA, Bunge lilikwishaazimia kwamba serikali iwasilishe mikataba husika Bungeni au kwenye Kamati zake kwa lengo la kuliwezesha Bunge kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri serikali;

NA KWA KUWA, Serikali haijatekeleza Azimio hilo la Bunge hadi sasa;

HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.

Imewasilishwa leo hii tarehe 28 Novemba, 2014.

------------------------------------------------------

ZITTO ZUBERI KABWE (MB)

MWENYEKITI

KAMATI YA PAC



HELKOPTA YA MALI ASILI YAANGUKA UKONGA MOMBASA

Wananchi wakiangalia helkopta hiyo
Helicopter mali ya serikali wizara ya mali asili yaanguka maeneo ya moshi bar mombasa Dar na kuua wote walio kuwemo na kuangukia nyumba za wananchi.

Polisi wameshafika eneo la tukio
Wananchi wenye nyumba hizo bado haijajulikana kama wamekufa ama hawakuwemo. Rubani na capt wa ndege hiyo inasemekana walikuwa na uzoefu mdogo sana(masaa machache sana) kutoka chuo cha 44 cha huko south African.





Thursday, November 27, 2014

SHEIKH PONDA AACHIWA HURU


APPEAL YA SHEIKH PONDA IMESOMWA AMESHINDA HUKUMU YA KUMTIA HATIANI ILIYOTOLEWA NA MAHAKAMA YA KISUTU IMEFUTWA SHEIKH YUKO HURU SASA NA WANAKWENDA MOROGORO.
Maandamano kuelekea Mtambani kuwasikiliza viongozi wa kiislamu

JAJI AMEMTANGAZA SHEIKH KUWA NI ULAMAA MKUBWA WA DINI YA KIISLAMU.

BAADA YA KUFUTIWA KESI HIYO NA KUACHIWA HURU POLISI WALIMKAMATA TENA KWA KUWA KESI YA MOROGORO BADO HAIJAISHA.


 HAWAJAWEKA WAZI KAMA KESI HIYO INA DHAMANA AU HAINA.





Sunday, November 23, 2014

TAMKO LA HIZB UT-TAHRIR JUU YA YANAYOTOKEA KENYA

Kwa mara nyengine tena Waislamu nchini Kenya   wameshuhudia uvamizi wa polisi wa misikiti miinne Sakina Musa, Swafaa na Minaa Mjini Mombasa.

Kitendo hiki cha kinyama kilichopelekea
mauaji ya mwanafunzi mmoja huku vijana wapato mia mbili na hamsini kutiwa mbaroni, kilifanywa chini ya kisingizio cha kuwafurusha vijana wenye misimamo mikali. Harakati ya Hizb
ut-Tahrir Afrika Mashariki inalaani vikali kitendo hiki na twasema yafuatayo:-

Ukatili wa polisi wa Kenya umezidi sana hasa kwa Waislamu ; Huku kukiwa kuna magenge ya-nayotekeleza mauaji kama vile Baghdad boys na Mungiki ambayo wengi ya wafuasi wake ni wakristo hatujashuhudia hata kanisa moja likivamiwa na polisi kama inavyofanywa kwa Waislamu. Bali polisi katika kuendeleza maonevu kwa Waislamu, huwapachika majina radicalists na
extremists kuhalalisha unyama wao dhidi yao. Na hii ndio sura kamili ya polisi leo ndani ya nidhamu za kibepari namna
wanavyotumiwa katika kuwafanyia unyama Waislamu. Madai ya kuwa kuna Waislamu wabaya na Waislamu wazuri
‘radicalists and moderates ni njama tu kuwagawanya Waislamu.

Na hata kama kuna tofauti baina ya Waislamu kifikra na kimisimamo,basi waachiwe wenyewe Waislamu kwani Uislamu uliwawekea utaratibu maalum wa kutatua kasoro hizo. Hivyo haijakuwa halali kwa serikali kuendeleza mateso kwa Waislamu kwa kisingizio hicho. Tunakataa miito hii pamoja na vita
kupambana na ugaidi kwani vyote hivyo ni kuushambulia Uislamu na Waislamu.

Udhalilifu huu umetokamana kukosekanwa na waakilishi wa kikweli  wa mambo ya Waislamu. Hata wale baadhi ya wanasiasa wanaojitokeza ati kukashifu unyamu huo, wao hufanya hivyo kwa lengo tu la kujitafutia umaarufu wa kisiasa. Ushahidi wa haya ni kuwa hao hao ndio huwadaa raia kuwa kushiriki kwao ndani ya nidhamu za kidemokrasia ndio njia ya kuzuia dhulma juu ya Waislamu. Na ukweli ni kuwa nidhamu za kidemokrasia ndio chanzo cha balaa zote zinazoshuhudiwa na watu wote Waislamu na wasokuwa waislamu.

Madhila haya leo ni sehemu tu ya miongoni mwa mengi yanayofanyiwa Waislamu kote dunia  na hayatokoma leo hadi pale Waislamu watapoweza kufanya kazi ya kubeba ulinganizi wa Kiislamu kwa lengo la kusimamisha utawala halisi wa Kiislamu Khilafah katika moja wapo ya nchi za Kiislamu.  Utawala huo ndio
utakaohifadhi kikweli Waislamu na Wasokuwa Waislamu na kuwakinga dhidi ya shari za maadui zao.

KUMB: 04 / 1436 AH   
25th Muharram 1436 AH
18/11/2014 CE
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut-Tahrir Afrika
Mashariki



RASMI: JAJA AONDOKA YANGA: NAFASI YAKE YAPEWA MBRAZILI MWINGINE

Kiungo mkabaji raia wa Brazil Emerson De Oliveira Neves Rouqe anatarajiwa kuwasili siku ya jumanne mchana jijini Dar es salaam kwa ajili ya majaribio katika klabu ya Young Africans na endapo atafuzu moja kwa moja atajiunga na mabingwa mara 24 wa Ligi Kuu Tanzania bara.

Emerson mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anachezea timu ya Bonsucesso FC iliyopo ligi daraja la pili nchini kwao Brazil, msimu uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Poland katika timu ya Piotrkow Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili nchini humo.

Ujio wa Emerson kuja kufanya majaribio nchini unakuja kufuatia mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil pia Geilson Santos "Jaja" kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda kwao Brazil na kutoa taarifa kwamba hataweza kurejea tena nchini kutokana kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.
Awali ilikua familia ya Jaja ije nchini katika kipindi cha mapumziko, lakini waliomba yeye Jaja ndio aende Brazil na mara baada ya kufika huko matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo yamepelekea kushindwa kurejea nchini
 kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.
Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Young Africans kubakia na wachezaji wanne tu wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hamis Kizza na Andrey Coutinho hivyo endapo Emerson atafuzu  atakuwaa
 anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kimataifa.

Endapo Emerson atafuzu majaribo pamoja na vipimo atajiunga na kikosi cha kocha mbrazil Marcio Maximo katika nafasi ya kiungo mkabaji ikiwa ni sehemu ya kuboresha timu kuelekea kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa.
Aidha kikosi cha Young African baada ya kuwa mapumzikoni kwa takribani wiki mbili, kinatarajiwa kuanza mazoezi siku ya jumatatu katika Uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo wa Nani Mtani Jembe
pamoja na mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania bara.


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU