Facebook Comments Box

Sunday, September 15, 2013

WAMAREKANI WADAI KUGUNDUA CHANJO INAYO ANGAMIZA VVU


Washington. Wanasayansi nchini Marekani wamegundua chanjo ambayo wanaamini itaweza kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa binadamu.
Katika majaribio ya chanjo hiyo, wanasayansi hao wameelezea kuwa imeonyesha mafanikio kwa kuangamiza kabisa virusi wanaofanana na VVU kwa nyani.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limechapisha kwenye tovuti yake kuwa baada ya kubaini hilo sasa wamekusudia kufanya majaribio ya chanjo hiyo kwa binadamu.
Likinukuu taarifa iliyochapishwa kwenye jarida la kisayansi linaloitwa; Nature, lilimnukuu Mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Oregon, nchini Marekani akisema walijiridhisha kuwa chanjo hiyo iliangamiza virusi vyote kwenye mwili wa nyani.
Virusi hao jamii yake inafanana sana na VVU wanajulikana kama Simian Immunodeficiency Virus (SIV) ikiwa na maana ni virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga ya kujikinga na maradhi kwa nyani.
Taarifa za kisayansi zinaonyesha kwamba SIV ni virusi ambao wamekuwa wakienea kwa njia ya kujamiiana miongoni mwa vizazi vya nyani na vilibadilika baada ya kuambukizwa kwa binadamu vikawa vimezaa VVU.
Wanasayansi hao wanasema kati ya nyani 16 waliopewa chanjo hiyo, waliyoipa jina la Cytomegalovirus (CMV),tisa walipona kabisa maradhi ya SIV.
Mtaalamu wa Taasisi ya Chanjo na Jeni katika Chuo Kikuu cha Oregoni, ambaye alihusika kwenye utafiti huo, Profesa Louis Picker aliielezea chanjo hiyo kuwa ni ya kutia moyo ukilinganisha na nyingine ambazo zimewahi kufanyika.
“Katika chanjo nyingi ambazo ziliwahi kuonyesha mafanikio ya kuangamiza virusi ni kwamba kuna baadhi ya seli virusi walibakia,” alisema Profesa Picker, akifafanua:
“Lakini kwa chanjo hii tulichunguza sehemu nyingi nyeti katika mwili wa nyani tukagundua kwamba hakuna kirusi aliyebakia.”
Alisema chanjo yao wameiamini kutokana na uwezo wake wa kupenya maeneo mbalimbali ya mwili kiasi kwamba siyo rahisi kirusi kubakia.
Wanasayansi hao walisema kwa kawaida nyani ambaye ameambukizwa SIV hufa ndani ya kipindi cha miaka miwili


YALIYOJIRI KATI YA YANGA NA MBEYA CITY

Basi la klabu ya Yanga likiwa linaingia katika uwanja wa sokoine mjini Mbeya limeshambuliwa na mashabiki wanaodhaniwa kuwa wa Mbeya City kwa kupigwa mawe, kitu kilichopelekea vioo vya gari hilo kupasuka.

Katika tukio hilo dereva wa basi la Yanga aliumizwa

Mechi iliisha kwa timu hizo kutoka suluhu ya Moja kwa Moja


 
 
 
Wachezaji wa Yanga wakimzonga refa baada ya kukataa bao lao

Wachezaji wa Yanga wakimuambia refa amuangalia mshika kibendera kakubali bao Basi la Yanga likiwa chini ya uangalizi wa Polisi Uwanja wa Sokoine lisishambuliwe zaidi
Yanafaa kula? Mayai yaliyoandikwa Kiarabu yaliyotolewa uwanjani kabla ya mchezo kuanza

Bendera ya Mbeya City na maandishi wa Kiarabu


Friday, September 13, 2013

HILI NDIO TUKIO JINGINE LA MTU KUMWAGIWA TINDIKALI LEO UNGUJA

Ikiripotiwa ni Padri wa kanisa katoliki cheju amemwagiwa tindikali leo. 


MAHAKAMA NCHINI INDIA YAWA HUKUMU KIFO WABAKAJI WANNE

Mahakama nchini India imewahukumu wanaume wote wanne kifo baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumuua mwanamke katika basi katika mji mkuu wa India Delhi mwezi Desemba mwaka jana.
Mmoja wao aliangua kilio na kuanguka baada ya kutangazwa kwa hukumu dhidi yao .
Taarifa zinazohusiana
afya
Msichana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 23 aliumizwa sana na baada ya wiki moja alifariki kutokana na majeraha .
Karibu miezi 9 baada ya ubakaji ulioitikisa India, jaji ametoa hukumu kwa wanaume wote wanne ambao tayari walikuwa wamepatikana na hatia ya uhalifu .
Wendesha mashtaka walikuwa wamewaombea hukumu ya kifo wakisema ingetoa ishara muhimu kwamba uhalifu wa aina hiyo hautakubalika kamwe .
Familia ya mwanamke huyo pia waliomba wanaume hao wanyongwe .
Lakini mawakili watetezi wa wanaume hao walipinga mapendekezo ya hukumu ya kifo , wakisema wateja wao hawakuwa na rekodi za uhalifu awali na kwamba wanastahili kusamehewa .
Kifo cha mwanafunzi huyo mwezi Disemba mwaka jana kilisababisha maandamano makubwa ya upinzani kote nchini India , yaliyoilazimisha serikali kubadili sheria zilizokuwepo za uhalifu wa ngono



Thursday, September 12, 2013

WAGENI WOTE WATAKAO INGIA ZANZIBAR KUPIMWA MALARIA

KITENGO cha kupambana na Malaria Zanzibar (ZMPC) kimesema kinatarajia kuanza kampeni ya kuchunguza malaria kwa wageni wote watakaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege na bandari ya Malindi.

Ofisa mwandamizi wa kitengo wa ZMPC, Mwinyi Mselem akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mikakati ya kupambana na malaria nchini, alisema kitengo kimepanga kutekeleza mikakati hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha kwamba ugonjwa wa malaria unatokomezwa na hakuna njia za kuambukizwa kwa wananchi.

“Tunakusudia kuanzisha zoezi la kupima afya za wageni wote wanaoingia nchini kupitia njia za uwanja wa 
ndege pamoja na bandarini ili kujuwa afya za wageni wanaoingia nchini,” alisema.

Alisema mikakati ya kitengo cha kupambana na malaria ifikapo mwaka 2017 ni kuhakikisha ugonjwa huo umetokomezwa na siyo tishio tena kwa afya za wananchi. Kwa sasa Zanzibar imefanikiwa kushusha maambukizi ya ugonjwa huo kutoka asilimia 32 hadi kufikia asilimia moja na kupunguza vifo vya akinamama na watoto.

Hata hivyo, Mselem alisema katika kipindi cha miaka miwili sasa kumejitokeza maambukizi mapya ya malaria kutokana na kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira na hivyo kupelekea mbu kuzaliana zaidi.

Alisema kitengo cha kupambana na malaria kinatarajia kuanza kazi ya kupiga dawa majumbani pamoja na sehemu za mazalia ya mbu. Mselem alisema kazi hiyo inatarajiwa kuanza katika kipindi cha msimu wa mvua za vuli, ambazo huibuka kwa mazalia mengi ya mbu yanayosababisha ugonjwa wa malaria.

Zanzibar inatajwa mfano wa kupambana na ugonjwa wa malaria, ambapo hivi karibuni Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton alizindua mradi wa kupambana na ugonjwa huo wa kupima damu hapo katika uwanja wa Amaan mjini hapa.

Khatib Suleiman
HabariLeo, Zanzibar


JWTZ YAKANA TAARIFA YA JAMII FORUM, TWITTER NA FACEBOOK

JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA
KURUGENZI YA HABARI NA UHUSIANO
Telex : 41051                                                      
Tele Fax  : 2153426
Barua pepe : ulinzimagazine@yahoo.co.uk
Tovuti : www.tpdf.mil.tz
Makao Makuu ya Jeshi,                
Simu ya Upepo  : “N G O M E”      
Simu ya Mdomo  : DSM  22150463
 Sanduku la Posta  9203,              
DAR ES SALAAM,                           

           12 Septemba, 2013. 
Taarifa kwa vyombo vya Habari

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) limepata habari kupitia mtandao wa Jamii Forumna Gumzo la Jiji  na mingineyo kuwa likizo zimesitishwa Jeshini  na waliokuwa  likizo wameitwa kurudi kazini.

          Taarifa hizo pia zimeeleza kwamba Brigedi za Tembo na Kifaru zimepewa maagizo ya kuwa katika hali 
ya utayari endapo watahitajika kusonga mbele.

          JWTZ  linapenda kuwaeleza wananchi pamoja na watumiaji wa mitandao hiyo kuwa taarifa hizo ni za upotoshaji mtupu na hazina ukweli wowote.  Aidha, taarifa hizo ni zenye nia ya kuzorotesha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yetu (Tanzania) na majirani zake. 

Sambamba na taarifa hii, pia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa za kutohusika na viunganishi vya JWTZ kwenye mitandao ya  ‘Facebook‘ – (Facebook/JWTZ) na  ‘Twitter‘  (Twitter/ JWTZ).

Mitandao hiyo yenye viunganishi vya JWTZ imekuwa ikijihusisha na kutoa taarifa ambazo zimekuwa zikichangiwa na watu mbalimbali, ambapo baadhi yao wamekuwa wakitoa taarifa za upotoshaji  na zisizo sahihi.  Tunapenda kutaarifu kwamba akaunti za facebook na twitter zilizotajwa siyo za JWTZ.

Hatua zimechukuliwa za kuwatambua wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

         Aidha inasisitizwa kwamba JWTZ lina taratibu za zake zinazotumika kufanya mawasiliano na Vyombo vya Habari, Taasisi, au mtu binafsi kuhusu utoaji wa taarifa.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi
Dar es salaam, Tanzania



AKAMATWA MUDA MCHACHE KABLA YA KUTIMIZA AZMA YAKE YA KUCHOMA QUR`AN

Kiongozi mmoja wa Kanisa nchini Marekani anayeishi jimboni Florida, Terry Jones alitiwa mikononi mwa polisi jana muda mchache tu kabla ya kutimiza azimio lake la kuchoma Quran takriban elfu tatu, katika siku ambayo taifa hilo lililkuwa likiadhimisha miaka 12 tangu Marekani ishambuliwe kigaidi Septemba 11.

Magazeti kadhaa ya jimboni Florida yaliandika ifuatavyo:

The Tampa Tribune: "When he and another pastor were pulled over by Polk County sheriff's deputies near the small town of Mulberry, their pickup bed was full of kerosene-soaked Qurans - and they were towing a 
large, barbeque-style grill behind the truck. The arrest happened shortly before 5 p.m., when Jones was scheduled to burn the Qurans - one for every victim of the terrorist attacks - at a public park just outside Mulberry."

The Polk County Ledger:  County officials had previously denied a permit for the event. The paper reports that in a press conference Sheriff Grady Judd said Jones had been stopped because his trailer did not have a license plate and he has been charged with "unlawful conveyance of fuel and unlawful carry of a firearm."
Essentially, Judd said, Jones was driving a "bomb" down the road.
"We couldn't allow that vehicle to continue down that road," Judd alinukuliwa na gazeti kusema hayo.

The AP: "Jones is the pastor of a small evangelical Christian church. His congregation burned a Koran in March 2011, and last year he promoted an anti-Muslim film. His actions have sparked violence in the Middle East and Afghanistan. The U.S. Central Command, based at MacDill Air Force Base in Tampa, earlier this week had urged him not to go through with Wednesday's event."

Hii si mara ya kwanza kwa Jones kufanya jaribio la kuchoma Quran kwani miaka mitatu iliyopita, alipigiwa simu na Robert Gates, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi wa wakati huo, akimtaka aachane na mpango wake wa kuchoma kitabu hicho kitakatifu cha Waisalam, kwa sababu kufanya hivyo kungehatarisha maisha ya askari wa Marekani waliopo ng'ambo, duniani kote.

Pamoja na kuwa alitii wito huo, mwaka 2012 mwezi Aprili alitimiza azma yake hiyo
.


MESUT OZIL KUANZA KUITUMIKIA TIMU YAKE MPYA YA ARSENAL JUMAMOSI NA SUNDERLAND



KIUNGO Mesut Ozil amewasili katika klabu yake mpya, Arsenal tayari kuanza kumtumikia Arsene Wenger anayekabiliwa na tatizo la wachezaji wengi majeruhi.

Mchezaji huyo aliyenunuliwa kwa Pauni Milioni 42 ataanza mazoezi leo makao makuu ya klabu, Colney London kwa mara ya kwanza tangu ahamie akitokea Real Madrid.
 
Na Wenger anajiandaa kumtumia mwanasoka huyo wa kimataifa wa Ujerumani katika mchezo dhidi ya Sunderland Jumamosi hii baada ya Tomas Rosicky kurejea kwenye mechi ya timu yake ya taifa akiwa majeruhi.
 
Mwanasoka huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Czech aliumia wakati timu yake ikilala 2-1 dhidi ya Italia na yuko shakani kucheza Uwanja wa Light.
 
Hiyo inaacha milango wazi mno kwa Ozil kuanza kazi Arsenal, licha ya kwanza atakuwa na siku mbili tu kamili za kufanya mazoezi na wenzake kabla ya mechi hiyo.
 
Licha ya msimu kuwa umekwishaanza kwa karibu mwezi mzima, Arsenal tayari ina idadi kubwa ya majeruhi. 


FAMILIA YA MATUMLA: TUNASHANGAZWA NA TAARIFA YA NDUGU ZETU KUKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA

TAARIFA za kukamatwa na unga kwa mabondia wawili Mbwana na Mkwinda wa familia maarufu ya mchezo wa ngumi nchini ya Matumla, zimeishangaza familia na jamii nzima ya Tanzania.

Bondia Rashid ‘Snake man’ Matumla ambaye ni kaka wa Mbwana na Mkwanda, amedai endapo itathibitika wadoeo zake wanajihusisha kusafirisha dawa za kulevya, watakuwa ameipa fedheha familia yao.

Mbwana Matumla ambaye ni mkubwa, ameelezwa kukamatwa mpakani mwa Uswisi na Ujerumani wakati Mkwanda Matumla amekamatwa Addis Ababa nchini Ethiopia.

Akikaririwa kuzungumza na wanahabari kadhaa, Rashid, bingwa wa zamani wa dunia wa WBU amesema:

    Tumesikia Mkwanda hadi ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia umethibitisha, lakini Mbwana bado hatuna uhakika ingawa hakuna anayeweza kumpata kwa sasa.

    Ni mwezi sasa umepita sina taarifa naye na hata wakati anaondoka hakuniaga, nimesikia kupitia

    vyombo vya habari. Kitendo cha mdogo wangu kukamatwa kimenisikitisha mno, siyo siri nimekwazika na ninarudia kusema hii ni fedheha kwenye familia yetu.
    
    Mimi mwenyewe nashangaa ni lini amejiingiza kwenye kazi hiyo, hata wakati anaondoka hakuniaga, mimi kaka yao na familia hatuelewi chochote.

    Unajua Mbwana hakumuaga hata mkewe, kweli inatusikitisha sana na tunasikia maumivu makubwa. Kama kweli itakuwa ni hivyo, basi watakuwa wameiangusha sana familia ambayo ilipigana kujenga jina. Lakini hatuwezi kuwatenga kwa kuwa ni ndugu zetu, tutawapigania.

Maisha:
Mkwanda alikuwa akiishi nchini Sweden ambako alikuwa na mpenzi wake aliyejaaliwa naye kupata mtoto mmoja aitwaye Liam aliyezaliwa mwaka 2010. Mpenzi wake huyo raia wa Sweden alikuwa mwanafunzi katika chuo kimoja mjini Norrkoping wakati Mkwanda alikuwa mwanafunzi katika chuo kingine akisomea Lugha ya Kiswidi. Alisema mdogo wake huyo alikuwa amebadilisha uraia na kuchukua uraia wa Sweden licha ya kwamba hapa Tanzania alikuwa amepanga Mbagala, Dar es Salaam na alikuwa anakuja na kukaa kwa muda na kisha kuondoka.

Kurejea:
Hivi karibuni inaelezwa alirejea jijini Dar es Salaam na alionekana ni mtu mwenye furaha na mishemishe kibao. Alikuwa anamiliki gari aina ya Toyota Vitz ambalo pia aliliuza lakini kuna taarifa kuwa, alinunua kiwanja katika moja ya maeneo ya Jiji la Dar.

Ngumi:
Katika familia ya Matumla, Mkwanda ndiye alikuwa bondia mdogo kuliko wote baada ya wengine sita. Kwa mujibu wa Rashid alipumzika kucheza ngumi miaka kadhaa iliyopita kutokana na kusumbuliwa na maradhi. Rekodi zinaonyesha kabla ya kupumzika kwa muda kucheza ngumi, Mkwanda alishinda mapambano manane (sita kwa KO) alipigwa mara tatu zote kwa KO alitoka sare mara moja tangu 2004. Mkubwa ni Ally ambaye ni marehemu, anafuatiwa na Rashid Matumla aliyewahi kuwa bingwa wa dunia mara mbili, bingwa wa mabara, Afrika mara moja na ndiye anaaminika kuwa bondia mkali zaidi ya wengine. Anafuatia Hassan, Mbwana ambaye anaelezwa ‘kudakwa’ Ulaya, Kareem na Mkwanda. 

--- Habari kwa mujibu wa magazeti ya MWANANCHI na GPL



Wednesday, September 11, 2013

OPERESHENI YA KUSAKA WAHAMIAJI HARAMU YASABABISHA MNYARWANDA KUJINYONGA

Raia wa Rwanda amejinyonga kwa kamba chumbani kwake, tukio linalohusishwa na zoezi linaloendelea hivi sasa nchini la kuwasaka wahamiaji haramu na kuwarejesha makwao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, marehemu anatajwa kuwa ni Francis Mathias (75), ambaye alikuwa mkazi wa kitongoji Kikukuru kata Kikukuru, tarafa Mabira wilayani Kyerwa mkoani Kagera.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kikukuru, Joseph Leo, jana alilithibitishia NIPASHE kutokea kwa tukio hilo na kuwa alipata taarifa hizo kutoka kwa binti wa marehemu juzi saa 3:00 asubuhi.

“Baada ya kupata hizo taarifa niliongozana na mgambo, tulipofika mlango wa chumba chake ulikuwa umefungwa kwa ndani, tukafanikiwa kuuvunja tukaingia ndani na kukuta amejitundika kwa kamba,” alisema Leo na kuongeza kuwa marehemu alikuwa mfugaji na mkulima.

Alisema kuwa kabla ya kujiua, mzee huyo alichana fedha za Kitanzania zinazokadiriwa kufikia Shilingi
milioni saba zikiwamo noti za Sh. 5,000 na za Sh. 10,000, ambazo zilikutwa ndani ya chumba chake.

Leo alisema baada kushuhudia alipiga simu kwa Ofisa Mtendaji wa Kata Kikukuru ambaye alifika na kupiga ngoma na watu walikusanyika kushuhudia kilichotokea na baadaye kwenda kutoa taarifa  katika kituo cha Polisi.

Alipotakiwa na NIPASHE kuthibitisha kama kweli mwananchi wake aliyejinyonga alikuwa raia wa Rwanda, Leo alithibitisha na kufafanua kuwa tayari alikwisha kumuorodhesha kwa lengo la kurejeshwa kwao katika opereshani iliyoanza Jumamosi ya kuwarejesha makwao wahamiaji haramu wanaoishi mkoani Kagera.
Aliongeza kuwa aliwahi kumhoji marehemu Mathias ambaye alimweleza kuwa alikuja Tanzania kutoka Rwanda tangu mwaka mwaka 1976.

Naye Ofisa Tarafa ya Mabira, Nicolaus Rugemalira, alisema uchunguzi wa awali wa kimazingira umeonyesha kuwa kulikuwa na mgogoro wa familia baada ya marehemu kutaka wauze mali zao zote warudi Rwanda, lakini familia yake haikukubaliana naye kutokana na mkewe kuwa raia wa Tanzania.

“Mke wake ni Mtanzania, inaonekana baada ya familia yake kukataa uamuzi wake wa kuuza mali zote ili waondoke, aliamua kuchukua uamuzi huo,” alisema Rugemalira.

Akizungumzia tukio hilo, binti wa marehemu, Melania Francis, alithibitisha kuwapo ugomvi kati ya baba yake na mama yake hali iliyosababisha mama yao kuondoka bila kufahamika alikoelekea.

Alisema siku ya tukio aliamka na kuwaandaa wadogo zake kwenda shuleni na baada ya hapo alikwenda shambani kuona kama vibarua wameanza kazi ya kulima, lakini aliporudi nyumbani alishangaa kuona mlango wa chumba cha baba yake bado umefungwa wakati haikuwa kawaida yake kulala hadi saa moja.

Melania alisema alibisha hodi bila majibu, akajaribu kufungua ikashindikana na alipochungulia aliona fedha nyingi zimetapakaa ndipo alipokimbia kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji.

“Nafahamu baba alikuwa na uwezo wa kumiliki fedha hizo, lakini sikufahamu anazihifadhi wapi,” alisema binti huyo wa marehemu.

Alisema wamezaliwa watoto watano katika familia hiyo na kwamba ndugu zake wawili walitoweka na kubakia watatu na kuongeza kuwa kuwa anatambua kuwa baba yake alikuwa raia wa Rwanda.

Alipotakiwa kueleza kama anafahamu alikoelekea mama yake, binti huyo alidai kuwa hafahamu ingawa anafahamu kuwa ni mzaliwa wa Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.

Kutokana na kutoweka kwa mama huyo pamoja na wanafamilia wengine, uongozi wa eneo hilo unaendelea na ufuatiliaji ili kujua wanafamilia wengine wamekwenda wapi.
--- via gazeti la NIPASHE


Tuesday, September 10, 2013

TFF YATHIBITISHA KUWA COASTAL UNION ILIBEBWA MECHI DHIDI YA YANGA

YANGA imemponza mwamuzi, Martin Saanya wa Morogoro aliyechezesha mechi yao na Coastal Union ambaye amefungiwa mwaka mmoja kwa kuchezesha mchezo huo chini ya kiwango.
Saanya amepewa adhabu hiyo ya kutochezesha mechi yoyote ya soka ndani ya kipindi hicho sawa na mshika kibendera namba moja wa mechi hiyo, Jesse Erasmo ambaye alishindwa kutoa uamuzi sahihi wa adhabu ya penalti waliyopewa Coastal ndani ya dakika za nyongeza kabla ya mpira kumalizika na kusababisha sare ya bao 1-1.
Penalti hiyo ndiyo ilisababisha vurugu ambazo zilifanywa na mashabiki wa Yanga ambao , walimshambulia mwamuzi kwa chupa za maji na kuvunja kioo cha basi la wachezaji wa Coastal na kumjeruhi kichwani beki wa timu hiyo, Hamis Hamad aliyelazimika kuwahishwa hospitali.
Adhabu hizo zimekuja baada ya Bodi ya Ligi kupitia taarifa ya kamishna wa mechi hiyo, Omary Walii kutoka Arusha.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Saanya na Erasmo wamefungiwa mwaka mmoja kuchezesha mechi za ligi baada ya bodi kupitia ripoti ya kamishina wa mchezo huo.
Saanya ameadhibiwa kwa kuchezesha chini ya kiwango na alitoa adhabu ya penalti iliyofungwa na Coastal akiwa mbali na tukio,” alisema Mwakibinga na kufafanua kuwa posho za waamuzi wa mechi kwa sasa ni Sh 250,000 mbali na nauli na teksi tofauti na zamani walipokuwa wanalipwa shilingi 170,000.
“Kwa upande wa Erasmo ndiye alikuwa eneo la tukio ilipotokea penalti, lakini alishindwa kumsaidia mwamuzi wa kati na kubaki ameduwaa kama asiye na uhakika.”
Mwakibinga alisema mbali na adhabu hizo kwa waamuzi, Kamati imemfungia kocha wa makipa wa Coastal Union, Juma Pondamali muda wa miezi mitatu na faini ya Sh1 milioni kwa kutoa lugha ya matusi kwa mashabiki wanaodaiwa ni wa Simba.
Katika hatua nyingine, Coastal imetozwa faini ya Sh100,000 kwa kuchelewa kikao cha maandalizi ya mechi asubuhi kwa dakika 23 huku Yanga ikitozwa faini ya Sh1 milioni kwa mashabiki wake kurusha chupa uwanjani na pia kumvamia mwamuzi huku viongozi wakishindwa kuwadhibiti.
Kuhusu basi la Coastal hakukuwa na taarifa kwani tukio lilitokea nje ya uwanja.

SOURCE> MWANASPOTI



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU