Facebook Comments Box

Friday, August 23, 2013

ANGALIA PENATI HII YA MWISHO ILIYOPIGWA KIUFUNDI KABISA

Ni penati ya mwisho ya ushindi na kijana kaipiga kwa ufundi kabisa


MAKATIBU NA MANAIBU WAKUU WAAPISHWA IKULU NA RAIS



 Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe Ombeni Sefue wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa ofisi ya Sekretariate ya Baraza la Mawaziri ambako watumishi wake wawili wameteuliwa kuwa manaibu Makatibu wakuu, ambao ni Injinia Angelina Madete (kulia kwa Rais) na Mhe. Consolata Mgimba (kushoto kwa Rais) mara baada ya kuapishwa Makatibu wakuu na Manaibu Katibu wakuu Ikulu jijini Dar es salaam leo.


 Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dkt Mohamed Ghalib Bilal na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue katika picha ya pamoja na Makatibu wakuu na manaibu Katibu wakuu wapya mara baada ya kuapishwa Makatibu wakuu na Manaibu Katibu wakuu Ikulu jijini Dar es salaam leo.

 Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dkt Mohamed Ghalib Bilal na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue katika picha ya pamoja na Makatibu wakuu wapya mara baada ya kuapishwa Makatibu wakuu hao na Manaibu Katibu wakuu Ikulu jijini Dar es salaam leo.

Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dkt Mohamed Ghalib Bilal na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue katika picha ya pamoja na Manaibu Katibu wakuu mara baada ya kuapishwa Makatibu wakuu na Manaibu Katibu wakuu hao Ikulu jijini Dar es salaam leo.
CHANZO:MICHUZI BLOG

PICHA: UAPISHWAJI WA RAIS MUGABE WA ZIMBABWE

Rais, Robert Gabriel Mugabe,  jana kwa mara ya saba katika historia ya nchi hiyo, alikula kiapo cha kuongoza Zimbabwe kwa nusu muongo ujao.

Shughuli za kuapishwa zilifanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Harare, Agosti 22, 2013 na kuhudhuriwa na wawakilishi wa mataifa mbalimbali kutoka barani Afrika.

Zifuatazo ni baadhi tu ya picha kutoka IKULU ya Tanzania, za kumbukumbu ya tukio hilo.



Thursday, August 22, 2013

SERIKALI YA WASIMAMISHA KAZI NA KUWAVUA MADARAKA MAAFISA WA JESHI LA POLISI

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Waziri Nchimbi amesema hatua hiyo ni katika kuendeleza vita ya kuhakikisha kuwa jeshi la polisi linakuwa na nidhamu, linatekeleza wajibu wake wa kutenda haki na kuwalinda raia na mali zao.

Waziri Nchimbi aliwataja waliovuliwa madaraka kuwa ni Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoani Arusha Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro, Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Inspekta Jamal Ramadhan, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Dumila Inspekta Juma Mpamba na mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Kasulu ASP Daniel Bendarugaho na kumsimamisha kazi Inspekta Isaack Manoni.

Alifafanua kuwa Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro alivuliwa madaraka kwa kushindwa kusimamia kikamilifu askari na maafisa walio chini yake ambao walikamatwa wakisafirisha bangi yenye uzito wa kilogramu 540 kwa kutumia gari la polisi. Alisema askari hao wawili waliokamatwa wakisafirisha bangi, walikuwa wakifanya kazi kwenye kituo cha Ngarananyuki na baada ya kukiri kosa walifukuzwa kazi mwezi Mei mwaka huu.

Alisema kwa upande wa Inspekta Jamal Ramadhan amevuliwa madaraka yake kwa kutochukua hatua stahiki baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara wa Mvomero Samson Mwita kubambikiwa fuvu la kichwa cha binadamu na askari polisi watatu wakishirikiana na matapeli wawili. “Katika tukio hilo Inspekta Isaack Manoni amesimamishwa kazi na atashtakiwa kijeshi kutokana na tuhuma za kumtorosha mtuhumiwa, Cpl. Edward aliyekuwa dereva wa gari la Polisi lililokamatwa na bangi kitendo ambacho kimelifedhehesha jeshi la polisi” alisema Waziri Nchimbi.

Alibainisha kuwa Inspekta Juma Mpamba amevuliwa madaraka hayo kwa kuonesha udhaifu katika utendaji wake wa kazi kwa kutosimamia kikamilifu askari walio chini yake kitendo kilichosababisha askari kujipangia kazi nje ya utaratibu na kumbambikiza mfanyabiasha huyo kesi kwa lengo la kujinufaisha kinyume na maadili ya kazi. Aliongeza kuwa askari waliohusika na tukio hilo wamefukuzwa kazi na kushtakiwa. Waziri Nchimbi alisema ASP Daniel Bendarugaho amevuliwa madaraka kwa kutokuwa makini katika kufanya na kusimamia upelelezi wa kesi ya mauaji ya marehemu Gasper Mussa Sigwavumba aliyeuawa baada ya kupigwa na askari polisi wawili Desemba mwaka jana.

Alisema upelelezi mbovu uliofanywa chini ya usimamizi wa Mkuu huyo wa upelelezi ulisababisha kesi hiyo kuondolewa mahakamani. Aliongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo utaanza upya ili haki itendeke.


KITUO CHA MABASI YA KUTOKA DAR KWENDA MIKOANI KUJENGWA MBEZI LUIS NA BASIHAYA: JIJI







TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itajenga vituo vya mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani katika maeneo ya Mbezi Luis na Boko-Basihaya. Ujenzi wa vituo hivyo ni utekelezaji wa mipango ya Jiji ya kuimarisha huduma za usafiri Dar es Salaam.

Kituo cha Mbezi Luis kitahudumia wasafiri wa Kanda ya Kati na Nyanda za Juu wakati Kituo cha Boko Basihaya kitatoa huduma kwa wasafiri wa Kanda ya Kaskazini. Kwa Kanda ya Kusini Halmashauri ya Jiji itajenga Kituo cha Mabasi Kongowe.

Kituo kitakachoanza kujengwa ni Mbezi Luis ambacho kitajengwa sambamba na Boko Basihaya. Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kimepangwa kutoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka kwa wasafiri wote watakaokuwa wakitumia vituo hivyo vya mabasi yaendayo mikoani. Ujenzi wa vituo vya Mbezi Luis na
 Boko Basihaya, kutokana na upembuzi yakinifu wa awali, unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 40 kwa kila kituo.

Ujenzi wa vituo hivyo unahitaji upembuzi yakinifu wa kina kwa lengo la kupata gharama halisi za utekelezaji wake, kubaini vyanzo vya fedha na kuangalia uwezekano wa kuzishirikisha taasisi mbalimbali za fedha na wawekezaji wanaoonyesha nia ya kushirikiana na Halmashauri ya Jiji katika ujenzi wa vituo hivyo ambavyo vitakapokamilika vitakuwa pia ni chanzo cha ajira kwa wananchi.

Katika kipindi hiki cha maandalizi ya ujenzi wa vituo hivyo, bado Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) kitaendelea kutoa huduma kwa wasafiri waendao mikoani na nchi za jirani. Halmashauri ya Jiji inapenda wananchi wafahamu kwamba UBT,

 kama ilivyopangwa na Serikali, itakuwa ni kituo kitakachotoa huduma ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka(Dar Rapid Transit-DART) baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu yake. Pamoja na hilo Halmashauri ya Jiji pia itajenga “shopping malls” na hoteli katika kituo hicho cha UBT

Kukamilika kwa ujenzi wa vituo hivyo vya mabasi ni mafanikio makubwa katika jitihada za serikali za kuimarisha huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo katika sekta hii, wananchi na taasisi mbalimbali wanategemewa kuendelea kutoa mapendekezo yao ya kuimarisha huduma za usafiri Dar es Salaam.

DIAMOND PLATNUMS AELEZEA KASHFA YAKE YA MADAWA YA KULEVYA TAZAMA ALICHO KISEMA



Msanii Wa Muziki wa Bongofleva mwenye jina kubwa mjini na mwenye Mkwanja mkubwa hapa nchini Naseeb Abdulmaliki “Diamond Platnumz” amejitokeza na kukanusha kuwa hahusiki na biashara ya madawa ya kulevya.
 
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na taarifa za Diamond kujihusisha na biashara hiyo hasa kutokana na ukaribu wake na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wenye maskani yao nchini Afrika Kusini.

 
Taarifa zaidi zinasema ni wafanyabiashara hao waliohusika kwa karibu kuusafirisha mwili wa marehemu Albert Mangwair, aliyefia huko huko Afrika Kusini ambaye taarifa za kifo chake ziligubikwa na matumizi ya madawa ya kulevya.

Akikanusha taarifa hizo Diamond amesema “Ni kweli mimi nina pesa za kutosha kuniwezesha kuishi maisha ninayotaka lakini sijawahi kujihusisha na biashara hiyo.

"Kufanya kazi kwa bidii kunalipa na kazi yangu inaonekana na ndiyo inayoniwezesha kuwa na fedha ambazo leo watu wameanza kuzitilia shaka. Sielewi nia ya watu hawa ni nini?”

Taarifa za Diamond kuhusishwa na mtandao huu zimeanza kushika kasi kufuatia miongoni mwa watu wake wa karibu kuonekana wakiwa karibu sana na akina Agnes Gerald “Masogange” (25) na Melisa Edward (24) kwenye uwanja wa kimataifa wa ndege wa Mwalimu JK Nyerere wa Dar es Salaam kabla hawajapanda ndege kuelekea Afrika Kusini ambako walikamatwa.


RAISI JAKAYA KIKWETE AFANYA MABADILIKO YA MAKATIBU WAKUU WA WIZARA MBALIMBALI


Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Ombeni Y. Sefue akiongea  na Waandishi wa Habari waliojikusanya jioni hii kuhusu Uteuzi wa Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu Wapya, jijini Dar es Salaam. Pembeni kushoto ni Bw. Salvatore Rweyemamu, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Baadhi ya walioteuliwa:
Dr Florence Turuka - Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
Bi Joyce Mapunjo -Katibu Mkuu wizara ya Afrika Mashariki
Bw Sihaba Mkinga -Katibu Mkuu -Habari, Michezo na Utamaduni
Bi Sofia Kaduma -Katibu Mkuu Kilimo na Ushirika
Dr Deo Mtasiwa -Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu akishughulikia Afya

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardh Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw Patrick Rutabanzibwa Amestaafu kwa hiari.
Wafuatao wameondolewa Ukatibu Mkuu na badala yake watapangiwa kazi nyingine:

1. Seth Kamuhanda
2. Kijakazi Mtengwa
3. Omary Chambo

Bw Peniel Lyimo aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu amehamishiwa Ofisi ya Rais kuwa Naibu Mtendaji Mkuu Kitengo cha PDU akishughulikia maswala ya Kilimo

  Orodha kamili ya walioteuliwa ni:
Jumanne Sagini amekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) awali alikuwa Naibu Katibu Ofisi wa Waziri Mkuu - TAMISEMI. Dk. Servacius Likwalile amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,awali alikuwa Naibu Katibu.
Dk. Patrick Makungu- Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo.

Alphayo Kitanda- Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, awali alikuwa Naibu Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI. Dk. Shaaban Mwinjaka - Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi,awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Dk.Uledi Mussa-Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, awali alikuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Profesa Sifuni Mchome- Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, awali alikuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania. Charles Pallangyo - Katibu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Anna Maembe -Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo, Sihaba Nkinga- Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo, Sophia Kaduma- Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Naibu makatibu wakuu wapya walioteuliwa ni:
Angelina Madete- Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Regina Kikuli -Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Zuberi Sumataba -Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia suala la elimu, Edwin Kiliba -Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI.

Dk. Yamungu Kayandabila -Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Adolf Mkenda -Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha anayeshughulikia sera, Dorothy Mwanyika -Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha anayeshughulikia Fedha za Nje na Madeni. Rose Shelukindo -Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, 

Dk. Selassie Mayunga -Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Monica Mwamunyange -Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Consolata Mgimba -Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Profesa Elisante ole Gabriel Laizer -Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Armantius Msole -Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waliopewa uhamisho kuwa ni:
John Mngondo amehamishiwa  Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ametoka Wizara ya Uchukuzi, Selestine Gesimba - Wizara ya Maliasili na Utalii anatoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Injinia Ngosi Mwihava anahamia Wizara ya Nishati na Madini kutokea Ofisi ya Makamu wa Rais.

Maria Bilia -Wizara ya Viwanda na Biashara kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Nuru Milao anahamia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hiyo ndio orodha yote ya walioteiuliwa, kuhamishwa na kuacha kazi.


Wednesday, August 21, 2013

WAMBURA AJITOA KWENYE KINYANG'ANYIRO CHA UCHAGUZI TFF


Aliyewahi kuwa mgombea wa Uchaguzi Mkuu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliosimamishwa na Fifa, Michael Wambura, amesema hatashiriki tena kwenye uchaguzi ujao wa shirikisho hilo, Oktoba 27.
 
Awali Wambura, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa FAT (sasa TFF), aliwania nafasi ya Makamu Rais katika uchaguzi uliosimamishwa na Shirikisho la Soka Ulimwenguni (Fifa), kutokana na kuwepo malalamiko kutoka kwa watu  walioenguliwa akiwamo yeye.
 
Jana TFF ilitangaza majina ya wagombea 58 wote ikiwa ndiyo siku ya mwisho  kurejesha fomu, lakini bila kuwepo kwa jina la Wambura ambaye  alipoulizwa na Mwananchi sababu ya kutogombea tena alisema: “Siwezi  kujisafisha na majitaka.”
 
“Nimeamua kupumzika, nilipigania haki imepatikana kwa kamati mbili kuundwa. Bila mimi kamati hizo zisingekuwapo, lakini jambo muhimu ni kwamba siwezi kujisafisha na majitaka,” alisema Wambura.
 
“Mfumo wa uongozi TFF ni mbovu, kumejaa siasa za majitaka, hizo kamati  zilizoundwa hazitafanya kazi kwa vile tu Wambura hayupo, ningekuwepo  zingepata kazi ya kufanya,” alitamba Wambura.
 
Nafasi ya Makamu wa Rais inawaniwa na Iman Madega, Ramadhan Nasib na  Walace Karia, huku wajumbe waliomba kuwakilisha kanda mbalimbali ni Abdallah Mussa, Kaliro Samson, Jumbe Magati, Mugisha Galibona, Vedastus  Lufano, Samwel Nyalla, Epaphra  Swai, Mbasha Matutu, Stanslaus Nyongo, Ally Mtumwa, Elley Mbise na Omari Walii. ni Ahmed Mgoyi, Yusuf Kitumbo, Ayoub Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja, Ayoub  Nyenzi, Cyprian Kuyava, David Lugenge, Elias Mwanjala, Eliud Mvela, John  Kiteve, James Mhagama, Kamwanga Tambwe na Stanley William Lugenge, Athuman Kambi, Francis Kumba, Zafarani Damoder.
 
Charles Komba, Hussein Mwamba, Stewart Masima, Farid Nahdi, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Riziki Majala, Twahil Twaha Njoki, Davis  Mosha na Khalid  Mohamed. Alex  Kamuzelya, Juma Pinto, Muhsin Balhabou, Omar Abdulkadir, Shaffih Dauda na Wilfred  Kidao. Kwa upande wa TPL Board waliojitokeza kuwania uongozi wa juu ni wawili Hamad Yahya (Mwenyekiti) na Said Muhamad Said (Makamu Mwenyekiti).Walioomba nafasi za ujumbe wa TPL Board ni Kazimoto Muzo, Michael  Kaijage, Omari Mwindadi, Salum Rupia na Silas Magunguma.
CHANZO:SHAFFIH DAUDA


TIMU ZOTE 14 ZAKABIDHIWA VIFAA KWA AJILI YA LIGI KUU YA VODACOM INAYOTARAJI KUANZA JUMAMOSI YA TAREHE 24/08/2013


Wadhamini wakuu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kampuni ya Vodacom Leo imekabidhi vifaa kwa timu zote 14 vyenye thamani ya Shilingi milioni 400.

Akizungumza kabla ya zoezi la kukabidhi vifaa hivyo kuanza, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba pamoja na kuishukuru Vodacom kwa kutekeleza majukumu yake ya kimkataba amevitaka vilabu vya ligi kuu kuu ya Vodacom kuheshimu chapa ya mdhamini wakati wote wa mechi za ligi.

“Ninatoa wito kwa vilabu vyote kutumia jezi zenye nembo ya mdhamini kama kanuni zinavyo sema, pia ninawaomba viongozi wote tuwe na Ushirikiano katika kuhakikisha ligi inafanikiwa kama inavyotakiwa,”

Wawakilishi wa timu mbalimbali zinazoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhiwa vifaa vya michezo na mdhamini wa ligi hiyo kampuni ya Vodacom tayari kwa ajili ya kuanza kwa msimu wa ligi kuu 2013/2014. Pamoja nao katika picha ni Mkuu  wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa kampuni  hiyo Kelvin Twisa,(Aliyeshikilia mpira) na Mkurugenzi  wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba.

Kama mzazi tusingependa kutumia kanuni na sharia kuadhibu klabu inayokwenda kinyume tunapenda kuona kila mmoja akimtendea haki mdhamini kama ambavyo nayeye anavyotimiza haki yake ya kutupatia vifaa hivi.”

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom, Kelvin Twissa alisema kuwa vifaa hivyo viko tayari na anaamini timu zote zimejiandaa vya kutosha na tayari kuingia katika mtanange wa ligi.

“Tunajisikia furaha sana kufikia hapa leo na kukabidhi vifaa hivi tukitekeleza matakwa ya mkataba wa udhamini, ni imani yetu kwamba timu zineshajiandaa vizuri na sasa tupo tayari kuanza msimu mpya wa 2013/2014.’Alisema Twissa

Twissa aliongeza kuwa vifaa vipya vilivyo kabidhiwa ni pamoja na seti za jezi mbalimbali, viatu vya mazoezi na mechi, soksi, vilinda ugoko (shin guards), nguo za mazoezi, nguo za kawaida, gloves na vifaa vingine.

Aidha, Pamoja na kukabidhi vifaa hivyo wao kama wadhamini wa ligi kuu pia wamefarijika kuona timu zote zimefanya maandalizi ya kutosha.

 “Hii ni  ishara tosha kuwa siku hadi siku ligi yetu imeendelea kuimarika na kuwa na ushindani mkubwa zaidi hakika tunajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya soka nchini,” alisema.

Twissa alihitimisha kwa kutoa wito kwa wadau wengine wenye malengo ya kukuza soka la Tanzania kujitokeza na kuongeza udhamini katika ligi ili kuleta tija zaidi huku akiendelea kuwakumbusha wanahabari wajibu wao wa kuitangaza ligi hususan vipaji.

CHANZO:BIN ZUBEIRY


KIM POULSEN AMEWAITA KAMBINI WACHEZAJI 24 KUIVAA GAMBIA



PICHA NA MAKTABA:

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amewaita kambini wachezaji 24 kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu nchini humo.

Wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini Agosti 29 mwaka huu kabla ya saa 1 kamili usiku. Kambi ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa kwenye hoteli ya Accommondia jijini Dar es Salaam.

Makipa walioitwa katika timu hiyo Juma Kaseja (Huru), Mwadini Ali (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Erasto Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na David Luhende (Yanga).

Viungo Khamis Mcha (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Dilunga (Ruvu Shooting), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Amir Kiemba (Simba), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga), John Boko (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na Juma Liuzio (Mtibwa Sugar).
CHANZO:TFF


SERIKALI YA RWANDA YATUPILIA MBALI USHAURI WA TANZANIA.


Mushikiwabo alisema wako tayari kuwapokea na kuwalinda wote waliofukuzwa Tanzania kwa kisingizio kuwa ni wahamiaji haramu, akieleza kwamba anasikitishwa kwa kuwa Tanzania haikufanya jitihada yoyote kuwasiliana na Rwanda kuhusu suala hilo kabla ya kuchukua uamuzi huo (HM).


"Ni uamuzi ambao umeshachukuliwa, hatukushirikishwa kwa namna yoyote na jukumu letu kama serikali na taifa ni kuwahakikishia ulinzi wote wanaokuja, na hili ndilo suala tunalolishughulikia kwa sasa," alisema.

Kwa mujibu wa gazeti la New Times, Mushikiwabo aliwaeleza waandishi wa habari kwamba agizo hilo la Rais Kikwete pamoja na ushauri wa kuitaka Serikali ya Rwanda kuzungumza na wanamgambo hasimu wa FDLR waliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hayatayumbisha uhusiano imara baina ya Watanzania na Wanyarwanda.

"Sisi si majirani tu, tuna mfungamano imara baina ya watu wetu pia, tuna mfungamano wa damu, wa kibiashara, na mengine mengi ya kutufanya tuendelee kuwa pamoja," alisema na kutumia fursa hiyo kuwakaribisha Watanzania nchini Rwanda.

Watanzania wanaweza kuishi hapa kwa umri wowote wanaotaka. Tunawachukulia kuwa ni watu wetu muhimu kwenye fungamano la Jumuiya ya Afrika Mashariki," alisisitiza.

Rais Kikwete wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kagera alitoa agizo la kuwataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu ama kuondoka au kuhalalisha ukazi wao, huku akitoa wiki mbili kwa zoezi hilo kutekelezwa, kabla ya kuanza kwa operesheni ya kuwasaka watu hao.

Kauli hiyo ilitokana na kushamiri vitendo vya kihalifu katika eneo la Kanda ya Ziwa, Rais hakutaja jina la nchi ya wahamiaji hao. Kwa ukanda huo Tanzania inapakana na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC.

Pia, Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi alizungumzia kusikitishwa na kauli za shutuma, kejeli na udhalilishaji zilizotolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda dhidi yake.

Mvutano baina ya Rwanda na Tanzania ulianza kuwekwa hadharani Mei mwaka huu, baada ya Rais Kikwete kuishauri Rwanda kukaa na kuzungumza na FDLR wenye makao yao DRC, hatua ambayo haikuifurahisha Serikali ya Rwanda.

Wakati Rwanda ikieleza hayo jana Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alizungumza na gazeti hili, na kutaka majibu ya kauli hiyo ya Rwanda yatolewe na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ally alisema kauli iliyotolewa na Rais Kikwete ilikuwa ni ushauri, kwamba Rwanda wanaweza kuukubali ama la.

"Kilichomkasirisha Rais Kikwete ni lugha za matusi zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa Rwanda, ila kwa hicho walichokisema sidhani kama kitakuwa na tatizo kwetu," alisema Mkumbwa.

Alifafanua kwamba, alipokuwa mkoani Kagera Rais Kikwete hakutoa agizo la Wanyarwanda kufukuzwa, bali alitoa agizo la kuanza kwa operesheni ya kuwakamata wahamiaji haramu, wale wanaomiliki silaha kinyume na taratibu.

"Rais alizungumzia masuala ya jinai 'Criminal Element', siyo kuwafukuza Wanyarwanda," alisisitiza.

Hatutazungumza na FDLR
Waziri wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo, aliendelea kusema sera ya Rwanda kuhusiana na makundi ya aina hiyo, iko wazi na haitabadilika, kauli ambayo amekuwa akiirudia kila mara na kuwataka wote wanaofikiria kuhusu Rwanda kuzungumza na FDLR kwa namna yoyote kusahau wazo hilo.

"Kama umehusika kwa namna yoyote na maangamizi, wewe utakuwa adui wa kila mtu. Ni wazi kwamba Wanyarwanda wote watakuwa kwenye majonzi iwapo kwa namna yoyote kutakuwa na mawasiliano ya FDLR," alifafanua.

Kundi la FDLR ambalo ni kifupisho cha Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, linaundwa na watu walioshiriki kwenye mauaji ya kimbari yaliyowalenga watu wa kabila la Watutsi mwaka 1994, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800,000 kwa miezi mitatu.

Kundi hilo ambalo limeweka makazi yake mashariki mwa DRC, linadaiwa kufanya mashambulizi kadhaa yakiwamo ya milipuko ya mabomu nchini Rwanda, ambapo mwezi uliopita shambulio la aina hiyo mjini Kigali lilisababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi watu kadhaa.

Uhusiano wa kihistoria
Familia za Rwanda zikiwamo zilizoishi Tanzania tangu miaka ya 1950, zimeelezwa kuwa zimekuwa zikiwasili nchini humo kupitia mpaka wa Rusumo baada ya agizo la Rais Kikwete kuwataka wawe wameondoka ndani ya wiki mbili, kabla ya kuanza kwa operesheni rasmi ya kuwaondoa.

Kwa mujibu wa mamlaka nchini Rwanda, mamia ya Wanyarwanda waliokuwa wakiishi mkoani Kagera ambako ndiko Tanzania inapopakana na Rwanda wamekuwa wakirejea kwa wingi, ambapo hadi juzi, zaidi ya watu 300 walikuwa wameshaorodheshwa kwenye ofisi za Uhamiaji. CHANZO:MWANANCHI

 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU