Facebook Comments Box

Wednesday, August 21, 2013

KATIBU MTENDAJI MPYA WA SADC APOKELEWA KWA SHANGWE WIZARA YA MAMBO YA NJE


Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akimlaki kwa furaha Katibu Mtendaji mpya wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),  Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax mara baada ya kuwasili Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mhe. Membe akimkabidhi shada la maua Dkt. Tax kwa niaba ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje mara baada ya kuwasili Wizarani hapo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule nae akimkarisha Dkt. Tax kwa furaha Wizarani.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Irene Kasyanju akimpongeza kwa shada la maua Dkt. Tax mara nbaada ya kuwasili Wizarani.

Dkt. Tax akipongezwa na kukaribishwa Wizarani na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Rajabu Gamaha.
Balozi mpya  wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz, nae pia aliungana na Wafanyakazi wa Wizara kumpongeza dkt. Tax. Anayeshuhudia pembeni ni Bw. Ali Mwadini, Katibu wa Naibu Waziri. 
Dkt. Tax akipongezwa na Bw. Omar Mjenga, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Asia na Australasia huku Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. James Lugaganya (kushoto) akishuhudia.
Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Diaspora akimlaki kwa shangwe Dkt. Tax wakati wa mapokezi.
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Simba Yahya nae akitoa pongezi zake za dhati kwa Dkt. Tax
Maafisa mbalimbali wa Wizara nao pia walikuwa mstari wa mbele kumpongeza Dkt. Tax.
Dkt. Tax akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka kwa Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku Mhe. Membe akishuhudia.
Mhe. Membe akifurahia jambo na Makatibu Wakuu wakati Dkt. Tax akisaini Kitabu cha Wageni.Picha na Reginald Philip.


MSANII WA BONGO FLEVA NASEEB ABDULMALIKI a.k.a DIAMOND ATAJWA SAKATA LA MADAWA YA KULEVYA




Utajiri, safari zake nje ya nchi vyatiliwa shaka
*Ahusishwa na mtandao hatari wa Masogange


KWA mara ya kwanza tangu lilipoibuka sakata la watu maarufu kujihusisha ama na utumiaji au usafirishaji wa dawa za kulevya, jina la mwanamuziki anayeaminika kuwa na ukwasi mkubwa kwa sasa hapa nchini, Nasseeb Abdulmaliki, maarufu zaidi kwa jina la Diamond, limeanza kutajwa kuwa ni miongoni mwa vigogo wa dawa hizo.

Tayari mjadala mkubwa wa chini chini umeibuka kwa watu mbalimbali wakiwemo mashabiki wake, na taarifa ambazo zimelifikia MTANZANIA Jumatano kutoka vyanzo mbalimbali zimedai kuwa, mwenendo wa maisha ya Diamond sasa unachunguzwa na baadhi ya maofisa wa vyombo vya dola vya ulinzi na usalama.

Kutajwa kwa jina la Diamond katika sakata hili, kunatiwa nguvu zaidi na mwenendo binafsi wa maisha wa msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi kipya, unaokwenda sambamba na ukwasi mkubwa alioupata katika kipindi kifupi.

Kama hiyo haitoshi, safari za nje ya nchi za mwanamuziki huyo unaohusisha ziara zake nchini Afrika Kusini na Uingereza, pia ni mambo ambayo yamechochea wingu la mashaka lililofikia hatua ya jina lake kuingizwa katika mtandao huo ambao katika siku za karibuni, umewagusa pia baadhi ya watu wenye majina makubwa katika jamii.

Kuhusu ziara hizo, kilicholeta mshtuko na dukuduku dhidi yake ni kuwapo kwa taarifa kwamba, katika moja ya ziara hizo za nje ya nchi, Diamond alifikia hatua ya kusafiri akitumia chumba kinachotumiwa na wageni mashuhuri (VIP), badala ya njia ya wasafiri wa kawaida.

Mbali na hilo, taarifa nyingine zinaeleza kwamba, mizigo ya msanii huyo ambaye mara kadhaa amekuwa akisafiri na kundi la wacheza shoo wake, imekuwa ikipita pasipo kupitishwa katika hatua za ukaguzi kwa namna ile ile ilivyokuwa kwa mabinti wawili wa Kitanzania walionaswa nchini Afrika Kusini baada ya kuruka mfumo wa ukaguzi wa JNIA.

Aidha, ukaribu wa kimahusiano kati ya Diamond na baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini na ambao majina yao pia yameanza kuhusishwa na biashara hiyo ya mihadarati, ni jambo jingine ambalo limechochea harakati za kufuatiliwa kwa karibu kwa nyendo za Diamond.

Taarifa zaidi kutoka JNIA zinaeleza kwamba, miongoni mwa watu wanaoweza wakawa wamemponza Diamond ni wale ambao walionekana kuwa karibu na Agness Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), siku walipokuwa wakisafiri kwenda Afrika Kusini kabla hawajanaswa katika uwanja wa Ndege wa Oliver Thambo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, wakiwa na shehena ya dawa za kulevya.

Mwenendo wa watu hao unatiliwa shaka kuwa huenda ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wenye maskani yao nchini Afrika Kusini, kwa sababu mbali na ukaribu na wasichana hao, pia walihusika kwa karibu kuusafirisha mwili wa mwanamuziki Albert Mangwair, aliyefia huko huko Afrika Kusini ambaye taarifa za kufa kwake ziligumbikwa na matumizi ya dawa za kulevya.

Alipoulizwa jana na MTANZANIA Jumatano kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu taarifa hizo na iwapo amekwishahojiwa na vyombo vya dola baada ya jina lake kuanza kutajwa kuwa miongoni mwa orodha ya wasanii wa muziki wanaosafirisha dawa za kulevya, Diamond alikiri kuwa na pesa za kutosha kuishi maisha anayoyataka, lakini akakana kujihusisha na biashara hiyo.

Akifafanua tuhuma moja baada ya nyingine kwa mpangilio aliokuwa akiulizwa na gazeti hili, Diamond alisema katika maisha yake, hajawahi kujihusisha na utumiaji au usafirishaji dawa za kulevya, lakini madai hayo yamekuwa yakitolewa dhidi yake na watu ambao hawajui siri ya mafanikio yake.

“Kazi ngumu siku zote inalipa, sasa napata matunda ambayo yanatokana na kile nilichokifanya, iweje watu wanitilie mashaka, Watanzania ni mashahidi wangu wananiona navyochumia juani, nitaendelea kulia kivulini tu kwani nakula kwa jasho langu.

“Siyo kweli kwamba mizigo yangu haikukaguliwa na kama haikukaguliwa na ingekuwa na kasoro, basi Uingereza wangenitia hatiani, nilipita na nilikaguliwa.” Alisema Diamond.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za kuwa mwanamtandao wa kundi la Masogange, pia alikanusha kwa kueleza kuwa hata siku aliyosafiri kwenda Afrika Kusini alikwenda peke yake uwanja wa ndege na kuongeza kuwa alikwenda huko kwa shughuli za kimuziki, ambapo safari nzima iligharimu zaidi ya Dola 30,000 za Kimarekani.

“Afrika Kusini nimekwenda kufanya kazi zangu na safari hiyo imenigharimu zaidi ya Dola 30,000, nilikwenda kurekodi nyimbo yangu mpya inayoitwa namba moja ambayo itaanza kusikika hivi karibuni.

“Unajua Watanzania sasa hivi wanajua mtu hawezi kufanikiwa au kupata maendeleo bila kuuza ‘unga’, hili si sawa juhudi za mtu ndizo zinamfikisha alipo, na mimi juhudi zangu ndio zinanifikisha hapa, watu waache kunijadili vibaya.” Alisema Diamond.

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja ikiwa ni takribani miezi miwili sasa tangu Watanzania wawili, Agness Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), waliokuwa na uhusiano wa karibu na baadhi ya wanamuziki maarufu hapa nchini, kukamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh bilioni 6.8.

Mbali na kuwa na uhusiano wa karibu na wanamuziki, Edward anadaiwa kuwa alikuwa mfanyakazi katika mgahawa mmoja maarufu jijini Dar es Salaam, unaomilikiwa na mmoja wa vijana matajiri hapa nchini ambaye hata hivyo gazeti hili halijafanikiwa kumpata ili kufanya naye mahojiano.

Wakati huo huo, tayari hatua za kinidhamu zimekwishaanza kuchukuliwa dhidi ya wafanyakazi wa JNIA waliohusika kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya, ambao Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametaja majina yao hivi karibuni na kuonyesha kwa waandishi wa habari ushahidi wa kuhusika kwao.

CHANZO:JAMII FORUMS



Tuesday, August 20, 2013

YANGA YABURUZA MKIA KATIKA MSIMAMO WA LIGI KUU YA TANZANIA BARA:

Kabla ya kuanza kwa Msimu wa ligi ya Vodacom Tanzania Bara msimamo huwa kama unavyoonekana hapo pichani, timu zimepangwa kwa kufuata mtiririko wa majina (Alphabetic Order) kwamba timu zenye herufi 'A' huwa zakwanza kama wanavyo onekana ASHANTI ya Ilala wakiwa juu kabisa ya msimamo huo wakati Mabingwa wa mwaka jana 2012 / 2013 YANGA wao wakiwa wanaburuza mkia.

Lakini mambo hugeuka pindi mtanange huo unaotarajiwa kuanza rasmi siku ya Jumamosi ya tarehe 24/08/2013 ambapo Ratiba ya siku hiyo timu zote 14 zitakuwa uwanjani kama ifuatavyo:-

YANGA vs ASHANT(U/Taifa), MTIBWA vs AZAM(Manungu), JKT OLJORO vs COASTAL UNION(Sh. Amri Abeid), MGAMBO JKT vs JKT RUVU(Mkwakwani), R.RANGERS vs SIMBA(Ally H.Mwinyi), MBEYA CITY vs KAGERA SUGAR(Sokoine), R.SHOOTING vs PRISONS(Mabatini).  





HALI SI SHWARI MISRI WAFUASI WA MORSI 38 WAUAWA GEREZANI



Kiongozi mmoja wa usalama nchini Misri ametangaza kuwa, wanachama 38 wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin wameuawa, katika tukio la mapigano kati ya askari polisi na watu waliokuwa na silaha, waliotaka kuwatorosha watu hao kutoka gerezani. 
 
Habari zinasema kuwa, mapigano hayo yalitokea karibu na jela ya Abu Zaabal katika mkoa wa al-Qalyubiyah. Aidha wafungwa hao walikuwa wamemteka polisi mmoja katika mapambano hayo.
 
 Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Misri imetangaza kuwa, polisi walifanikiwa kumuokoa polisi huyo ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya. Jana wafuasi wa Ikhwanul Muslimin walisitisha maandamano mjini Cairo kwa kile walichosema kuwa ni kuepusha umwagikaji damu zaidi dhidi yao.  
 
Ripoti iliyotolewa na harakati hiyo, ilisema kuwa, Ikhwan wameamua kusitisha maandamano yao, kutokana na kuwepo hali tete nchini humo. Kabla ya hapo, ilikuwa imepangwa kufanyika maandamano ya nchi nzima, kwa ajili ya kutaka kurejeshwa Muhammad Mursi, Rais halali wa Misri aliyepinduliwa na jeshi la nchi hiyo.




SAFARI NZIMA YA SHEIKH PONDA NA YALIYOJIRI

Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda alisafirishwa jana kwa helikopta kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa kujibu mashtaka yanayomkabili.

Ponda jana alianza kwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu asubuhi na kufutiwa mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili baada ya kusomewa mara ya kwanza Agosti 14, mwaka huu akiwa kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kumshtaki.

Alidaiwa kutenda makosa hayo katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano kati ya Juni 2 na Agosti 11 mwaka huu.

Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa 12 asubuhi na baadaye alipandishwa kizimbani na kufutiwa kesi hiyo, baada ya Wakili Kweka kuwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Hata hivyo, baada ya kufutiwa mashtaka hayo, aliendelea kushikiliwa na kisha akachukuliwa na kupelekwa Morogoro ambako pia alisomewa mashtaka ya uchochezi.

Kuwasili Moro

Sheikh Ponda aliwasili kwa helikopta ya polisi na kutua kwenye Uwanja wa Gofu, Morogoro akiwa chini ya ulinzi wa polisi na alipakiwa kwenye gari maalumu ambalo liliongozana na magari mengine matatu ya polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama ukiwajumuisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), askari wa upelelezi, Usalama wa Taifa pamoja na mbwa wa polisi na kusababisha shughuli za kazi katika Mahakama hiyo na ofisi za jirani kusimama kwa muda.

Baada ya kufika mahakamani saa tano asubuhi, magari yalisimama kwa takriban dakika 30 kabla ya kumtoa na kumwongoza kwenye Mahakama ya wazi ambayo tayari ilikuwa umejaa watu.

Baada ya kumalizika kusomwa kwa kesi hiyo, msafara uleule ulimrejesha Uwanja wa Gofu saa sita mchana na kupandishwa kwenye helikopta kurejea Dar es Salaam.

Mahakamani Morogoro

Ponda alisafirishwa kwa helikopta ya polisi hadi Morogoro na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi akiwa chini ya ulinzi mkali.

Wafuasi wa Ponda wapiga kambi Segerea

Mara baada ya kumfikisha katika Mahakama hiyo iliyofurika mamia ya waumini na wafuasi wake, Wakili wa Serikali, Bernard Kongola alimsomea mashtaka matatu yanayomkabili.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate alisema: “Agosti 10, mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro Ponda Issa Ponda, aliwaambia wafuasi wake.

“Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watakuja kwenu na watajitambulisha kwamba wao ni Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya msikiti yenu na muwapige sana.”

Kongola alisema kauli hiyo ilikuwa ikiumiza imani za watu wengine na kwamba hatua hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lililotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9, mwaka huu ikimtaka kuhubiri amani ndani ya mwaka mmoja na kwenda kinyume na kifungu cha Sheria namba 124 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Ponda alikana.

Katika shtaka la pili, Ponda anadaiwa Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro aliwaambia Waislamu kuwa Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.

Alisema Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo na kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine jambo ambalo ni kinyume cha Kifungu cha Sheria 129 cha mwaka 2002, shtaka ambalo pia alikana.

Shtaka la tatu linafanana na lile la pili lakini na upande wa mashtaka ulieleza kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine na kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha Kifungu 390 cha Sheria na Kanuni ya Adhabu namba 35 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Sheikh Ponda alilikana. Baada ya kusomwa kwa mashtaka yote matatu, wakili wa Serikali aliiambia Mahakama kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na kupanga kesi kuanza kusikilizwa Septemba 2 mwaka huu. Upande wa utetezi uliomba Mahakama kupanga kuanza kusikilizwa kwa kesi Agosti 26, mwaka huu.

Hakimu Kabate aliwapa mawakili kujadiliana na baadaye kuomba kesi hiyo ianze kusikilizwa Agosti 28 mwaka huu.

Wakili alalamika

Akizungumza Dar es Salaam jana, Wakili wa Ponda, Juma Nassoro alilaani kitendo cha kuondolewa kwa mteja wake gerezani na kwenda kusomewa mashtaka mapya Morogoro bila taarifa.

Alidai kuwa polisi wanaendelea kukiuka taratibu za kumshikilia kiongozi huyo kutokana na kufanya mambo kinyume na sheria kwa lengo la kutaka waumini kufanya vurugu ili waendelee kumshikilia kiongozi huyo.
“Kitendo cha kumuondoa mteja wangu gerezani na kwenda kumsomea shtaka jingine Morogoro nimelilaani. Sijalipenda. Polisi hawakuwa na nia nzuri na Ponda kwa sababu sheria zinajulikana na kila mtu ana haki ya kutetewa,” alisema Nassoro.

Akizungumzia kufutiwa kesi Mahakama ya Kisutu, Nassoro alisema Serikali imeamua kufuta kesi kabla ya kusikilizwa baada ya kuona imeelemewa kwani alishapeleka maombi ya kuirudisha Mahakama Kuu kutoka Kisutu kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na maombi hayo yalipewa namba 11/2013.

Msemaji wa familia, Isihaka Rashidi alisema: “Hawa jamaa wamempeleka Morogoro kwa siri kwa sababu jana (juzi) tulikwenda Segerea hakukuwa na hizo taarifa. Tumekuja kushtuka asubuhi baada ya mke wake kwenda kumpelekea chai na kuambiwa ameondolewa na kupelekwa Morogoro.”

Alisema baada ya kupata taarifa hizo iliwalazimu kuwasiliana na ndugu zao waliopo Morogoro kwa ajili ya kwenda mahakamani kusikiliza kesi hiyo.

*Imeandikwa na Lilian Lucas na Hamida Sharrif (Morogoro), James Magai, Aziza Masoud na Aidan Mhando, Dar. (Gazeti la Mwananchi)



PROF WARIOBA ATEULIWA NA RAIS KUWA MKURUGENZI WA TSN



UDA YAPELEKA MABASI MIKOANI KWA AJILI YA WANAFUNZI: YAWEKA PIA MABASI KWA AJILI YA WANAWAKE NA WALEMAVU

Wanafunzi wa mikoa mbalimbali nchini wataondokana na kero ya usafiri wa daladala baada ya kampuni ya UDA kuingiza magari 10 kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi ili kuwahi masomo.

Aidha, wanawake, wanaume na watu wenye ulemavu watakuwa na mabasi maalumu ambayo yatatoa huduma mikoani. 

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Ofisa Rasilimaliwatu wa UDA, Cyprian Malekela alipozungumza na waandishi wa habari jinsi kampuni hiyo inavyopambana na changamoto za usafiri ukiwamo uboreshaji wa huduma za usafiri mikoani.

Alisema kampuni hiyo kwa kuanzia, itatoa mabasi 10 ya wanafunzi kila mkoa na itaanza na Mwanza, Dodoma, Iringa, Mbeya na Arusha na sasa iko katika hatua ya mwisho ya mazungumzo na walimu wakuu wa shule za
msingi na sekondari ili kujua vituo watakavyopandia wanafunzi na muda wa kuwachukua na kuwarudisha.

Malekela alisema kampuni hiyo itakuwa na magari mengine 15 ya wanawake ambao hawawezi kugombania magari, 10 kwa ajili ya wanaume huku mengine sita yakiwa ni maalumu kwa watu wenye ulemavu.

"Kampuni imedhamiria kuboresha huduma zake kwa kuongeza idadi ya magari kwa ajili ya wanafunzi, wanawake, walemavu na wanaume lengo ni kutoa huduma za usafiri kila mkoa ili kuboresha huduma ya usafiri na kuondoa kero kwa wananchi wanaohitaji usafiri wa uhakika," alisema.

Aliongeza kusema kwamba awali kampuni hiyo kabla haijabinafsishwa ilikuwa ikimilikiwa na Serikali huku ikiwa na magari saba, lakini sasa iko mikononi mwa Mtanzania ambaye ameongeza idadi ya magari hadi 40.

Alisisitiza kuwa UDA imedhamiria kuboresha huduma za usafiri kila mkoa na kutoa rai kwa wamiliki wa kampuni na taasisi nchini kukodisha magari hayo ili yatoe huduma na hata madereva na wahudumu wa mabasi ya UDA wamepewa mafunzo maalumu ya kuhudumia abiria. -- HabariLeo



PICHA: KWA UCHACHE MAANDAMANO YA CHADEMA MWANZA

Chini ni picha kwa uchache maandamano ya wafuasi wa chadema jijini Mwanza kwa ajili ya kumng'oa meya wa jiji hilo.  Wafuasi hao wanadai hana uhalali wa kuwa madarakani



PICHA: WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YA SKOL WAKIFANYAKAZI BILA VIFAA MAALUMU VYA KAZI

Picha chini ni wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya Skol ambao kwa sasa wanatengeneza barabara ya tabata wakiwa wanasafisha barabara eneo la tabata posta bila vifaa vya kuzuia vumbi puani mwao.



PICHA: CHADEMA MKOANI KAGERA KATIKA KUJADILI KATIBA MPYA

Picha chini zikionesha viongozi wa ngazi za juu wa chama cha demokrasianna maendeleo chadema walivyofika mkoanI Kagera katika kujadili kuhusu mabaraza ya katiba mpya na katiba mpya kwa ujumla.



Monday, August 19, 2013

JENGO MALI YA WAISLAM LILILO BINAFSISHWA NA BAKWATA LAVUNJWA

Jengo la Bakwata lililopo kwenye makutano ya Barabara ya Morogoro na Bibi Titi jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia juzi lilibolewa ghafla wakati mali za wapangaji zikiwemo ndani na kusababisha hasara kubwa ya
uharibifu na upotevu wa mali.

Chanzo kimoja cha habari eneo hilo kimedai kuwa BAKWATA wamelibinafsisha jengo hilo kwa mwekezaji kutoka nje ya nchi bila kuwashirikisha wapangaji wake. Mwekezaji huyo ndiye anayedaiwa kutoa agizo la kubomoa jengo hilo kabla ya notisi aliyoitoa kwa wapangaji hao kumalizika.



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU