TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
09/06/2013
MAONI YA AWALI YA MWENYEKITI WA CUF KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA
UTANGULIZI;
Kwanza
naipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kazi kubwa waliofanya ya kuratibu
maoni na kuja na mapendekezo ya katiba mpya ambayo hayakushinikizwa na
matakwa ya Chama tawala cha CCM. Tume imeonyesha ujasiri mkubwa na
hakika wahafidhina wa chama hicho watachukia sana.
Mambo mengi
yaliyopendekezwa na Chama Cha Wananchi CUF yameingizwa katika Rasimu ya
Katiba. Mambo hayo ni pamoja na mfumo wa Muungano wa serikali tatu,
kuruhusiwa mgombea binafsi, Rais kutangazwa kushinda akipata zaidi ya
asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa la sivyo uchaguzi urudiwe kwa wale
wawili walio ongoza kwa kura, Tume huru ya uchaguzi, Mawaziri kutokuwa
wabunge, Spika kutokuwa mbunge, haki za watu wenye ulemavu, haki za
binadamu na mengine mengi.
Hata hivyo mambo mengi muhimu kama
vile umilikaji wa ardhi, maliasili na rasilimali za nchi kutumiwa kwa
manufaa ya wananchi wote, elimu, afya, mazingira ya kukuza uchumi
unaoleta neema kwa wananchi wote, wajibu, uwezo na uhuru wa serikali za
mitaa hayajaingizwa ndani ya katiba kikamilifu kwani rasimu ya katiba
imeshughulikia mambo ya muungano.
Mambo ya Muungano ni saba:
Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki
Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa
Vyama vya Siasa na Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mwongozo wa Tume kuhusu utoaji wa maoni ulijikita katika maeneo yafuatayo;
Misingi
na Maadili ya Kitaifa, Madaraka ya Wananchi, Muundo wa Nchi na Taifa
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Haki za Binadamu na Wajibu wa
Wananchi, Ardhi, Maliasili na Mazingira, Mihimili ya Nchi (Ardhi, Watu
na Utawala), Mihimili ya Utawala (Serikali, Bunge na Mahakama), Serikali
za Mitaa, Muundo na Mamlaka yake, Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Mambo
mengi muhimu kwa mwananchi wa kawaida ikiwa ni pamoja na serikali za
mitaa, umilikaji wa ardhi, haki za huduma za afya na elimu, na matumizi
ya maliasili hayajaingizwa katika katiba hii na yanatarajiwa kuingizwa
kwenye katiba ya Tanzania Bara. Rasimu ya katiba kwa wananchi wa
Tanzania Bara haijakamilika mpaka Rasimu ya katiba ya Tanzania Bara
itakapokuwa tayari. Hotuba ya uzinduzi wa katiba ya Jaji Warioba
haikulifafanua suala hili. Hakuna mantiki ya kupigia kura ya maoni
katiba ya jamhuri ya muungano bila kuwa na katiba ya Tanzania Bara kwa
upande wa bara na marekebisho ya katiba ya Zanzibar isikinzane na katiba
ya jamhuri ya muungano kwa upande wa zanzibar. Katiba ya Tanzania Bara
na katiba ya Zanzibar iwe ni sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kuwepo
kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara kutasaidi kuondoa kuweka asasi
mbili au tatu zinazofanya kazi moja. Kwa mfano Tume ya Uchaguzi, Jeshi
la Polisi, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Taasisi ya kuzuia
na kupambana na rushwa ya serikali ya Muungano ikafanya kazi pia kwa
serikali ya Tanzania Bara ikiwa wananchi wa Tanzania Bara hawana tatizo
na utaratibu huo.
MAPENDEKEZO YA JUMLA;
- Pendekezo
langu la msingi ni kwamba, kura ya maoni isubiri kukamilishwa kwa
rasimu ya katiba ya Tanzania Bara na zote zikajadiliwa na wananchi kwa
pamoja. Sina pingamizi kuwa Wajumbe wa Tume wa Tanzania Bara waandae
rasimu ya Katiba ya Tanzania Bara, na wajumbe wa Zanzibar waandae
mapendekezo ya marekebisho ya katiba ya Zanzibari ili isikinzane na
katiba ya Jamhuri ya Muungano. Muda wa kuyatekeleza haya na kubadilisha
sheria zifuate matakwa ya katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015
haupo. Serikali imeeleza kuwa haina nia na Rais Kikwete hataki kabisa
kujiongezea muda kwa kisingizio cha kukamilisha utaratibu wa katiba
mpya. Wananchi pia wamechoka wanataka mabadiliko.
- Katika
masuala ya haki za binadamu ningependa Katiba itamke wazi kuwa mwanamke
mjamzito ana haki ya kupata lishe bora na huduma za afya wakati wa
ujauzito na kujifungua. Vile vile watoto bila kujali uwezo wa wazazi wao
wana haki ya lishe bora, huduma za msingi za afya na elimu inayomuandaa
mtoto kukabiliana na changamoto za maisha.
- Pendekezo la
Rasimu ya Katiba ya kuwepo Tume Huru ya Uchaguzi ni la msingi.
Pendekezo hili lianze kufanyiwa kazi mara moja ili kufanya mabadiliko ya
sheria ya uchaguzi na Tume ya uchaguzi ili uchaguzi wa 2015 uendeshwe
na Tume iliyo Huru kweli. Mchakato wa mabadiliko ya katiba utaendelea
baada ya uchaguzi mpaka ukamilike na sheria husika kufanyiwa mabadiliko.
- Siyo
lazima Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wawe watu
waliyewahi kushika wadhifa wa Jaji wa Makakama ya Juu, Mahakama ya
Rufani au Mahakama Kuu na ameshika wadhifa huo kwa kipindi kisichopungua
miaka mitano kama Rasimu ya Katiba inavyoelekeza katika kifungu 181(4).
Masuala ya kusimamia uchaguzi ni ya utawala na uendeshaji kuliko ya
kutafsiri sheria. Majaji siyo wasimamizi na mameneja wazuri wa utawala
na logistics. Nchini Ghana mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ambaye kafanya
vizuri siyo Jaji bali ni Profesa wa sayansi ya siasa – Jaji Lewis
Makame kwa miaka zaidi ya 15 na hakufanikiwa kujenga Tume ya Uchaguzi
yenye uwezo na kuaminika. Ni vyema wigo wanaoweza kuomba kuwa wenyeviti
wa Tume ukapanuliwa na kuingiza wenye uzoefu wa utawala na logistics.
Tume ina mwanasheria wake ambaye ataelekeza na kushauri masuala yahusiyo
sheria.
- Kasoro kubwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
ni kwamba haina nyenzo za kutimiza malengo muhimu ya katiba yenyewe.
Ibara ya 6(b) imeeleza kuwa “lengo kuu la Serikali litakuwa ni maendeleo na ustawi wa wananchi.”
Mambo ya uchumi yote isipokuwa Benki Kuu na sarafu hayamo katika orodha
ya mambo ya Muungano. Hata suala la uratibu wa sera za uchumi halimo.
Ibara ya 7(2) inaeleza “mamlaka ya nchi na vyombo
vyake vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote kwa lengo la
kuhakikisha kwamba: (c)Serikali itahakikisha kuwa shughuli zinazofanywa
zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa
unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa
jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine; (d)ardhi ikiwa
rasilimali kuu na msingi wa Taifa, inalindwa, inatunzwa na kutumiwa na
wananchi wa Tanzania kwa manufaa, maslahi na ustawi wa kizazi cha sasa
na vizazi vijavyo; (e)maendeleo ya uchumi wa Taifa yanapangwa na kukuzwa
kwa ulinganifu na kwa pamoja na kwa namna ambayo inawanufaisha wananchi
wote; (f)kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi
maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu kipato chake;
(j)utajiri wa rasilimali na maliasili za Taifa unaelekezwa katika kuleta
maendeleo, kuondoa umaskini, ujinga na maradhi”. Serikali ya Muungano haina nyenzo ya kusimamia mambo hayo.
- Ibara ya 11 inazungumzia utekelezaji wa malengo ya taifa. Kifungu (2) kinaeleza “Serikali
itatoa taarifa Bungeni si chini ya mara moja katika kila mwaka, kuhusu
hatua zilizochukuliwa na mamlaka ya nchi ili kuhakikisha utekelezaji wa
malengo ya Taifa yaliyoainishwa katika Katiba hii. (c) kiuchumi,
Serikali inachukua hatua zinazofaa ili: (i) kuwaletea wananchi maisha
bora kwa kuondoa umaskini; (ii) kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali
zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kuwa utajiri wa Taifa
unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa
jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine; (iii) kuweka mazingira
bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa
wakulima, wafugaji na wavuvi; (iv) kuweka mazingira bora ya kufanya
biashara na kukuza fursa za uwekezaji; (v) kuweka mazingira bora kwa
ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima,
wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na nyenzo kwa ajili ya kuendeleza
shughuli zao; (vi) kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa mazao kwa
wakulima, wafugaji na wavuvi, utafutaji na uendelezaji wa masoko ya
mazao yao; (vii) kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji wa
mizania ya bei za mazao na pembejeo; (viii) kuimarisha na kuendeleza
uwekezaji wa ndani, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, maeneo ya ufugaji
na vifaa vya uvuvi; (ix) kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa fursa
na nafasi za wazi kwa watu wote na kuanzisha shughuli za kiuchumi na
kukuza mazingira yaliyo bora kwa ajili ya kuhamasisha sekta binafsi
katika uchumi; (x) kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya
kazi anapata fursa ya kufanya kazi, kwa maana ya kufanya shughuli yoyote
halali inayompatia kipato; (xi) kuweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya
kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kujipatia elimu na kuwa huru
kupata fursa sawa ya kutafuta elimu katika fani anayoipenda hadi kufikia
upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake. Mambo yote haya siyo ya
muungano”. Serikali ya Muungano itawezaje kutoa taarifa Bungeni kwa mambo ambayo haiyasimamii.
- Ukizingatia
mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa na Rasimu, Serikali ya Muungano
haina vyanzo vya mapato ya kodi. Ibara ya 215 imeeleza Vyanzo vya mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakuwa:“(a)
ushuru wa bidhaa; (b) maduhuli yatokanayo na taasisi za Muungano; (c)
mchango kutoka kwa Washirika wa Muungano; na (d) mikopo kutoka ndani na
nje ya Jamhuri ya Muungano”. Katiba haizungumzii taasisi yeyote ya kukusanya kodi. Jambo
la saba la muungano ni Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi
yatokanayo na mambo ya Muungano. Mambo sita ya Muungano hayalipi ushuru
wa bidhaa. Biashara siyo jambo la Muungano kwa hiyo ushuru wa
forodha, kodi za ongezeko la thamani (VAT), excise duty, kodi ya mauzo
haziwezi kuwa suala la Muungano. Mwaka wa fedha wa 2010/11
Mapato ya serikali Asilimia 34.3 ushuru wa forodha na VAT katika bidhaa
zinazoagizwa toka nje, Asilimia 18.6 kodi (VAT na Excise duty) za bidhaa
zinazozalishwa ndani ya nchi. Asilimia 29 kodi ya mapato. Kodi na tozo
nyingine asilimia 10.5, Mapato ya halmashauri asilimia 2.8. Kodi ni
chanzo cha mapato ya serikali lakini pia ni sera ya uchumi. Viwango gani
vya kodi havina athari kubwa kwa wananchi maskini na kupunguza motisha
ya uzalishaji na uwekezaji? Serikali za washirika wa Muungano
hawatakubali Serikali ya Muungano kutoza kodi katika maeneo ambayo siyo
ya muungano. Katiba haina muongozo wowote wa michango toka
washirika wa Muungano. Rasimu hii ilivyo ikipitishwa kutakuwa na mgogoro
mkubwa wa fedha za kuendeshea serikali ya Muungano na hatma yake
itakuwa Muungano kuvunjika.
- Katika mambo ya
uchumi Tume haikufanya uchambuzi wa kina wa kuwa na katiba inayojenga
mazingira mazuri ya kukuza uchumi unaoleta maendeleo kwa wote. Katiba
haiibani serikali iwe na utaratibu mzuri wa bajeti. Katika mambo ya
usimamizi wa matumizi ya serikali na kazi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali rasimu hii ime –“copy” na ku-“paste” katiba ya sasa bila kutathmini kama mfumo wa hivi sasa unafanya kazi. Eneo hili linahitaji kufanyiwa uchambuzi zaidi.
- Ibara za 213 na 214 zinawapa uwezo Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mshirika wa Muungano “zitakuwa
na mamlaka ya kukopa fedha ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano kwa
ajili ya kugharamia shughuli zilizo chini ya mamlaka yake.” Katika utaratibu huu nchi inaweza kughubikwa na madeni ikiwa serikali tatu zitashindana kukopa ndani na nje ya nchi. Lazima pawe na mwongozo wa kudhibiti mikopo na kuongezeka kwa deni la taifa. Nchi inaweza kuingizwa katika mgogoro wa madeni. Uhuru wa serikali zote tatu kukopa ndani na nje ya nchi inaweza kusababisha kukua kwa madeni kupita kiasi.
Serikali za washirika zina vyanzo vya mapato serikali ya muungano
haina. Kwa Rasimu ya Katiba hii serikali za washirika ndizo
zinazokopesheka na siyo serikali ya muungano.
- Rasimu ya Katiba bila kusema hivyo inapendekeza kuwepo na Benki Kuu tatu. Ibara ya 217 inaeleza“Kutakuwa
na Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayojulikana kuwa
“Benki Kuu” ambayo itakuwa na majukumu yafuatayo: (a) kutoa sarafu,
kudhibiti na kusimamia mzunguko wa sarafu; (b) kuandaa na kusimamia Sera
na Mipango inayohusiana na sarafu; (c) kudhibiti na kusimamia masuala
ya fedha za kigeni; na (d) kusimamia Benki za Washirika wa Muungano.” Ibara ya 218 inaeleza “Serikali
za Washirika zitakuwa na Benki zitakazokuwa najukumu la kutunza akaunti
ya fedha za Serikali husika, kusimamia Sera za Kifedha na benki za
biashara katika mamlaka zao.” Kazi ya Benki Kuu ni kusimamia Benki
za Biashara, sera za fedha na hasa riba, na mfumo wa malipo. Kazi hizi
zitafanywa na Benki za Washirika wa Muungano.Moja ya chanzo cha mgogoro wa Euro ni
kutokuwepo usimamizi wa pamoja wa Benki za biashara. Hivi sasa Ukanda
wa Euro unajaribu kuandaa utaratibu wa pamoja wa kuifanya Benki Kuu ya
Ulaya (ECB) kusimamia Benki za Biashara. Kama tuna sarafu moja
tuwe na Benki Kuu moja. Benki Kuu isiposimamia benki za biashara
haitaweza kudhibiti na kusimamia ujazi wa fedha (money supply)
- Ibara ya 105 inaeleza “(2)
Wajumbe wa Bunge watakuwa wa aina zifuatazo: (a) Wabunge waliochaguliwa
kuwakilisha majimbo ya uchaguzi; (3) Kwa madhumuni ya Ibara ya ndogo
(2)(a), kila mkoa kwa upande wa Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa
Zanzibar, itakuwa ni jimbo la uchaguzi”. Nini vigezo vya kufanya
mikoa na wilaya kuwa majimbo ya uchaguzi? Utaratibu wa kuanzisha mikoa
na wilaya ni wa serikali washirika au wa Serikali ya Muungano? Hata
hivyo ibara ya 180 (a) inaeleza “mamlaka zinazosimamia uchaguzi kutangaza majimbo kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge.” Majimbo ya uchaguzi yataundwa na Tume au tayari yameishatajwa na katiba?
- Mamlaka ya Bunge katika kuisimamia serikali katika masuala ya bajeti ni madogo. Ibara ya 107 (2) inaeleza, “katika
kutekeleza majukumu yake, Bunge litakuwa na madaraka yafuatayo: (c)
kujadili mgawanyo na kuidhinisha matumizi ya fedha kwa Wizara, taasisi
na mashirika ya Serikali; (d) kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati
wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti; (e) kujadili na
kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa
kutekelezwa na Serikali katika Jamhuri ya Muungano; (f) kutunga sheria
ya kusimamia utekelezaji wa mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi”. Hata hivyo Mambo ya Muungano hayahusishi Mpango wa Maendeleo wa taifa.
- Ibara ya 177 inaeleza “Bila
ya kuathiri masharti ya Katiba hii, utumishi wa umma na uongozi katika
Jamhuri ya Muungano utazingatia misingi kwamba utoaji wa ajira na uteuzi
wa viongozi utakuwa kwa uwiano baina ya Washirika wa Muungano, kwa
kuzingatia weledi na taaluma katika eneo au nyanja husika.” Nini maana ya uwiano? Je maana yake nusu ya wafanyakazi watoke Zanzibar na nusu watoke Tanzania Bara?
- Taasisi
ya kuzuia na kupambana na rushwa ni muhimu iwemo ndani ya Katiba.
Rasimu haina asasi hii muhimu ya usimamizi na uwajibikaji. Tunarudia
pendekezo letu kuwa Katiba ieleze kuwepo kwa Tume ya Kupambana na Kuzuia
Rushwa na kueleza kazi zake. Tume hii iwe na uhuru wa kupeleka kesi
mahakamani bila idhini ya Mkurungezi wa Mashtaka ya Umma (DPP).
- Katiba
imejaa imani kuwa vyeti vya shule na vyuo ndiyo elimu na hekima na kwa
kutumia sifa za vyeti vya elimu inawanyima haki wananchi wengi kushiriki
na kuwania uongozi katika ngazi mbalimbali. Ibara ya 75(f) inaeleza
sifa moja ya Rais kuwa “anayo angalau shahada ya kwanza ya chuo kikuu kinachotambuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.” Cheti
cha shahada siyo kipimo kizuri cha elimu, hekima na uwezo wa kuongoza.
Bill Gates hakumaliza masomo yake ya shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha
Harvard. Aliona anapoteza muda akaanzisha kampuni ya Microsoft. Kama
Bill Gates angekuwa Mtanzania, Rasimu ya Katiba ingemzuia kugombea Urais
kwa kuwa hana cheti cha shahada. Steve Jobs pia hakumaliza na kupata
shahada badala yake alifanya masomo aliyoyaona muhimu na kuanzisha
kampuni ya Apple. Hapa Tanzania sidhani kama Said Salim Bakhresa ana
shahada yeyote. Taarifa iliyoko Wikipedia na gazeti la Forbes inaeleza
aliacha shule akiwa na miaka 14 na akaanza biashara ya kuuza potato mix.
Kama taarifa hii ni kweli basi huenda hata darasa la 8 hakumaliza.
Lakini uwezo, uzoefu na elimu itokanayo na uzoefu wa kazi ni kubwa
kuliko hata mtu mwenye PhD ya biashara. Mzee Bakhresa hana sifa ya
kugombea Urais kwa kuwa hana shahada ya kwanza. Sina uhakika kama
Freeman Mbowe ana shahada. Ikiwa hana siyo haki kumzuia kugombea Urais
kwa sababu hiyo. Mwache agombee na wengine wajenge hoja hana maadili na
uwezo wa kuongoza nchi. John Major alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza
mwaka 1991 – 97 hana shahada ya Chuo Kikuu. Kuna watu wengi wenye
shahada nyingi lakini hawana hekima wala busara. Vyeti vingi vys siku
hizi ni vya kughushi na inawezakana kabisa usiweze kugundua kuwa
vimeghushiwa. Sifa ibakie kusoma na kuandika kiswahili. Wache wapiga
kura waamue kuwa elimu ya mgombea haitoshi kumfanya kuwa Rais. Sifa ya
elimu ya mgombea ubunge ni kidato cha nne. Rasimu itamzuia Mzee Bakhresa
hata kugombea ubunge kwa sababu hana cheti cha kidato cha nne. Kuna
Watanzania wengi waliomaliza darasa la nane au la saba la zamani wenye
elimu bora kuliko aliyemaliza kidato cha nne hivi karibuni. Kuna watu
wengi wamemaliza darasa la 7 wana uzoefu mzuri na wana uwezo wa
kuwawakilisha wananchi katika Bunge. Vigezo vya vyeti vya elimu
visitumiwe kuwanyima wananch haki zao za kisiasa. Kigezo cha shahada pia
kimeingizwa katika uteuzi wa Mawaziri. Watu wenye uzoefu na uwezo wa
uongozi lakini hawana vyeti vya shahada hawawezi kuteuliwa kuwa
mawaziri. Nastaajabu hii obsession na vyeti imetoka wapi?
- Ibara ya 31 inazungumzia Dini. “(1)
Kila mtu anao uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya imani
ya dini na anao uhuru pia wa kubadilisha dini, imani yake au kutokuwa na
imani na dini. Kifungu cha (5) Ni marufuku kwa mtu, kikundi au taasisi
ya dini kutumia uhuru wa kutangaza dini kwa kukashifu imani na dini
nyingine, kujenga chuki au kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya
kutetea imani au dini”. Tatizo ya ibara hii ni tafsiri ya
kukashifu. Imani za dini zina tofauti. Imani ya msingi ya dhehebu moja
inaweza kuwa kufuru kwa dhehebu lingine na ikatafsiriwa kuwa ni
kukashifu. Kuna masuala ambayo jamii inapaswa kujenga maelewano ya
kuvumiliana na kuheshimiana na kukubali tofauti za imani bila kugombana.
Kuliweka katika katiba inaweza kujenga chuki na ikatafsiriwa kuwa
inalenga kundi fulani. Ibara na 5 imelenga kikundi au taasisi ya dini. Je vikundi ambavyo siyo vya dini vinaruhusiwa kukashifu imani na dini?
- Serikali
ya Muungano itakuwa na Jeshi la ulinzi, Polisi na Usalama wa Taifa.
Serikali za washirika zinaruhusiwa kuwa na polisi na usalama wa taifa.
Inawezekana serikali ya Muungano ikaongozwa na Chama A, Serikali ya
Zanzibar ikaongozwa na chama B na serikali ya Tanzania Bara ikaongozwa
na chama C. Serikali zote zina polisi na usalama wa taifa wake,
haitakuwa kasheshe ndani ya nchi? Sina uhakika katiba imeweka bayana
utaratibu wa kuzuia migongano kati ya vyombo vya Muungano na vyombo vya
Washirika.
Haya ni mapendekezo ya awali tu, mapendekezo
mengine yataendelea kutolewa kwa kadri ambavyo tutazidi kuichambua
rasimu hii ya katiba. Natoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha kuwa
wanaitafuta rasimu hii bila kuchoka, kuisoma na kuielewa na kuendelea
kutoa mapendekezo yao kwa tume ya mabadiliko ya katiba iwe ndiyo lengo
kuu.
Kwa sababu tume imetangaza kuwa itachapisha rasimu katika
magazeti ya serikali kwa maana ya HABARI LEO na ZANZIBAR LEO, tunaona
kama huku ni kuififisha rasimu isiwafikie watanzania wengi zaidi.
Kuna
haja ya dhati, tume ikaitangaza rasimu katika magazeti mbalimbali ya
kila wiki na ya kila siku ili kuhakikisha kuwa rasimu imefikiwa na
imesomwa na watanzania wengi. Na nakala zitakazobakia “returns” baada ya
mauzo ya magazeti husika tume izinunue nakala hizo na izisambaze kwa
utaratibu maalum mikoani na vijijini.
Ni ushauri wetu kwa Tume
pia kwamba baada ya kazi kubwa waliyoifanya, wasikubali kuyumbishwa na
wahafidhina wasiopenda mabadiliko wanaotokana na CCM. Tume iwe na
msimamo na iangalie wananchi wanataka nini na itetee masuala ya msingi
na ya maslahi ya wananchi ambayo inaona ni muhimu yakatetewa kwa maslahi
ya taifa na hasa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi.
Na mwisho,
Tume ihakikishe kuwa masuala haya tunayoyashauri kwa awamu yanapewa
uzito na tafakuri pana ili kuipata katiba itakayokuza uchumi imara,
kuongeza ajira kwa vijana na kuinua maisha ya wananchi wa kipato cha
chini.
“Mungu Ibariki Tanzania”
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.Mwenyekiti,
09 Juni 2013, Dar Es Salaam.