Imeandikwa na Saleh Ally
MGOGORO
wa kimuziki kati ya msanii Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’ na kituo
kimoja cha redio umezidi kuchukua kasi huku makundi mawili, kila moja
likitengeneza ngome yake na kuamini linachoamini.
Kundi ambalo
linamuunga mkono Jaydee na kumuona ni mkombozi, anazungumza kwa niaba
yake na wasanii wengine, la pili ni lile linalobaki upande
unaoshambuliwa, linatetea ngome yake.
Jaydee anashutumu kubaniwa
nyimbo zake na kituo hicho ambacho kupitia mitandao kadhaa ya kijamii
ameeleza wazi kuwa wanambania, wanaziponda lakini hata watangazaji wake
wamekuwa wakionyesha chuki binafsi dhidi yake.
Jaydee pia
aliwaponda wasanii Ben Pol na Linah anayetokea THT kwamba walishindwa
kutokea kwenye uzinduzi wa video ya wimbo wake wa Joto Hasira, kwa madai
walizuiwa na bosi wao.
Ujasiri huu wa Jaydee ndiyo kitu bora
ambacho kimekuwa kikitakiwa kufanyika kutoka kwa wasanii, yaani
wapigane kutetea muziki wa Tanzania hasa kama kuna watu au kundi la watu
limejikita katika kuuangamiza.
Lakini ni tofauti kidogo, kwani
wasanii wengi wamekuwa imara na kuwa tayari kujitetea wenyewe tu na si
vingine. Nasisitiza mara nyingi, wao ndiyo wahusika wa kwanza na
wanapaswa kuanzisha mapinduzi kuanzia kwao, mfano kusema naonewa si kitu
kibaya lakini je, umewahi kupigania wanaoonewa?
Kujitetea pekee
unaweza kufanya, lakini vipi utafanikiwa kama asilimia kubwa ya kundi la
wanamuziki linaendelea kuonewa. Ukibaki hauonewi pekee na asilimia
kubwa ya wasanii au wanamuziki inaonewa, kunaweza kuwa na
mapinduzi sahihi?
Ndiyo
maana nashangazwa kusikia Jaydee leo anaona ubovu wa kituo hicho,
anathubutu kusema hadharani akionyesha wazi ameumia. Lakini miaka 10 au
zaidi iliyopita, Jaydee alikuwa kimya na hakuwaza kusema kwamba kituo
hicho kinawabania wasanii wengine na ‘kumtukuza’ yeye hata kama muziki
wake haukuwa wa kiwango kilichokuwa kinazungumzwa.
Siwezi kusema
muziki wa Jaydee ni mbaya, nimekuwa kati ya mashabiki wake. Lakini
yoyote atanichekesha akisema nyimbo albamu zake zote alizotoa zilikuwa
katika kiwango cha juu sana na ndiyo maana leo ni maarufu.
Hakuna
asiyejua kwamba miaka nenda rudi, wasanii wamekuwa wanaongoza kwa
unafiki, kutopendana wenyewe, kugeukana na hata kujenga makundi lukuki,
ndiyo maana kila kukicha wamekuwa wakishambuliwa maana katika maisha yao
hawana umoja.
Jaydee alianza kuwa mtangazaji katika kituo hicho
baada ya kuacha kurap, akaamua kuachana na kurap na mwisho kuwa msanii
wa nyimbo za kubembeleza, mara ya kwanza akianza kutikisa na albamu ya
Machozi, Solo Thang anaweza kuhadithia vizuri kuhusu hili.
Kuanzia
albamu ya Machozi, kituo hicho ndicho kilisimama kuhakikisha anakuwa
bora hata kama muziki wake haukuwa ukimzidi kila mwanadada wakati huo.
Angalia,
kulikuwa wasanii kama Stara Thomas, Carola Kinasha ambao kiuwezo
walikuwa juu kuliko Jaydee, lakini hawakupewa nafasi ya kutosha, badala
yake Jaydee ambaye hakuthubutu kuwatetea hata kidogo akaendelea
‘kubebwa’ na watu wakaamini ni bora kuliko yeyote kwa upande wa akina
dada au kina mama katika kuimba, haikuwa hivyo.
Angalia albamu ya
Binti, karibu nyimbo zote zilikuwa na ujumbe mmoja, ulikuwa
ukimshambulia mwanaume mmoja ambaye alikuwa amemuumiza Jaydee. Takribani
ujumbe wa nyimbo karibu zote ulikuwa ni mmoja, lakini ilibebwa na
kuonekana ni moja ya albamu bora kabisa kuwahi kuwepo katika muziki wa
Tanzania, kitu ambacho hakikuwa sahihi.
Wakati huo wasanii lukuki
walilia kubaniwa, mmoja wao alikuwa ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye
ndiye alimtambulisha mwanadada huyo alipomshirikisha katika wimbo wa
Mambo ya Fedha, kabla ya hapo hakuwa na jina. Jaydee hakuwahi kuungana
naye hata kidogo hata kwa mstari mmoja wa kumtetea au kuunga mkono
kutetea muziki wa Tanzania, kuonyesha anapinga mwenendo wa
wanaolazimisha kuwabagua wasanii au kufanya mambo kwa mabavu kwa kuwa
wameshika mpini.
Hakuna aliyesikia kilio cha Sugu, wasanii
wanaochipukia bila ya kujua wasemacho, kisa nyimbo zao zinapigwa
redioni, ili kuonyesha shukrani za dhati wakaanza kutangaza Sugu
anatapatapa na amekwisha kimuziki!
Ajabu, asilimia kubwa ya
maneno yake ndiyo yanayozungumzwa leo, ndiyo yanatumiwa na kila msanii
anayebanwa au kuhisi kaonewa. Angalia, hata Jaydee naye ameingia huko!
Swali langu hapa je, Jaydee na wengine wanaolalamika, wamekwisha
kisanii?
Ndiyo maana nasema, tasnia ya muziki hasa muziki wa
kizazi kipya umejaza watu wavivu kufikiri, wenye mioyo ya ‘Kichina’,
wasio na uwezo wa kuthubutu hata kidogo ambao wanasubiri wayumbe au
kuumizwa wao ili wamtafute wa kumuangushia lawama.
Jiulize, kama
Jaydee alibebwa kwa miaka 10, halafu leo analalamika atakuwa sahihi?
Sitaki kumpinga kwa kuwa kuna kitu anakiona lakini ninaamini alikiona
tokea mapema, akauchuna.
Bado nasisitiza, yeye na wengine wote
wanaolia baada ya kuguswa wao nawaita wanafiki, wanapigana kwa ajili yao
na si kwa muziki wanaoutumikia. Iwapo wangekuwa tayari kupambana kwa
ajili ya muziki huo, msanii kama Jaydee asingeanza vita leo.
NARUDI KWA JAYDEE
Sijawahi
kuingia naye katika malumbano zaidi ya miaka 10 tokea alipokuwa
mwanahabari mwenzangu na sasa msanii. Lakini nathubutu kumueleza kuwa ni
kati ya wasanii wasiojali muziki wa Tanzania na wanajiangalia wao
zaidi.
Picha ya unafiki na kujiangalia mwenyewe inaonekana sasa
ingawa takribani miaka mitano iliyopita nilianza kuinusa. Leo analia,
anabaniwa na anauona moto unaounguza muziki wa Tanzania ulivyo mkali.
Naamini
aliuona miaka kibao nyuma, lakini kwa kuwa alikuwa akitetewa hakuweza
kuangalia kwamba rafiki zake, wasanii waliombeba kabla walikuwa
wakiungua. Akaendelea kuwapita kwa raha zake mustarehe.
Tungeweza
kumuita Jaydee ni mpambanaji kama angewakosoa hao anawakosoa sasa
katika kipindi walichokuwa wamempa mbeleko yeye, basi kweli ingeonekana
anapigania muziki wa Tanzania. Sasa anapigania chake tu!
Jaydee
amefika mbali kimuziki, alikuwa bora jukwaani na nyimbo kadhaa na nyingi
zikapewa ‘over promotion’ lakini bado ninaweza kumuita mkongwe. Ajabu
alibaki chipukizi hadi leo katika suala la kutetea haki za wasanii na
muziki wenyewe.
Sitaki kumkatisha tamaa kwa mapambano
aliyoyaanza, ninaamini ana nafasi ya kuanza kuusaidia muziki ambao
umemsaidia. Lakini ndiyo kipindi ambacho anaweza kupata machungu
waliyopata wasanii wenzake kunyeshewa mvua na kuunguzwa na jua wakati
akiwa kivulini kwa ‘msaada’.
Anachokifanya leo Jaydee ni nyongeza
tu ya walichokifanya Sugu au Afande Sele au wasanii wachache walioamua
kuwa wakweli au wale walioamua kuwa wabunifu kama Ambwene Yessaya ‘AY’,
aliyekimbia vita ya redio na kuingia katika kurekodi video bora
zilizoendelea kumng’arisha.
Simzuii, Jaydee kuendelea kupambana, lakini namuasa anachokifanya kama ni kwa ajili ya muziki akipozwa tena, asirudi nyuma.
Ninachomkumbusha,
hata yeye amekuwa kundi moja na analowalaumu ambao angeweza kuwashauri
mapema ‘ndani ya mjengo’ kama angekuwa na nia nzuri na muziki wa kizazi
kipya. Msisitizo ‘Joto Hasira’ liwe la kweli.