![]() |
| Baadhi ya wagombea wa urais Kenya |
Monday, March 4, 2013
UTATA WA KIFO CHA BENSON MOLLEL
| Benson Mollel wa kwanza kushoto akiwa katika moja ya shughuli za UVCCM mkoani Arusha |
MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) taifa, kupitia Mkoa wa Arusha, Benson Mollel (26) amekutwa
amefariki dunia ndani ya Hoteli ya Lush Garden Business, iliyopo Mtaa
wa Jacaranda katikati ya Jiji la Arusha.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema Mollel alikutwa
akiwa amekufa jana mchana na kwamba tukio hilo limezua hofu kwa wakazi
wa Jiji la Arusha, huku wakijiuliza chanzo cha kifo chake.
Kifo cha mwanasiasa huyo mchanga ambaye pia
alikuwa ni mfanyabiashara wa madini mkoani hapa, kimezusha maswali mengi
wakati wengine wakihusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa na upande
mwingine wakidai ni masuala la kibiashara.
Hisia hizo zinatokana na ukweli kwamba Arusha ni
jiji lenye hekaheka za kisiasa hasa ndani ya CCM ambapo Mollel alikuwa
mmoja wa vinara wake.
Polisi waliwasili hotelini hapo saa 8.00 mchana na
kuupakia mwili wa marehemu kwenye gari na kisha kuupeleka Hospitali ya
Mount Meru kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya wa Arusha (OCD), Gilles
Muruta akizungumza katika eneo la tukio alisema: “Tunachunguza tukio
hili ambalo ni la ghafla.”
Akizungumzia kifo hicho, Katibu Mkuu wa UVCCM,
Martin Shigela alisema: "Tumepokea kwa masikitiko kifo cha Mollel
japokuwa sifahamu nini hasa kimejiri huko."
"Kuna rafiki yake alinipigia simu kuniarifu kuhusu
kifo hicho na nikawaambia kama UVCCM Taifa tupate maelezo kamili na
tujue nini cha kufanya. Iwapo familia itakuwa na mipango yoyote
watutaarifu," alisema Shigela.
Baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wa madini
mkoani Arusha walionekana nje ya hoteli hiyo baada ya taarifa za kifo
hicho kusambaa na wengine walishindwa kujizuia kisha kuangua vilio.
Miongoni mwao ni kada wa Chadema, James ole Millya
na diwani wa CCM Kata ya Mlangarini, Mathias Manga. Katibu Mwenezi wa
CCM wa Mkoa wa Arusha, Isaack Kadogoo ambaye pia alifika eneo hilo
alisema kwamba wamepokea taarifa za tukio hilo kwa mshtuko mkubwa.
Uongozi wa hoteli hiyo haukuwa tayari kulizungumzia kwa madai kwamba limefikishwa katika vyombo vya usalama.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani
ya hoteli hiyo vilidai marehemu aliwasili usiku, juzi Jumamosi hotelini
hapo akiongozana na mwanamke aliyetambulika kwa jina la Nancy na
kuchukua chumba namba 208.
SOURSE: MWANANCHI
Sunday, March 3, 2013
MBATIA, ULUOCH WAKATAA KUSHIRIKI KWENYE TUME YA KUCHUNGUZA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE
![]() |
| Mh Mbatia |
WAKATI Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiweka hadharani majina ya wajumbe wa Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo ya mwaka 2012 ya Kidato cha Nne jana, baadhi ya wajumbe waliopewa heshima hiyo ya kusaidia kutafuta sababu za matatizo ya elimu na jinsi ya kuyatatua, Mbunge wa Kuteuliwa James Mbatia na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch, wamekataa uteuzi huo. Mbatia katika hoja yake kwa waandishi wa habari jana, alisema kwa kuwa hadi jana hakuwa amepata taarifa ya maandishi kuhusu uteuzi wake, asingeweza kutamka kama amekubali au la, hadi atakapokuwa amepata maandishi hayo akisema atakapoyapata ndipo, “nitafanya uamuzi kwa maslahi ya pamoja ya Watanzania.” Hata hivyo, habari za uhakika kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, zilisema Mbatia alifahamishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo kwa njia ya simu afike Ofisi ya Waziri Mkuu achukue barua yake ya uteuzi kama walivyofanya wajumbe wengine. Oluoch alipotafutwa azungumzie uamuzi wake wa kujitoa kwa mujibu wa barua aliyoiwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema yuko mkutanoni akaomba apigiwe baada ya nusu saa na ilivyofanyika hivyo, alikata simu kila alipopigiwa. Ikiwa nia yetu ni thabiti ya na kweli ya kutaka kubadili mwenendo wa mambo yasiyo sahihi katika nchi ya Tanzania, hatuna budi kutii na kufuata sheria tulizojiwekea sisi wenyewe. Kama siyo kasuku, kila leo tunaimbiana misemo maarufu tunayonukuu kutoka kwa watu mahiri, mfano, “insanity: doing the same thing over and over again and expecting different results. ~Albert Einsten” na “walk the walk, talk the talk” (ingawaje hii tumeibadili tunavyojua kwa akili yetu ati, ‘walk the talk’ -- hakuna msemo kama huo! How do you walk the talk? Kupinda tu misemo ya wenyewe). Sasa ikiwa Waziri Mkuu aliripotiwa na Ofisi yake kuwa alikutana na Wajumbe wa Tume aliyoiteua, bila ya kupata hakika ya kila mteuliwa --iwe ni kwa njia ya kumpigia simu kuthibitisha, kutuma ujumbe mfupi wa simu, kutuma barua, nukushi, barua pepe n.k-- kuwa (1) Amepata taarifa rasmi ya uteuzi huo na (2) Ameridhia uteuzi huo; Waziri Mkuu akaitisha kikao ijapokuwa baadhi ya wajumbe hawakuwemo kikaoni bila ya kuwa na hakika kama wanaopelea wametoa taarifa rasmi ya udhuru wa kutokuhudhuria kikao hicho, sioni ni kwa namna gani Mbatia analaumiwa kususia Tume il hali anaifuata sheria. Kuongoza ni mfano na Kiongozi ni mfano. Kwa wasiojali sheria au wanaojiona wapo juu ya sheria ama wenye adabu za woga, hili litakuwa jambo la kipuuzi kwao. Kwao wao amri ya mkubwa inatiiwa bila kuhojiwa hata kama imekiuka sheria, hata kama nchi ni ya utawala wa kiraia na haiendeshwi kijeshi. Kwao kuvunja sheria mama si jambo la ajabu. Ndiyo wale kila leo wanaimba misemo kama kasuku bila kutafsiri wala kujua maana yake. Na hao hawakawii kusema kwa kuwa huyu ni mmoja wa wanachama wa upinzani, basi lolote lile hata liwe jema atapata pa kupinga tu. Na utawasikia majuha hao wakijitapa kwa bezo la kejeli, “sheria Bongo?” Utakuwa na kasoro ukithubutu kusema Mbatia hana nia ya kusaidia nchi kuondokana na tatizo kwa kuhoji utaratibu uliotumika kumfikishia taarifa. Angekuwa hana nia angetumia miaka inayokaribia kumi kutafiti kuhusu elimu na kisha kukusanya vielelezo na kuwasilisha hoja Bungeni kuhusu uozo wa elimu? Kama anaweza kuunda hoja yenye nguvu hivyo kwa maslahi binafsi, je atakapounda hoja inayolihusu Taifa?
SOURCE: WAVUTI
YALIYOJIRI KWENYE KILIMANJARO MARATHON LEO: WAKENYA WAENDELEA KUTAMBA
![]() |
| Washiriki wa Kilimanjaro Marathon wakiwa tayari kabisa kwa ajili ya kukimbia |
![]() |
| Vituko hafikukosekana wazungu hawa wao hawakukimbia marathon ila wametembea mpaka wamemaliza |
![]() |
| Dr Fransis akifurahia medali na |Carl baada ya kumaliza kilomita 21 |
![]() |
| Dr Sudai (kulia) akiwa na Dr Joseph (katikati) wakifurahia medali zao |
![]() |
| Principal Investigator wa MEPI Tanzania kutokea marekani akifurahia medali yake baada ya kumaliza kilomita 21 na Carl Jacob |
![]() |
| Motta, Carl na Kimario baada ya kumaliza mbio. \Wanafunzi wengi wa KCMUCo wameshiriki kwenye mashindano haya na kufanya vyema. Japo ushindi umeenda kwa wakenya |
![]() |
| Kocha wa Taifa Stars Kim Poulsen akiwa na Dr Josephine |
Saturday, March 2, 2013
SIMBA WAPOKELEWA VIZURI NA LIBOLO
| Kipa wa Simba, Abel Dhaira na mlinzi, Said Nassor Chollo mara baada ya kuwasili Uwanja wa Calulo ambao uko kilomita 300 kutoka Luanda. Ndege inayoonekana pichani ni ya tajiri wa Libolo, Lui Compos ambayo Simba ilitumia kutoka mji mkuu wa Angola, Luanda. Picha na Edo Kumwembe, Angola |
Hata hivyo, Simba wamefikia katika hoteli ya tajiri wa Libolo huku wakipandishwa katika ndege mbili ambazo pia zinamilikiwa na kipoba huyo.
Wekundu hao wa Msimbazi wanacheza na Recreativo Libolo ya hapa kesho Jumapili katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba ilifungwa bao 1-0 kwenye mchezo wa awali jijini Dar es Salaam.
Simba ilitua Luanda jana Ijumaa saa 5.30 asubuhi za Tanzania na kupakiwa kwenye ndege mbili kwenda mjini Calulo ambako ni umbali wa dakika 30 kutoka Luanda. Ndege ilizopanda Simba zinamilikiwa na tajiri wa Libolo, Rui Campos.
Baada ya kutua Simba walipokewa vizuri na wenyeji wao lakini walilazimika kuhaha kwa dakika kadhaa kutafuta vifaa vyao ambavyo ni bips (vizibao vinavyovaliwa juu ya jezi za mazoezi), koni na mipira ambayo wahumudu wa ndege ya Kenya Airways hawakuwa na jibu zaidi ya kuahidi kuvitafuta zaidi na huenda leo Jumamosi Simba wakavipata.
Mbali na vifaa hivyo hata begi la beki Amir Maftah halikupatikana. Simba iliwasili Calulo saa sita mchana na kufikia hoteli ya Ritz inayomilikiwa na wapinzani wao ambao waliwaazima vifaa kwa ajili ya mazoezi na hali ya hewa na hapa ni joto kali sawa na Dar es es Salaam.
Kiraka Haruna Moshi hayupo na Simba Angola baada ya kupimwa jijini Dar es Salaam na kubainika kwa ana malaria 19 huku kocha wa viungo Moses Basena akibaki kumuuguza mkewe.
Kwenye Uwanja wa ndege wa Calulo, Simba ilipokelewa na wanajeshi na kusindikiwa hadi hotelini ambapo mazingira ya mjini hapa hayajaendelea sana kama ilivyo Luanda na hata uwanja itakapochezwa mechi wa Manispaa ya Calulo Estadio Municipal de Calulo unabeba mashabiki 10,000 tu.
Kocha wa Simba, Patrick Lieweg alisema kikosi chake kipo katika hali nzuri na wako safi kisaikolojia tayari kwa ushindi na kusonga mbele kwenye mashindano hayo.
Nitalazimika kumuanzisha Seseme kwavile Haruna Moshi hayupo lakini kimsingi timu imekuja hapa kushinda na nimewasisitiza wachezaji hilo na wakanielewa, tutapambana mpaka dakika ya mwisho,alisema Mfaransa huyo mwenye miaka 60 ambaye hii itakuwa mechi yake ya 54 kuiongoza klabu kwenye michuano ya kimataifa ya CAF.
SOURCE: MWANASPOTI
FIFA YAWASILISHA MAREKEBISHO 10 YA KATIBA KWA WARAKA
Rais wa FIFA Sepp Blatter akiwa
na Rais wa TFF Leodegar Chilla Tenga walipokutana hivi karibuni makao
makuu ya FIFA jijini ZurichShirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limetuma mapendekezo 10 ya
marekebisho ya Katiba yake kwa wanachama wake kwa njia ya waraka.Mapendekezo
hayo yametumwa kwa kila nchi mwanachama kupitia waraka namba 1320,
ambapo wanachama kwa kupitia kwa mashirikisho yao ya mabara watapiga
kura ya ndiyo au hapa.
Kwa upande wa Afrika, wanachama wa FIFA
wanatakiwa kuwasilisha kura zao kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF).Baadhi ya mapendekezo
hayo ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa
FIFA (FIFA Congress). Makamu wa Rais wa FIFA na wajumbe wa Kamati ya
Utendaji wanaochaguliwa katika mabara ambapo itabidi wathibitishwe na
FIFA Congress.
Muundo wa Kamati ya
Utendaji; nafasi moja ya vyama vya mpira wa miguu vya Uingereza (British
FAs) sasa inahamishiwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA). Pia
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya FIFA anatakiwa kushiriki vikao vya
Kamati ya Utendaji bila kuwa na haki ya kupiga kura.Uchaguzi
wa Rais; mgombea anatakiwa kuungwa mkono na idadi ya kutosha ya vyama
wanachama kutoka katika mabara mawili tofauti. Ukomo wa uongozi;
kuanzisha vipindi vya uongozi. Ukomo wa umri; ukomo wa umri usiozidi
miaka 72 wakati wa kugombea utekelezwe.Uwakilishi
wa kutosha kwa makundi yenye maslahi katika FIFA; makundi yenye maslahi
katika mpira wa miguu kama wachezaji wapate uwakilishi katika Kamati ya
Mpira wa Miguu. Uteuzi wa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia; uteuzi
sasa ufanywe na Mkutano Mkuu wa TFF.
SOURECE: www.issamichuzi.blogspot.com
Friday, March 1, 2013
POLISI MKOA WA KINONDONI YAKAMATA MAJAMBAZI NA SILAHA
Baadhi ya silaha zilizokamatwa klatika msako na Polisi Mkoa wa Kinondoni zikiwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay leo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela akionesha bastola zilizokamatwa na Polisi wakati wa msako wa majambazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela akionesha nondo zilizokamatwa wakati wa msako huo.MNYIKA: NCHI IMEINGIA TENA KWENYE MGAO WA UMEME

Mbunge wa jimbo la Ubungo-Chadema Mh John Mnyika-
---
Nchi
imeingia tena katika mgawo wa umeme kinyume na ahadi iliyotolewa na
Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo bungeni tarehe 28
Julai 2012.
Hali hiyo
ni matokeo ya Serikali kutozingatia tahadhari niliyoitoa bungeni tarehe
27 Julai 2012 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kwa nyakati
mbalimbali kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini juu ya
hali tete iliyotarajiwa kuwepo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika
utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme.
Ikiwa ni
sehemu ya wajibu wa kibunge wa kuisimamia Serikali nawataka viongozi na
watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Nchini
(TANESCO) kuacha kuficha hali ya mambo na kuwaeleza ukweli wananchi
kuhusu mgawo wa umeme uliojitokeza na hatua za haraka zinazochukuliwa
kurekebisha hali hiyo.
Iwapo
Wizara na TANESCO hawatatoa matangazo ya ukweli kwa wananchi, kwa nafasi
yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nitaeleza vyanzo vya mgawo
wa umeme uliojitokeza ili hatua ziweze kuchukuliwa wakati huu ambapo
wajumbe wa kamati ya nishati na madini wenye wajibu wa kuisimamia
Serikali kwa niaba ya Bunge katika sekta hizo nyeti hawajateuliwa.
Aidha,
pamoja na kutoa maelezo kuhusu mgawo wa umeme, Wizara ya Nishati na
Madini na TANESCO watumie nafasi hiyo pia kueleza hatua zilizochukuliwa
kuhusu ukaguzi wa awamu ya pili kuhusu tuhuma za ufisadi katika ununuzi
wa vifaa na uzalishaji wa umeme wa dharura ikiwemo kuhusu mafuta mazito
ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
Ikumbukwe
kwamba mwanzoni mwezi Agosti 2012 Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (NAOT) iliunda timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalum wa
hesabu za Shirika la Umeme (TANESCO) kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa
fedha za umma zilitajwa bungeni na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani tarehe 27 Julai 2012 na Waziri
wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya hoja ya Serikali tarehe 28
Julai 2012.
Wizara ya
Nishati na Madini na TANESCO waeleze pia hatua iliyofikiwa kuhusu
uchunguzi mwingine uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma
(PPRA) kuanzia mwezi Agosti 2012 wa mchakato wa ununuzi wa mafuta mazito
ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme wa dharura kutokana na tuhuma
mbalimbali zilizotolewa bungeni kuhusu ununuzi huo suala ambalo Kambi
Rasmi ya Upinzani ilitaka pia tarehe 27 Julai 2012 liundiwe kamati teule
ya Bunge ili uchunguzi wa kina uweze kufanyika.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
27 Februari 2013
CHANZO CHA HABARI HII: www.dj-sek.blogspot.com
Subscribe to:
Posts (Atom)












