Facebook Comments Box

Wednesday, February 20, 2013

ANGALIA VIBONZO HIVI VINAVYOHUSU MATOKEO YA KIDATO CHA NNE

Uzuri wa wachora vibonzo ni utumiaji wao wa mchoro kuwakilisha maada ambayo kwa mtu mwingine angehitaji kurasa nyingi za karatasi ili kueleweka. Angalia vibonzo hivi viwili ambavyo vinatosha kabisa kukupa taswira ya elimu hapa Tanzania




Tuesday, February 19, 2013

MWENYEKITI WA KIJIJI ALIEUZA MLIMA ATIMULIWA MADARAKANI NA WANANCHI

WANANCHI wa Kijiji cha Zuzu Kata hiyo mkoani Dodoma, Wameiangusha Serikali ya Kijiji hicho iliyokuwa ikiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti Peter Mtawale (49) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye ameamua kuiacha Ofisi yake kwa kosa la kuuza Mlima wa Widete.

Mtawale aliyezaliwa 1963 alikubali kujiuzulu kwa kuutangazia Mkutano wa Hadhara karibuni mwaka huu baada ya kubanwa na tuhuma nyingi ikiwemo ya kuuza Mlima huo kwa Mwekezaji ambaye alikiri Serikali yake ilimruhusu uchimbaji wa Rupia bila kuwaarifu wananchi.

Mbali ya Tuhuma za kuuza Mlima bila kuwataarifu wananchi na Uongozi wa Kata, nyingine ni pamoja na mauzo ya Changarawe (Kifusi), Maji, Mchanga,  Ufujaji  wa Fedha ya Malambo Mbgani, Ushuru wa Magari, kuingia kwa wageni bila taarifa, Kutoitishwa kwa Vikao na kusoma Mapato na Mtumizi, Milio ya Milipuko, na Viongozi kufunga Maji bila Mita.

“Kuna Uchochezi ninaofanyiwa na Diwani wa Kata Awadhi Abdalah (CCM), Mwenyekiti wa Changu (CCM) Omari Kagusi na Katibu Mwenezi Solo (CCM) ambapo 14.1.2012 walifanya kikao cha Siri kunijadili bila kunitaarifu,”alisema Mtawale alipohojiwa na kuonekana anafanya kazi zake kwa kuongozwa na Kigogo mmoja wa Kata anayempotosha.

Alipoulizwa kwa nini Serikali yake haikuwaarifu wananchi juu ya kuuzwa kwa Mlima huo hadi wakapatana Mwekezaji akipata anachochimba Mwekezaji atachukua asilimia 60% na Kijiji asilimia 40% alisema, kwa kuwa vikao vinakaa mara tatu kwa mwaka ilikuwa wawaarifu Machi, 2013.

Pamoja na kukiri kuingia mkataba huo mwezi Desemba 2012 alikubali walifanya makosa ya kutowaarifu wananchi na Uonozi wa Kata, lakini akasema Katibu Tarafa Joyce Malare ametumwa kutatua mgogoro huo lakini walishindwa kukaa hadi 21.1.2013 kutokana na koramu (akidi) kutokutimia.

Diwani Abdalah alipoulizwa alikiri kuwepo kwa Mgogoro huo na kusema yeye ametoa Taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ambaye amesema analifanyia Kazi, lakini alishangaa Katibu Tarafa kuanza kumuingilia akifanya Kazi za Kisiasa ili kumgonganisha na Wananchi Jambo alilosema hawezi kuvumilia na kukubali wananchi wadhulumiwe haki yao.

Aidha Katibu Tarafa Malare alipoulizwa na mwandishi amefikia wapi katika utatuzi wa mgogoro huo, hakuonesha ushirikiano na kuanza kumponda Mwandishi, “…nani kakwambia umbeya huo? ...Kwa utaratibu nikifanya kazi nampelekea mkubwa wagu siyo wewe!!”

Alimwagika maneno yasiyo na staha bila kujua Mwandishi alimhoji Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Lephy Benjamini juu ya mgogoro na kujibiwa anaushughulikia Malare.



HUYU NDIO AFISA MTENDAJI MKUU MPYA WA TTCL


 Picture
Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL imemteua Dkt. Kamugisha Kazaura kuwa Ofisa mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo.

Dkt. Kazaura amechukua nafasi ya aliyekuwa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Said Amir Said ambaye amestaafu hivi karibuni kwa mujibu wa sheria. Kabla ya uteuzi huo Dkt. Kazaura alikuwa ni Afisa mkuu wa ufundi (CTO)wa TTCL.

Bodi ya wakurugenzi ya TTCL imewaomba wafanyakazi na menejimenti kumpa afisa Mtendaji mkuu mpya ushirikiano wa kutosha ili kuwa na mshikamamo wa pamoja ili kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi.

Kwa kusisitiza Bodi imesema, “Tufanye kazi na tusonge mbele pamoja, kama timu ililyoshikamana pamoja na iliyodhamiria kuinua utawala bora.”

Dkt. Kamugisha Kazaura alitunukiwa shahada ya Uzamili (Masters) na Uzamivu (PhD)katika fani ya Habari na mawasiliano ya simu katika chuo kikuu cha Waseda kilichopo Tokyo, Japan.


KIPANYA: BUNGE LISIPORUSHWA LIVE



OLD BAGAMOYO ROAD KUITWA MWAI KIBAKI ROAD KUANZIA KESHO

Hapa ni Msasani Kwa Warioba katika barabara ya Old Bagamoyo Road ambayo kuanzia kesho itaitwa Barabara ya Mwai Kibaki Road kwa heshima aliyotunukiwa kiongozi huyo wa Kenya na Hlmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kufuatia ziara yake ya kitaifa ya siku mbili itayoanza kesho jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Saidi Meck Sadik, barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 10.1 ni kuaniza kwenye mataa ya Moroccco karibu na makao makuu ya Airtel hadi mzunguko wa kuelekea Africana kule Mbezi Beach, mkabara na uwanja wa kulenga shabaha wa JWTZ.

Akiongea usiku huu, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Rais Kibaki anatarajiwa kuwasili kesho saa 9 alasiri na kupkewa na mwenyeji wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambapo usiku atamwandalia dhifa ya kitaifa Ikulu.  Keshokutwa. Alhamisi, Rais Kibaki ataongea na wazee wa Dar es salaam katika ukumbi wa PTA ulioko viwanja vya SabaSaba barabara ya Kilwa Road. Pia atatembelea sehemu mbalimbali atazopangiwa katika ziara yake hiyo ambayo pia ataitumia kuwaaga Watanzania kwani muhula wake wa uongozi utafikia kikomo baadaye mwaka huu.


HII NDIO HISTORIA YA CLOUDS ILIPOTOKEA NA ILIPO SASA




JERRY MURO KUENDELEA KUWA HURU

UPANDE wa Mashitaka katika rufaa ya kupinga kuachiwa huru kwa Aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji (TBC) Jerry Murro aliyekuwa anakabiliwa na mashitaka ya kuomba rushwa ya Sh milioni 10 umeiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam kuamuru kesi hiyo isikilizwe upya.


Mawakili wa wa Serikali walidai hayo jana mbele ya Jaji Fauz Twaib kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikosea kisheria katika kuweka kumbukumbu ya Mwenendo wa
kesi hiyo jambo lililosababisha kutoa uamuzi usio wa haki.

Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi alikata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa Novemba 30 mwaka juzi na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Frank Moshi, ambayo ilimuachilia huru Murro, Deogratius Mgasa na Edmund Kapama waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka hayo.

Katika rufaa hiyo, Wakili wa Serikali Awamu Mbagwa alidai kuwa mahakama haikuandika vizuri kumbukumbu za ushahidi na vielelezo  katika Mwenendo wa kesi ambapo kuna baadhi ya
ushahidi haueleweki unamaanisha nini jambo lililosababisha Hakimu kufikia uamuzi usio wa haki.

Aidha alidai kuwa kuna baadhi ya vielelezo na ushahidi haupo kwenye mwenendo wa kesi,  ikiwemo maelezo ya onyo yaliyotolewa na Murro katika kituo cha polisi na kitabu cha wageni waliofika katika hoteli ya Sea Cliff ambayo wajibu rufaa wanadaiwa kuomba rushwa.

Aliieleza mahakama kuwa, kitabu cha wageni kilikataliwa kupokelewa mahakamani kama kielelezo lakini katika Mwenendo wa kesi haijaandikwa na hata uamuzi wa pingamizi la kielelezo hicho haukutolewa na kudai kuwa kukosekana kwa uamuzi huo kumesababisha Hakimu kutofikia uamuzi wa haki.

Aidha katika mwenendo wa kesi hakuna kumbukumbu za wao kuwasilisha Mkanda wa kamera inayonasa matukio (CCTV) ulioonesha wajibu rufaa walipokwenda kufanya
makubaliano ya kupokea rushwa, lakini walishindwa kuuangalia na  baadaye wakaamua kutumia picha za kawaida.

Aliongeza kuwa kesi hiyo awali ilikuwa inasilizwa na Hakimu Gabriel Mirunde lakini Hakimu Frank Moshi ndiye aliyetoa hukumu hivyo kutokana na kuandikwa vibaya kwa mwenendo wa kesi hiyo Hakimu Moshi alishindwa kuelewa ushahidi na utoa uamuzi usio wa haki.

Akijibu hoja wakili wa Murro, Richard Rweyongeza aliiomba mahakama kutupilia mbali hoja hiyo kwa uwa haina  misingi kisheria pia wakata rufaa hawajaeleza ni vipi kukosewa kwa mwenendo wa kesi hiyo kumesababisha kufikia uamuzi usi sahihi.

Naye Wakili wa wajibu rufaa wengine, Majura Magafu alidai kuwa wakata rufaa hawajalalamika kuhusu hukumu iliyotolewa bali maandishi katika mwenendo wa kesi  na katika hukumu hiyo hakuna sehemu ambayo Hakimu alilalamika kuwa alipata shida kusoma mwenendo wa kesi hiyo.

Alidai endapo mahakama itamua kesi hiyo isikilizwe upya itakuwa ni sawa na kufanyabiashara ya kuchagua mahakimu kuwa kama wameshindwa kwa hakimu huyo wajaribu kwa mwingine jambo ambalo haliruhusiwi kisheria.

Warufani walikuwa na sababu nne lakini imesikilizwa sababu moja ambapo baada ya kusikiliza hoja hizo Jaji Twaib aliahirisha shauri hilo hadi Aprili 29 mwaka huu atakapotoa uamuzi.

Washitakiwa wanadaiwa kuwa waliomba rushwa kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage kwa lengo la kuzuia kutangazwa kwenye
televisheni habari za tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma akiwa mhasibu wa halmashauri hiyo.

Katika madai hayo, Muro na wenzake wanadaiwa Januari 28 mwaka jana jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa hilo na Januari 29 mwaka jana katika Hoteli ya
Sea Cliff Dar es Salaam waliomba rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa Wage.


Monday, February 18, 2013

INGIA HAPA KUPATA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012




Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa (MB) leo ametangaza rasmi matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne, maarifa na QT.

Jumla ya watahiniwa waliofaulu kwa Mujibu wa Matokeo hayo ni  23520 kuanzia dara la I hadi la IV  huku katika mchakato huo wasichana waliofaulu katika mchakato huo ni 7178 na wavulana ni 16342.Aidha Waziri Kawambwa amesema kuwa waliofaulu kwa daraja la kwanza ni 1641, daraja la pili ni 6495 na daraja la tatu ni 15426 na walio feli ni 24903.

Shule bora ni pamoja na St. Francis Girl ya Mbeya, Marian Boys ya Bagamoyo, Feza Boys DSM, Marian Girls Bagamoyo, na Simini ndizo zipo tano bora huku shule nyingine ni Kanosa, Jude, St. Mary.

 Ingia hapa kupata hayo matokeo

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012

MPASUKO WAIKUMBA UVCCM

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Sadifa Juma Khamis

 Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), limeingia katika mpasuko mkubwa baada ya baadhi ya wajumbe kukusudia kutoa hoja ya  kumwondoa Mwenyekiti wa umoja huo, Sadifa Juma Khamis, kwa madai ya kukiuka  kanuni na hotuba  ya ufunguzi wa kikao cha baraza hilo iliyoonyesha kuwadhalilisha.
 
Chanzo kutoka ndani ya kikao hicho kilichotarajiwa kumalizika jana katika ukumbi wa White House, mjini Dodoma, kilisema hali ya kutokuelewana ilitokea mara baada ya Sadifa kutoa hotuba hiyo juzi mchana.
 
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kulikuwa na hali ya kutoelewana ndani ya kikao hicho huku wasemaji wa umoja huo wakikatizwa mara kwa mara na kelele za kuzomeana.
 
“Baadhi ya vijana walikaa katika makundi na kuazimia kumuondoa mwenyekiti kwa kitendo chake cha kuwadhalilisha tena mbele ya waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa kikao hicho,” kilisema chanzo hicho. 
 
Pia vijana hao walikasirishwa na kitendo cha Mwenyekiti wa Taifa  Sadifa kumtimua mmoja wa waliokuwa wagombea wa nafasi ya umakamu mwenyekiti, Paul Makonda,  kwa madai kuwa alikaririwa na vyombo vya habari  mara baada ya uteuzi huo akitaka kupewa nafasi ya kufikiriwa. 
 
Aidha, wajumbe wa Baraza hilo walikerwa na kitendo cha Sadifa kumwachisha kazi mmoja wa watumishi wa umoja huo kutokea Visiwani Zanzibar aliyejulikana kwa jina moja la Jamal. 
Mvutano huo uliodumu kwa zaidi ya saa mbili na kutawaliwa na vikao vya siri, ulifanya kuchelewa kuanza kwa kikao hicho kwani badala ya kuanza saa 5:00 asubuhi kilianza saa 7:00 mchana.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mjumbe kutoka mkoani Mbeya, David Mwakiposya, alisema hotuba aliyotoa mwenyekiti wao ni mbovu na haifai. 
 
“Kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Vijana wa CCM ya mwaka 2008, Baraza Kuu ndilo linathibitisha uteuzi wa wajumbe wa Baraza, lakini cha kusikitisha aliwafukuza wajumbe wawili ambao  wakati wa mkutano mkuu yeye aliwateua na tena aliwaita mwenyewe waje katika mkutano huu,” alisema na kuongeza kuwa:
 
“Ni kitendo kisichofaa kabisa katika nchi yetu wakati tungali tunatengeneza demokrasia. Bahati nzuri alilizungumza hili mbele yenu, hapa mmeniuliza maoni yangu kuhusiana na hotuba hii maoni yangu ndiyo hayo siiungi mkono hotuba yake.” 
 
Mwakiposya alisema Sadifa aliongea kuhusiana na suala la mapenzi ndani ya baraza hilo kwamba limekuwa likisababisha kuvujishwa kwa siri za vikao, jambo ambalo alisema halina ukweli wowote. 
 
Alisema mwenyekiti huyo katika hotuba yake aliwatuhumu meza kuu (viongozi wa juu wa umoja huo ), kuwa wamekuwa wakijihusisha na mapenzi na hivyo kazi hazifanyiki jambo ambalo halina ukweli.
 
“Mimi kama mjumbe wa Baraza Kuu nimesikitishwa, nimeguswa, sifurahishwi na hayo yaliyojitokeza katika hotuba hiyo, “ alisema Mwakiposya huku akisisitiza kuwa hayo ni maoni yake binafsi.
 
Kuhusu suala Mwenyekiti huyo kutamka wakati akiwania nafasi hiyo aliingizwa katika makundi yanayojiandaa kwa ajili ya urais, Mwakiposya alisema: “Hiyo ndiyo tabu ya kuwa na kiongozi anayeamini katika hili huku anatenda hivi.” 
 
“Alipowateua hawa watu aliowafukuza tuliamini kuwa haegemei katika makundi, lakini katika utekelezaji hakuna….Mimi sifahamu katika UVCCM kama kuna makundi, lakini baada ya kusema hilo nikajua kuwa kumbe kuna makundi,” alisema. 
 
Na kwa upande wa siri kuvuja, alisema yeye ni mmoja wa watu ambao anaamini kuwa kiongozi yoyote anayevujisha siri za vikao hafai katika uongozi. 
 
Hata hivyo, alisema hajawahi kusikia kuhusiana na kuvujishwa kwa siri za vikao na viongozi licha ya kuwafahamu viongozi mbalimbali wa umoja huo. 
 
“Tunaonyana ndani ya vikao halali hatuwezi kuzungumza  kwa waandishi wa habari mambo ambayo tunayaona kuwa hayaendi sawa tutayazungumza ndani ya vikao vyetu,” alisema alipoulizwa kuhusiana na kauli kuwa kuna baadhi ya makundi yalionekana kukaa kabla ya kuanza kwa  kikao cha siku ya jana. 
 
Kuhusu madai ya kutaka kumng’oa mwenyekiti wao, Mwakiposya alisema hajasikia kitu kama hicho na kwamba kama kinakuwapo umoja huo unataratibu za kikanuni za kufuata ili kumng’oa mwenyekiti. 
 
“Kanuni ya mwaka 2008 inasema kama ikithibitika kiongozi yeyote amekiuka kanuni Baraza linaweza kutoa pendekezo katika kikao cha juu kumsimamisha, lakini kama sisi tunataka kumsimamisha kama vijana hatujafikia huko bado,” alisema.
 
Alisema iwapo ikidhibitika kuwa hawawezi kwenda sambamba na kiongozi yeyote yule basi watafukuzana. 
 
Alipoulizwa kama mwenyekiti huyo amekiuka kanuni yoyote, alisema amekiuka kanuni ya kufukuza watumishi wa umoja huo kwa kumfukuza mmoja wa watumishi kutoka Zanzibar. 
Alifafanua kwa mujibu wa kanuni, kikao chenye mamlaka ya kumfukuza mtumishi ni Baraza Kuu la Umoja wa Vijana. 
 
Kwa upande wake, Mjumbe Halmashauri Kuu ya CCM (jina tunasitiri), alisema alisikia tetesi kuhusiana na kung’olewa kwa mwenyekiti, lakini UVCCM ni jumuiya ya muda mrefu ambayo ina taratibu zake za kumuondoa kiongozi. 
 
“Usiwaone hivi, hawa ni viongozi waliokomaa, hakuna ambalo linaweza kuharibika ila inachofahamu hakuna mtafaruku na kama ulikuwapo umeisha,” alisema na kuongeza wajumbe hao wako salama na wanaendelea vizuri. 
 
Alisisitiza kuwa hakuna mkanganyiko utakaotokea mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha siku mbili ambacho kitafuatiwa na semina na kwamba hakuna kitu kipya kwa kuwa kila inapokaa jumuiya hiyo kumekuwa na harakati.
 
Katika tukio jingine waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari,  walijikuta wakikalishwa na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Mboni Mhita, kwa zaidi ya saa tatu katika ukumbi wa mikutano wa sektarieti ya chama hicho. 
 
Mhita aliwaita kwenye chumba hicho, kwa madhumuni ya kuwaeleza kile kilichotokea katika kikao hicho kwa siku mbili za juzi na jana. 
 
“Tukubaliane nitazungumza nitazungumzia agenda za jana (juzi) na kinachoendelea leo (jana), tu, lakini sitazungumzia yatokanayo…ama vinginevyo muendelee kumsubiri Katibu Mkuu aje aongee nanyi,” alisema. 
 
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuletewa faili aliloliitisha, aliondoka na kuwataka waandishi wa habari kuendelea kusubiri kwa sababu alikuwa akimsubiri mjumbe wa kitengo fulani aje azungumzie mambo ambayo hata hivyo hakuyafafanua.
 
Akijibu madai hayo, Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge, alisema walipanga kuanza kikao saa 7:00 mchana na kwamba kwa kuwa wajumbe wanafahamiana kukaa katika makundi si kosa.
 
“Maana Katiba yenyewe inaruhusu watu kukaa vikundi ili mradi wawe hawavunji taratibu, sheria na kanuni…baada ya muda kufika si waliingia kwenye kikao kama jana (juzi) kikao kilikuwa kizuri tofauti na vyombo vya habari mlivyokuwa mkisema huko nje,”alisema.
 
Kuhusu hoja ya kumng’oa kwa madai ya kukiuka kanuni, Sadifa alihoji  “ Kanuni namba ngapi?.. Jamal hajafukuzwa sasa wewe utuambie aliyemfukuza ni nani? Jamal ni mjumbe halali wa hiki kikao kama angekuja lakini kwa bahati nzuri ama mbaya, Jamal mwenyewe alinifuata baada ya majina kurudi na kuniambia kuwa amechoka anataka apumzike.”
 
Alisema  kwasababu Jamal anafanya kazi mbili Zeco visiwani  Zanzibar na katika Chama kama Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Vijana, alimuomba apumzike ili aendelee na utumishi wake serikalini. 
 
 Kuhusu hotuba yake kuwadhalilisha, Sadifa aligeuka mbogo: “Nani, wajumbe? Tutajie? ama wewe? Eh, tuthibitishie.”
 
Hata hivyo, alikanusha kuwa hakuna mjumbe aliyedhalilishwa wala aliyelalamikia hotuba yake na kuwalaumu waandishi wa habari kuwa wana matatizo ya kuwagombanisha watu.
 Kuhusu Makonda, alisema kanuni ya Umoja wa Vijana inasema yeye anateua mtu  ambaye anatakiwa kuthibitishwa ndani ya kikao cha Baraza Kuu la umoja huo na kanuni hizo haziruhusu kupeleka kila kitu katika vyombo vya habari.
 
 Alisema baada ya kuona magazeti yamemnukuu Makonda akisema kuwa hawezi kukubali uteuzi huo ili asije kuonekana kuwa amehongwa, alifahamu hizo ni hasira za uchaguzi.
 
 “Kwa hiyo mimi nilimpigia simu mmoja mmoja, Makonda  Msarika, jamani nimeona statement (taarifa), hizi katika magazeti haya, hebu niambieni uteuzi huu mmeukubali ama mmeukataa? Wao wenyewe hakuna aliyekuja kunipa kauli yake kama wamekubali uteuzi,” alisema.
 
 Alimtolea mfano Makonda kuwa amemwita wakutane lakini alikataa,” unajua siasa lazima ukae na mwenzako mzungumze mbadilishane mawazo ndiyo siasa, jana usiku (juzi ), baada ya kumaliza kikao, nilimpigia tukutane…tukae tuvunje migogoro iliyokuwapo, lakini hakuonekana.”
 
Alisema baadhi ya wajumbe walipoona ujio wa Makonda, walitaka kufanya vurugu wakihoji juu ya ujio wake.
 
“Kwa sababu pia baadhi ya wajumbe kwa kuona Paul Makonda, pale walitaka kuanzisha vurugu, kwa busara tukatuliza sijui tumeelewana vizuri?...Alitakiwa baada ya kusomwa kanuni na kujulikana wajumbe, basi wajumbe wabaki kwa wakati ule si mjumbe kwa maana hakuthibitishwa na Baraza Kuu kwa hiyo alitakiwa kwanza atoke ili Baraza Kuu liridhie ama lisiporidhia sawa,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE


MULUGO: MATOKEO YA KIDATO CHA NNE KUTANGAZWA LEO

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philipo Mulugo

 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inatarajia kutangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana.
 
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philipo Mulugo, aliiambia NIPASHE katika mahojiano jana kuwa taratibu zote kwa ajili ya kutangaza matokeo hayo zimekwisha kukamilika na sasa yatatangazwa rasmi leo. 
 
Wiki iliyopita Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza ajira mpya za walimu aliahidi kuwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yatangazwa mwishoni mwa wiki hiyo, lakini hata hivyo hayakutangazwa.
 
Dk. Kawambwa ambaye aliulizwa ni kwa nini matokeo ya mtihani huo yanacheleweshwa kutangazwa ukilinganisha na miaka ya nyuma, alisema kimsingi hayajachelewa kwa sababu wanafunzi watakaochaguliwa kuingia kidato cha tano wanatakiwa kuripoti mwezi Julai mwaka huu. 
 
“Kila mtu anauliza suala la matokeo, kimsingi hatujachelewa sababu hata wanafunzi watakaochaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano watajiunga mwezi Julai, Mungu akipenda yatatangazwa kabla ya Jumamosi,” alisema Dk. Kawambwa.
 
CHANZO: NIPASHE


CHADEMA KUITIKISA ARUSHA LEO

 
 
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo kinafanya mkutano mkubwa wa hadhara Arusha,ambao pia utatumika kuzindua utekelezaji wa sera yake ya utawala wa majimbo kwa kuzindua Jimbo la Kaskazini.
Katibu wa Muda wa Kamati ya Uratibu Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema mkutano huo utafanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro na utahudhuriwa na wabunge wote wa Chadema kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini na kuhutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe. Kwa mujibu wa Golugwa, Kanda ya Kaskazini inajumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
“Tunazindua Kanda ya Kaskazini kutekeleza uamuzi wa Baraza Kuu lililoagiza mfumo na shughuli za uendeshaji wa chama ushuke hadi ngazi ya majimbo ambayo ndiyo sera ya Chadema,” alisema Golugwa.
Kabla ya mkutano wa leo, viongozi zaidi ya 200 wa Chadema kutoka mikoa na majimbo 30 ya Kanda ya Kaskazini wakiwamo wabunge, wenyeviti, makatibu, wenyeviti na mameya wa Halmashauri zinazoongozwa na Chadema,walifanya vikao vya ndani kuweka mikakati na mfumo wa utendaji kikanda. Kwa mujibu wa Golugwa, ambaye pia ni Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, kikao cha ndani pia kilihudhuriwa na mwasisi na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei.
Mbowe ambaye ni mmoja wa wajumbe waliohudhuria vikao vya ndani, ndiye atakuwa mgeni rasmi na mzungumzaji mkuu kwenye mkutano wa hadhara ambao pia utatumika kuwatambulisha wajumbe wa timu ya uratibu ya Kanda ya Kaskazini.
Mkutano huo ni wa pili kwa Chadema ndani ya wiki mbili zilizopita baada ya kufanya mkutano mkubwa Dar es Salaam uliotumika kuueleza umma udhaifu wa mhimili wa Bunge na ukandamizaji  unaodaiwa kufanywa dhidi ya wabunge wa chama hicho na uongozi wa mhimili huo wa dola.
Katika mkutano huo, viongozi wa Chadema waliutangazia umma namba za simu za Spika Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai ili wananchi wawapigie au kuwatumia ujumbe mfupi kuwashinikiza kufuata Katiba, Sheria na Kanuni za bunge katika uendeshaji na maamuzi ya chombo hicho.


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU