Facebook Comments Box

Wednesday, October 17, 2012

KILICHOMUUWA KAMANDA BARLOW CHAHUSISHWA NA KISASI CHA MAPENZI

MWELEKEO wa upelelezi wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow umebadilika na sasa tukio hilo linahusishwa na kisasi cha mapenzi na tayari mtu mmoja anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi Mwalimu Dorothy Moses kutiwa mbaroni na polisi.Awali, ilidaiwa kwamba Kamanda Barlow ambaye aliuawa kwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi muda mfupi baada ya kumfikisha mwalimu huyo nyumbani kwake, alivamiwa na majambazi. Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI, Robert Manumba alithibitisha jana kukamatwa kwa mtu huyo (jina tulihifadhi) akisema: “Ni kweli mtu mmoja amekamatwa, lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia kwa kina kuhusu suala hilo kwa sababu bado tunamhoji na tunaendelea na uchunguzi. Tutakapokamilisha, tutatoa taarifa.” Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola pia alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo. Hata hivyo, alisema amesikia habari hizo kwa kuwa yuko safarini kwenda mkoani Kilimanjaro kwenye mazishi ya kamanda huyo... “Hayo nimesikia, lakini kwa sasa sipo Mwanza hivyo siwezi kuzungumzia lolote.” Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinaeleza kwamba upelelezi wa mauaji hayo umefanikiwa kwa hatua kubwa na kwamba mtu huyo alikamatwa Dar es Salaam baada ya kuwekewa mtego na makachero waliopo katika timu ya uchunguzi na alisafirishwa hadi Mwanza ambako anashikiliwa na jeshi hilo. Ilielezwa kuwa mtu huyo alikamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa za siri za kiitelejensia kutoka kwa watu mbalimbali. “Kuna hali imefunguka na imesaidia sana. Inaonyesha kwamba Dorothy alikuwa na uhusiano na mtu huyu ambaye alikuwa akifika nyumbani kwake, kama mumewe na watu wanajua jambo hili,” alieleza mmoja wa askari polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini. Alisema kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba uamuzi wa mwalimu huyo kusitisha uhusiano wa mapenzi na mtu huyo huenda ndicho chanzo cha mauaji hayo lengo likiwa ni kumshawishi Dorothy kurejesha uhusiano. “Mimi natambua kwamba huyu jamaa na Dorothy walikuwa na uhusiano na inajulikana mjini kuwa hata mke wa mtuhumiwa anatambua jambo hilo kwani walishagombana siku moja mjini na hata katika msiba nyumbani kwao na mtuhumiwa,” alisema mama mmoja (jina tunalo), aliyejitambulisha kama mmoja wa marafiki wa karibu wa Dorothy. Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitangiri (jina tunalo), anasema amekuwa akimfahamu mtuhumiwa aliyekamatwa kama baba mwenye nyumba hiyo na kila mara amekuwa akimkuta hapo nyumbani wakati wa kujisomea na wanafunzi wenzake. “Mimi ninamfahamu kama baba wa rafiki yangu na nimewahi kumkuta wakati wa kujisomea hapo nyumbani na watoto wa nyumba hiyo.” Dorothy ambaye ametajwa kuwa mjane, ni Mwalimu katika Shule ya Msingi Nyamagana na tangu kufariki kwa mumewe Ofisa wa zamani wa TRA, Modest Lyimo mwaka 1997. “Watu wote wanajua kwamba mtuhumiwa alikuwa akitembea na huyo mwalimu, wameonekana mara nyingi wakiwa muziki,” alieleza mmoja wa ndugu wa karibu wa mke wa mtuhumiwa. Hili ni tukio la tatu mkoani Mwanza kutokea kwa ofisa wa polisi kuuawa. Katika tukio la awali lililotokea mwaka 1987, askari aliyetambulika kwa jina la Inspekta Gamba aliuawa kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi eneo la Nyakato na katika tukio la pili mwaka 1997, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Kati ASP Mahende aliuawa kwa kupigwa risasi eneo la Bugando saa nne usiku alipokuwa akifuatilia majambazi waliokuwa wakijitayarisha kuvamia. Dar wamuaga Kamanda Barlow Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliongoza waombolezaji waliofika kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Barlow nyumbani kwake, Ukonga Dar es Salaam jana. Mwili wa Kamanda Barlow ambao unasafirishwa leo kwenda mkoani Kilimanjaro kwa mazishi, uliwasili nyumbani kwake saa 6.45 kabla ya kupelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Ukonga kwa ajili ya ibada na kutoa heshima za mwisho. Akitoa salamu za Serikali, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima alisema kifo cha Kamanda Barlow ni pengo kwa taifa... “Tutahakikisha watuhumiwa wanapatikana kwa mikono yote miwili na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.” Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema alisema juhudi za kuwasaka watuhumiwa zinaendelea kwa ushirikianao wa wananchi. “Kifo cha Kamanda Barlow kimeacha pengo kwani hivi sasa askari mmoja analinda watu 1,300 hivyo kwa kifo chake unaweza kuona ni pengo la aina gani na ukilinganisha yeye alikuwa kamanda wa mkoa mzima,” alisema IGP Mwema. Alisema jeshi lake litaendelea kulinda amani ya wananchi na kifo cha Kamanda Barlow kinalifanya liongeze nguvu. Akitoa mahubiri, Padri Veri Urio alisema kila jambo hutokea kwa wakati na kifo cha Kamanda Barlow kimesababishwa na watu. Alisema mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa mtu ni Mungu pekee hivyo waliosababisha kifo chake siku ikifika, watajibu kwa nini walifanya hivyo. IGP Mstaafu, Omary Mahita alisema atamkumbuka Kamanda Barlow kwa uchapaji wake kazi tangu akiwa polisi Interpol (polisi kimataifa)alifanya kazi kwa weledi uliotukuka. “Daima nitamkumbuka kwani nimefanya naye kazi sehemu tofauti na askari waliobaki waige mfano wake wa uwajibikaji” alisema Mahita. Mbali ya Dk Bilal, viongozi wengine walioshiriki katika ibada hiyo jana ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, makamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), makamanda wa polisi, viongozi wa Serikali na vyama vya siasa na wananchi.

Saturday, October 13, 2012

MNYAMA AANZA KUSUASUA




DK: Mpira unamalizika hapa uwanja wa Mkwakwani kwa matokeo ya sare tasa.

DK 85: Simba  0 - 0 Coastal

DK 78: Atupele Green anakosa bao la wazi 

DK 75: Coastal wanafanya mabadiliko anaingia Danny lyanga anatoka Soud.

DK 68: Simba wanafanya mabadiliko anatoka Daniel Akuffoer anaingia Salim Kinje.

DK 65: Nsa Job anapewa kadi nyekundu baada ya kupewa kadi ya pili ya njano.

DK 63: Nsa Job anapiga shuti kali linaokolewa kwa ustadi mkubwa na Juma Kaseja.

DK 60: Mwamuzi anawapa kadi za njano Nsa Job na Amir Maftah.

DK 55: Coastal wanakosa bao la wazi huku Simba wakifanya mabadiliko anatoka kinda Haruni Chanongo anaingia Uhuru Suleimani.

DK 47: Anaingia Lameck Dayton kuchukua nafasi ya Razack Khalfan aliyeumia.

DK 46: Kipindi cha pili kinaanza na ghafla Razack Khalfan anakaa chini akionekana kuwa na maumivu, machela zinambeba na kumtoa nje ya uwanja kwa jinsi inavyoonekana sidhani kama atarudi dimbani.

Mpira ni mapumziko hapa Mkwakwani Simba 0 - 0 Coastal.

DK 45: Coastal wanaendelea kuishika nafasi ya kiungo kwa sababu Selembe, Razack na Santo wanaelewana sana pia udhaifu wa Boban katika kukata unawapa wakati mgumu Kiemba na Kazimoto katika kuweza kumiliki dimba.

DK 40: Nsa Job anakosa bao la wazi bada ya kazi nzuri iliyofanywa na Selemani Kassim.

DK 35: Timu zote zinafanikiwa kufika kwenye lango la wapinzani lakini wanashindwa kuzitumia nafasi zao vizuri.

DK 30: Coastal 0 - Simba

DK 26: Simba wanapata kona yao ya kwanza lakini haizai matunda.

DK 25: Coastal wanaonekana kutawala sehemu ya kati ya kiungo inayochezwa na Jerry Santo na Razack Khalfan.

DK 20: Coastal 0 - 0 Simba

DK 15: Kichwa kizuri cha Felix Sunzu kinatoka nje.


DK 13: Haroun Chanongwa anapiga bonge la shuti linagonga mtambaa wa panya kipa wa Coastal Chove anashindwa kuzuia.


DK 10: Simba 0 - 0 Coastal


DK 9: Coastal wanafanya shambulizi la kushtukiza na mpira unatoka juu ya lango.


DK 1: Mpira unaanza hapa mkwakwani - Simba wamevaa jezi nyeupe na bukta nyekundu, Coastal wamevaa jezi nyekundu juu nyeupe chini.
endelea kufuatilia mtandao huuu tutakuletea picha zote za mchezo huu wa leo. 


PICHA YA JOE MAKINI YAVUJA

Picha ikimuonesha mwamba wa kaskazini a.k.a mweusi Joe makini akiwa na mrembo warda. picha hii imevuja. samahani lakini.....

KWA HERI KAMANDA LIBERATUS BALLOW

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza RPC Liberatus Ballow ameuwa usiku wa kuamkia leo na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi katika eneo la Kitangiri karibu na Hotel ya Tai Five majira ya kati ya saa saba hadi nane. Haya yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Mwanza Injinia Everest Ndikillo wakati akitoa taarifa za tukio la kuuawa kwa Kamanda Ballow. Tukio hilo ambalo limeacha simanzi kubwa kwa wakazi wa jiji la Mwanza pamoja na familia yake huku watu wa kijiuliza kuhusiana aliyehusika na mauuaji hayo ya kikatili. Taarifa ya Mkuu wa Mkoa zinasema kuwa Kamanda Ballow alikiuwa anatoka katika kikao cha harusi na ndugu yake aitwaye Sembeli Maleto kilichokuwa kinafanyika katika Hotel y a Florida na kish akumpelek amwanamke aitwaye Dorcas Moses Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Nyamagana maeneo ya barabara ya Kona ya Bwiru kwenda Kitangiri. Walipofika getini kwa Mama Dorcas mara waliwaona watu wawili wakiwa wamevaa makoti ya PolisiJamii, Mama Dorcas alimuuliza Kamanda Ballow kama anawafahamu Kamanda akasema kuwa hawa na watu wa ulinzi wa Jamii wako doria. Mara wale watu waliongezeka na kuwa sita wakaanza kama kuzozana wao kwa wao na ndipo Kamanda alipowauuliza kuna nini, Mmoja wao akajibu hakuna kitu na ikapelekea Kamanda kutaka kutoka nje ila wale watu watatu wakaizingira gari ya Kamanda Ballow aina ya Rav 4. Kamanda Ballow alipoona kama hali hewa inabadilika alichukua redio call ili aweze kuwa taarifu askari na ndipo wale jamaa walipompiga risasi kichwani nakupelekea kifo chake. Taratibu za mazishi ya Kijeshi bado zinaendelea na nyumbani kwa marehemu ambapo mwandishi wa blogu hii amefika na kukuta watu mbalimbali wakiwa katika hali ya majonzi sana. Mke wa Kamanda Ballow yuko Dar es Salaam na anatarajia kufika Mwanza. Mpaka sasa Polisi wanamshikilia mtu mmoja aitwaye Dorcas kwa ajili ya Mahojiano huku uchunguzi mkali ukiendelea kuhusiana na kifo cha kamanda Liberetus Ballow.

Wednesday, October 10, 2012

NANI NI CCM-B? CHADEMA AU CUF?


Madhumuni ya Chama cha wananchi CUF kama yalivyo katika Katiba  yake ni, “Kuwaunganisha watanzania wakatae uonevu,kudhalilishwa,kunyanyaswa,kubaguliwa au maovu mengine yanayoweza kufanywa dhidi ya heshima ya utu wa binaadama, yawe yanayotendwa na Serikali, kikundi cha watu walio na uwezo kwa ajili ya mabavu yao au kwa ajili ya kujinufaisha kwao kiuchumi au kisiasa na kiitikadi au kwa kujali dini, kabila jinsia au rangi zao”. (Kifungu cha, 6[1] Katiba ya CUF uk.12)

Na, JUMA DUNI HAJI


Kwa kiasi miaka miwili sasa ndugu zetu wa CHADEMA wamekuwa wafanikiwa wakisambaza na kufanya siasa nyepesi nyepepi za maji taka kwa watanzania bara kwamba eti CUF ni “CCM-B” kwa sababu ya kuunda Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar (Government of National Unity Zanzibar) Dhamiri yangu leo ni kufanya uchambuzi na kuweka wazi kwamba hoja ni “U-CCM-B” au choyo na Kuchukizwa kwa CHADEMA kwa wazanzibari kusikilizana? au ni ukosefu wa dira na agenda sahihi ya kisiasa? Hoja hii ya “U-CCM–B” imerejewa tena na viongozi wa CHADEMA pale Mheshimiwa. James Mbatia alipokubali uteuzi wa Rais Kikwete wa kumteua kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Watanzania wanapaswa kufahamu kwamba kilichopo pale Zanzibar ni SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA SIYO VYAMA VYA UMOJA WA KITAIFA. Hakuna chama cha CUF wala CCM ambacho kimeungana na kufanya viwili hivyo kufanya umoja unaoitwa CCM-CUF Taifa au vinginevyo. Serikali ya umoja wa kitaifa ilipatikana baada ya kura ya maoni ya Tarehe 31 Julai, 2010 kupigwa na asilimia 66.3 ya wazanzibari bila kujali ni chama gani walikubali kuundwa Serikali hiyo ya GNU. Ni wananchi wa Zanzibar siyo wanachama wa vyama waliopiga kura ya maoni. Tunapokutana katika baraza la mawaziri hatukutani viongozi wa vyama , bali ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi (Siyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi) wanaokutana na kujadili masuala ya maendeleo ya nchi yao na wala si maendeleo ya vyama vyao, wakati wowote chama cha Mapinduzi wanapokutana huwa wanazungumza masuala ya chama chao, na CUF huzungumza chama chao. Kwenye baraza la mawaziri tunazungumza nyaraka za  wizara za Serikali siyo za idara ya chama chochote kati ya hivyo viwili. Sasa huu “U-CCM-B au A” unatoka wapi.

Kama hoja ni chama kuingia Serikalini! Hebu tuone  “UCCM-B” upo wapi?

Madhumuni ya Chama cha wananchi CUF kama yalivyo katika Katiba  yake kifungu cha, 6[8] Katiba ya CUF uk.13) ni “kushika hatamu za dola ili dola au serikali itekeleze vizuri itikadi na sera za chama na ustawi wa Taifa letu” Chama cha siasa ambacho hakina malengo ya kuunda serikali na au kuingia serikalini kuweza kusimamia utekelezaji mzuri wa sera na itikadi na badala yake inajielekeza katika kazi ya kulipua “MABOMU” na kung’ang’ania kupiga kelele za ufisadi hali chama chenyewe na watendaji wake wakiamini kuwa ufisadi ni sehemu ya njia ya kupata manufaa ya kisiasa na kiuchumi, tunavishukuru vyombo vya habari kwa kutujulisha kuhusu hali hii. Hebu tujikumbushe tuone “UCCM-B” upo wapi? Mwaka 1991 Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi Rais wa CCM alimteua Mabere Marando (NCCR) kuwa mjumbe wa Tume ya kuratibu maoni ya wananchi juu kuanzishwa mfumo wa Chama kimoja au vyama vingi chini ya Mwenyekiti Jaji Nyalali, Mwaka 2001, Mabere Marando huyu huyu alichaguliwa na bunge  kuwa Mbunge wa Bunge la EAC akiwa NCCR na kumshida marehemu Bob Makani aliyesimamishwa na CHADEMA, CHADEMA wakarudia, lugha hii wanaowaambia wazanzibari kwamba NCCR Mageuzi ni CCM-B. Leo Mheshimiwa. Marando ni CHADEMA, U-CCM–B wake umeyayuka maana kaingia katika chama kitakatifu kinachopokea maono kutoka kwa Mungu?

Mwaka 2008 Mheshimiwa Rais  Jakaya Kikwete alimteua Zitto Kabwe kuwa mjumbe wa Kamati ya Madini chini ya Mzee Jaji Mark Bomani. Iliandikwa kuwa Mheshimiwa Mbowe amekatisha masomoni yake kutoka nchini ujerumani alikuja kwenye kikao kuthibitisha uteuzi huo, Si Zitto Kabwe wala  chama cha CHADEMA kilichojitangaza kuwa wao ni CCM-B ! , Mwaka huu Rais Kikwete amemteua Prof. Mwesiga Baregu kuwa mjumbe wa Kamati ya kuratibu maoni ya uandikwaji wa katiba ya Jamhuri ya Muungano. Viongozi wa CHADEMA Mr. Slaa na Tundu Lissu wakampongeza Rais na Prof. Baregu, lakini muasisi wa CHADEMA akasema uteuzi huo wa Mheshimiwa Kikwete una “UDINI” akimaanisha WAISLAMU WAMO KATIKA HUO UTEUZI WA KIKWETE!!! HATA hivyo CHADEMA haijawa CCM-B.

John Mnyika na Tundu Lissu walikua na kesi za uchaguzi dhidi ya CCM kule Singida na pale Ubungo. Kesi hizi wameshinda zote chini ya utetezi wa mwanasheria Mkuu wa Serikali ya CCM. Hawasemwi kwamba wametetewa na mwanasheria  wa serikali ya CCM na hivyo ni CCM-B!, April 17, 2012 umefanyika uchaguzi mwengine wa EAC pale bungeni na CHADEMA walikua na wabunge 43 kati ya 48 wa chama hicho wakati kura zikipigwa. Antony Komu mgombea wa CHADEMA alipata  kura 93, kura 50 kati ya hizo zilikua za  wabunge wa CCM. CHADEMA wakaenda mahakamani ili uchaguzi urudiwe ili wapate nafasi ya kuwapata wabunge zaidi kumchagua Komu. Hapa UCCM-B. haukuwepo? Tarehe 22/08/2012 Mahakama kuu kanda ya Tabora imetengua matokeo ya Uchaguzi Jimbo la Igunga na kuwapa ushindi wa kesi hiyo CHADEMA. Uchaguzi utarudiwa. Jee CHADEMA wamesaidiwa na Jaji wa Serikali ya CCM na hivyo na wao ni CCM-B?  Mheshimiwa, James Mbatia alikua na kesi ya uchaguzi ya Jimbo la Kawe lakini akashindwa na Halima Mdee (CHADEMA). Mbatia akaenda Mahakamani kisheria. Viongozi wa CHADEMA wakatafuta njia za kiungwana kumaliza tatizo hilo nje ya Mahakama. Tarehe 6 Februari 2012 makatibu wakuu wa NCCR-Mageuzi Samwel Ruhuza na Wilbroad Slaa walikubaliana kufutwa kwa kesi hiyo No.101/2010 na kumuacha Halima Mdee abaki kuwa Mbunge. Jee Halima nae ni NCCR-B au Mbatia CHADEMA-B?

Mwaka 2001 Rais Mkapa alimteua Mh. Hamad Rashid kuwa Mbunge, wakati huo siasa za ushabiki na mapambano zilikua kubwa mno na CHADEMA kilikuwepo- hoja ya CCM-B hawakuisema. Mwaka 2009 Mheshimiwa Rais Kikwete alimteuwa Mheshimiwa, Ismail Jusa kuwa Mbunge Hoja za “UCCM-B” haikuwepo! Mwalimu Nyerere aliwahi kumpigia kura Paulo Ndorobo wa NCCR-Mageuzi jimbo la Musoma  na Mheshimiwa Ndorobo akashinda Nyerere alikuwa NCCR?

Kuna lugha ya kiswahili ya kuonewa bata kwa sababu ya umbo na sifa zake. Bata akitembea huambiwa anakata viuno kama mrembo wa Tanzania. Hivyo ndivyo alivyoumbwa, hakuchagua kukata viuno anapotembea na wala hajui kwamba anafanya hivyo. Bata huyu huyu anapotafuta chakula kwenye tope huambiwa anakula uchafu sina hakika kwamba CHADEMA wanapokubali uteuzi wa Rais huyu huyu ikawa ni sahihi chakula chao safi, lakini wengine wanapoteuliwa na Rais, kwa CHADEMA hua sawa na kula tope za choo. Kwa  CHADEMA  kuku anapokwenda haja kubwa hua anakunya, lakini bata huambiwa kahara, hakunya: wote wamekunya mmoja amekunya kutu ngumu mwengine kanya kutu laini, wote wamekunya mavi ya kuku na yote yananuka.Vipi CHADEMA wao wajione watakatifu wanapopata uteuzi kwa Rais wengine wawe wamekufuru, huu ni unafiki na uzandiki wa viongozi wanaotaka eti wapewe dhamana ya kuongoza nchi kwa akili kama za Panzi. Kule Kigoma CCM na CHADEMA walikubaliana na CCM kuunda Serikali ya Halmashauri ya Kigoma nusu kwa nusu ya madiwani kwa miaka mitano. Hoja ya CCM kuioa CHADEMA CCM-B haikutajwa, yaani yale kwa CHADEMA  yalikua na mavi ya kuku CUF na CCM Zanzibar ni uharo wa bata. Kule Arusha kulikua na Serikali ya aina hiyo, mpaka yalipotokea malumbano na upuuzi wa wawakilishi wa wananchi [madiwani] walipozuiliwa na chama chao CHADEMA kuwawakilisha barazani.

Wengi tumezoweshwa kwamba siasa ni uongo na mchezo mchafu, Hapana, Moja ya suala ambalo CUF na viongozi wake tunalisimamia na kutaka watanzania waamini kuwa Siasa si uongo wala si mchezo mchafu bali baadhi ya wafanya siasa[wanasiasa] ndio waongo na wachafu. Kama viongozi wanaweza kusema uongo wa kiwango cha uharo wa bata wakiwa nje ya Ikulu watakunya nini hawa wakiingia ikulu? Kama kuna viongozi wanaweza kuiba wake za watu na kuja jukwaani kujisifu kwamba wao ni wezi wa wake za watu, jee wakiwa ikulu watafanyaje hawa?, watawapanga foleni wanawake wote waliopo pale kwa uwezo wa  madaraka yao ya urais na kuwalazimisha kufanya nao ngono. Hivyo tunategemea hawa wakajenge nyumba ya umalaya pale ikulu, je nyie ndiyo munashangilia hayo? Eti kunja ngumi, ngumi gani ya wizi wa wake za watu? Eti kunja ngumi, ngumi ya kutengeneza vifo vya watanzania wenzetu? Watanzania muna kila sababu za kutafakari na kuchukua maamuzi sahihi juu ya hatma na mustakbali wa maisha yenu ya sasa na kizazi kijacho, wapi pa kuunganisha nguvu zenu ili mabadiliko ya kweli kiuchumi na kisiasa yaweze kupatikana. Siasa za milipuko na mihemuko za leo linasemwa hili na kesho linasemwa vinginevyo jambo hilohilo hazina nafasi kwa CUF ya DIRA YA MABADILIKO.

SUALA LA U-A na U-B unatoka wapi na unakujaje katika mahusiano ya chama kimoja na kingine wakati kilichojenga umoja ni ridhaa ya wazanzibari. Mwaka 2005 hadi 2010, wabunge wa Chama cha wananchi CUF kiliunda kambi ya upinzani na wabunge wa CHADEMA bungeni kwa miaka mitano, na Dk. Slaa akawa Naibu kiongozi wa kambi hiyo kwa muda wote wa miaka mitano. MheshimiwaZitto na wabunge wengine wa chama hiki wakishika nyadhifa za uwaziri kivuli wa Kambi hiyo. Ilikua ni Serikali kamili nje ya Serikali ya Muungano. Vyama viwili hivi viliendelea kubaki na shughuli zake ndani na nje ya Bunge. Mbona hoja ya CHADEMA kujiita CUF-B haikuja wala hawakujigamba hivyo kuwa wao ni CUF-B? Chama cha wananchi CUF kilifanya hivyo kwa sababu madhumuni yake ni: “Kuwaunganisha watanzania wakatae uonevu,kudhalilishwa,kunyanyaswa,kubaguliwa au maovu mengine yanayoweza kufanywa dhidi ya heshima ya utu wa binaadama, yawe yanayotendwa na Serikali, kikundi cha watu walio na uwezo kwa ajili ya mabavu yao au kwa ajili ya kujinufaish kwao kiuchumi au kisiasa na kiitikadi au kwa kujali dini, kabila jinsia su rangi zao”.

Muda wote huu vyama vya upinzani tumeshindwa kuungana na kukiondoa chama cha CCM kwa sababu ya udhaifu huu wa CHADEMA kujikubalisha kujigawa mafungu huku CCM ikichekelea na kutuona wajinga. Ujinga na upumbavu huu umezidi tulipogundua kwamba Viongozi wa CHADEMA wanaonesha udhaifu wao kwa kukosa furaha kuwaona wazanzibari wanasikilizana na nyinyi wananchi munafurahia hilo kwamba tuaachwe wazanzibari tuuwane na kwamba eti hicho ndiyo chama munachokitaka eti kiingie Ikulu. Msimamo huu wa CHADEMA ni kuthibitisha kwamba Wazanzibari kugombana ndiyo furaha ya viongozi wa Chama hicho, maana furaha na agenda ya muda mrefu ya baadhi ya viongozi watanganyika wawe wa CCM au CHADEMA ni kuhakikisha WAZANZIBARI tunawagawa ili tuwatawale (divide and rule them) Kama hivyo ndivyo wazanzibari hatuna sababu ya kushangaa ya jinsi viongozi wenzetu wa Tanganyika munavyotuona, maana sisi wazanzibari ambao wazee wetu akina mzee Karume na Mzee Thabit Kombo walimuamini mwalimu Nyerere kwa kuunganisha nchi mbili hizi kwa faida ya pande mbili, leo vijana wake waliorithi siasa zake wanaziendeleza kwa kutuambia eti Zanzibar siyo nchi. Wakati viongozi (Tundu Lissu) wanafurahia na kushikilia kwamba Zanzibar siyo nchi, chama hicho hicho kinashikilia hadharani kupitia kwa Joshua Nassari mbunge wa CHADEMA wa Arumeru Maashariki, anapendekeza na kusisitiza kuwa mikoa ya kaskazini ya Tanganyika kujitenga na kua taifa pekee. CUF hatuamini katika siasa za kikabila na kuigawa nchi mapande pande kwa siasa za itikadi za kimajimbo. Maana kama Arusha ijitenge na wasukuma wa Mwanza na Shinyanga ambao ni wengi na ni mikoa miwili tajiri kuliko mikoa yote nao  pia watajitenga na wale wa Mbeya watajitenga na wale kusini kwa wamakonde nao watajitenga. Kwa hivyo hata hiyo Tanganyika pia haitokuwepo. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mara kadhaa kwamba Tanzania ipo kwa sababu ya Zanzibar. Msimamo wetu ni kuwa wazanzibari hawako tayari tena kufanywa koloni la Tanganyika. Kinachohitajika sasa ni kurekebisha makosa yaliyofanywa miaka 50 iliyopita yaliyoasisiwa na mwalimu Nyerere mwaka 1964.

Ninachotaka kuwakumbusha watanzania na Machadema, ni kwamba Mimi binafsi na wenzangu wengi ni wahanga wakubwa wa siasa mbovu za zamani za Zanzibar, tuliathirika sana kwa kubambikiwa kesi za uhaini na kesi za mauaji, leo ni waziri wa Serikali ya umoja wa kitaifa siyo umoja wa vyama vya CCM na CUF. Wazanzibar tumemaliza matatizo yetu ya ndani wenyewe, tumeamua kujenga nchi yetu, wakati nyinyi yenu munaitayarisha ibomoke, sisi huko tumeshatoka. Fursa ya kujenga siasa za kistaarabu, siasa za heshima, siasa zenye lengo la kuwasaidia watu wetu kuondokana na lindi la umasikini, maradhi na ujinga ipo, HATUJACHELEWA! Tuutumie vyema mchakato wa uratibu wa ukusanyaji maoni ya katiba, ipendekezwe uwepo wa UUNDWAJI WA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA, CUF katika manifesto yetu ya mwaka 2010 tuliieleza hili. CUF chini ya dira ya mabadiliko[vision for change] inaamini katika mazungumzo [dialogue],

Kwa hivyo CHADEMA angalieni siasa zenu kama mnataka kuendelea na siasa za kuonja umwagaji wa damu kisha ndo muamini juu ya ‘diablogue’ endeleeni kujaribu, kama munaamini kuwa njia siasa hizo mnazozitaka zisizo na ushirikiano na wenzenu, siasa za nchi isitawalike, siasa za maandamano, siasa za propaganda chafu, siasa za kubaka wake za watu, siasa za kutaja mafisadi wazuri na mafisadi wabaya, kama mnaamini kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo kutoka kwa Mungu. Namaliza kwa kuwaambia Zanzibar kuna Serikali ya umoja wa kitaifa , hakuna muungano wa vyama vya kitaifa, wala hakuna CCM-B wala CUF –G. Kilichopo ni Serikali siyo vyama kuunganisha nguvu kujenga taifa letu. Na ndugu zangu watanganyika hamtaweza katu kumaliza migogoro yenu ya kisiasa na kidini kama hamukuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Mungu Ibariki Tanzania!

Mungu Ibariki Zanzibar!

 

Muandishi wa makala hii ni waziri wa Afya wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar na mjumbe wa baraza kuu la uongozi CUF Taifa. Harakati za kisiasa zilimuweka ndani bila kuhukumiwa miaka mine[4]




Tuesday, October 9, 2012

MAJAMBAZI YAKAMATWA KWA CCTV BAADA YA KUIBA KWENYE M-PESA




JANET JACKSON NDANI YA HIJJAB



Pop star Janet Jackson mwenye umri wa miaka 46 ambae ni mpenzi wa zamani wa producer Jermain Dupri anaolewa mwaka 2013 na tajiri bilionea wa kiarabu Wissam Al Mana na inaaminika kwamba Janet itabidi abadili dini na kuwa muislam

YANGA WALALA TENA MZUNGU WA NNE

HISTORIA ya wachezaji wa Yanga kulala mzungu wa nne imejirudia tena Bukoba, baada ya kulala kwa kubanana katika kitanda kimoja kama ilivyokuwa Mbeya, licha ya kufikia katika Hoteli ya Smart, yenye hadhi kubwa.

Hali kama hiyo ilijitokeza wakati timu hiyo ikijiandaa kucheza na Prisons, Mbeya, huku aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet akianika ukweli ambao baadaye ulimponza na kufukuzwa.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wachezaji alisema, mambo ni yale yale kama ilivyokuwa Mbeya.

“Mambo kama ya Mbeya, hoteli ni nzuri, lakini wachezaji tumelala wawili wawili katika hoteli, pamoja na kupata huduma nzuri lakini tatizo lilikuwa ni hilo,” alisema mmoja wa wachezaji hao.

Hata hivyo wachezaji wanatarajiwa kurejea kwa usafiri wa basi, badala ya ndege maalumu ya kukodi ya Kampuni ya Precision Air, iliyotumika kwenda Kagera kwa ajili ya mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Kagera, uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Habari zilizopatikana kutoka kwa kiongozi mmoja, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, zinasema wachezaji hao watarejea kwa usafiri huo baada ya mchezo wao dhidi ya Toto African, ambao utachezwa keshokutwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Wachezaji hao wanatarajiwa kuondoka mjini Mwanza Ijumaa, baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Toto African, kwa basi maalumu walilopewa na wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania TBL kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.

Hata hivyo, gazeti hili liliweza kuongea na mkuu wa msafara, Mussa Katabaro, ambaye alisema anachojua yeye ni kwamba timu yao itarejea kwa ndege kama ilivyokuja.

Wakati huo huo, uongozi wa Kagera Sugar uliondoa mabango ya wadhamini wa Yanga, Kampuni ya Bia Tanzania, kutokana na kuwa wenyeji wa mchezo huo.

Kagera Sugar ambao ndio wenyeji wa uwanja huo kupitia kwa mratibu wake Mohamed Hussein, ilikataa katu katu mabango hayo kuwekwa katika uwanja huo, kwa kuwa wao ndio wa miliki wake.

MATUMLA NDANI YA MKASI NA SALAMA JABR





VURUGU ZA UVCCM MARA NDIO HIZI




UDA KULITEKA SOKO LA TANZANIA BAADA YA KUPATA MUWEKEZAJI

 
Picture
Viongozi wa Kampuni ya Simon Group na wengine Wakielekea kuzindua mabasi15 waliyowekeza UDA.
KAMPUNI ya Usafiri jijini Dar es Salaam (UDA) imejipanga kuteka soko la usafiri nchini ifikapo mwezi Machi mwaka 2013.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena alipokuwa akipokea mabasi 15 kutoka kampuni ya Tata Africa ya India ikiwa ni sehemu ya mabasi 30 yanayotarajiwa kuingizwa nchini ifikapo Desemba mwaka huu.

Kisena alisema kampuni ya Simon Group iliyowekeza katika shirika la UDA imejipanga kuwa kampuni kubwa barani Afrika kwa mtaji wa Dola25 milioni (sawa na Sh375 bilioni)  utakaowezesha kupatikana kwa mabasi 300 ifikapo mwezi Machi mwakani, “Simon Group imejipanga kuwa kampuni kubwa Afrika ifikapo Machi mwakani na tuna mpango wa kununua mabasi 300 kwa mtaji wa Dola25 milioni,” alisema Kisena.

Aliongeza kuwa kati ya mabasi hayo kutakuwa na mabasi ya wanawake, mabasi ya wanafunzi, mabasi ya binafsi, mabasi ya mikoani na mabasi yatakayosafiri barani Afrika, “Mazingira mabovu ya sasa ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam mara kwa mara yamekuwa yakisababisha udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake, bila shaka wengi wenu mtakumbuka vizuri kisa cha Maumba. Tunataka kukomesha udhalilishaji huo kwa wanawake ili wasafiri kwa uhuru na raha mstarehe,” alisema Kisena.

Kuhusu mabasi ya wanafunzi, alisema yatakuwa matano kila barabara kuu jijini Dar es Salaam na yatafanya kazi hiyo tu.

Kuhusu mabasi ya binafsi (Executive class), alisema yatakuwa na nauli ya juu lakini yatatoa huduma kama vile televisheni, vinywaji, magazeti na kiyoyozi, “Tunataka tuwahamasishe watu wasitumie tena magari yao binafsi. Unajua kwa mwezi mtu hutumia katiya Sh800,000 hadi Sh1milioni kununua mafuta ya gari, hela ambayo ni nyingi mno. Lakini kwa kutumia usafiri huu, inawezekana kubana matumizi,” alisema.

Akizungumzia mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) alisema kuwa wanatarajia kushinda zabuni ya kuuendesha kwa kuwa kampuni hiyo haina mshindani katika usafirishaji nchini, “Kwa sasa Dart inajengwa barabara ya Morogoro na barabara itakamilika mwaka 2014. Kwa sasa tutaendesha mradi huo kabla Dart haijaanza na kwa barabara nyingine baada ya hapo. Kwa kuwa sasa UDA haina mpinzani katika sekta ya usafirishaji nchini, naamini tutashinda zabuni ya kuendesha,” alisema. Aliongeza kuwa mradi huo unatarajia kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 1,500.
Picture
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group,Robert Kisena (wa pili kulia) Wawekezaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA akipokea mfano wa funguo kutoka kwa Meneja wa Biashara wa TATA Afrika Holding Tanzania Ltd,Srinivas Nemalapuri (wa pili kushoto) kulia ni Mkurugenzi wa Simon Group, Leonard Rubuye na kushoto Kaimu Meneja Biashara,Sarvan Keshri. ikiwa ishara makabidhiano ya mabasi 15 katika awamu ya kwanza, hafla hiyo ilifanyika kwenye Ofisi za UDA Dar es Salaam.
Picture
Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group,Robert Kisena (wa nne kushoto) akiwaongoza viongozi wengine ndani ya Basi la UDA.



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU