Gazeti la Wall Street Journal linayo ripoti kuwa
 watengenezaji wa simu maarufu ya iPhone na kifaa cha iPad, Apple 
wanajishughulisha kutengeneza gari litakalotumia umeme ikiwa ni 
changamoto kwa kampuni ya Telsa inayotawala soko hilo kwa sasa.
Taarifa hiyo ya WSJ haijamtaja mtoboa siri hiyo zaidi tu ya kusema kuwa ni mwajiriwa wa Apple anayefanya kazi katika mradi huo.
Mtoa habari huyo ametanabahisha kuwa wapo watu mamia kadhaa wanaofanya 
kazi kwa siri kutengeneza gari hilo la mradi uliopewa jina la "Titan" na
 tayari wameshaunda muonekano unaoelekea kabisa kufanana na 'minivan'. 
Msemaji rasmi wa kampuni ya Apple alipoulizwa kuhusu hilo alikataa kuthibitisha au kukanusha taarifa hizo.
Nalo gazeti la Financial Times lina habari ambayo
 chanzo chake ni mtu ambaye hakutaka kutajwa, akisema kuwa wafanyakazi 
wa Apple wamekuwa wakitafiti kuhusu vipuri vya magari katika eneo moja 
huko Silicon Valley.
Waajiriwa wa hivi karibuni katika kampuni ya Apple ni pamoja na mkuu wa 
kitengo cha utafiti cha Mercedes-Benz katika tawi la Silicon Valley.
