Watoto sita wakiwemo wawili wa kiume wenye umri wa miaka 8 hadi 14 wameharibiwa 
vibaya sehemu zao za siri baada ya kubakwa kanisani na watu wanaodaiwa 
ni wachungaji.
Kamanda wa Polisi Arusha, Leberatus Sabas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na watuhumiwa wa tukio hilo wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini hapo kwa uchunguzi zaidi.
Wakiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru walikopelekwa 
kwa matibabu na kuangaliwa maambukizi ya magonjwa ya zinaa, watoto hao 
walidai kufanyiwa mchezo huo kwa nyakati tofauti  na wachungaji watatu 
wa kanisa hilo lililopo eneo la  Feed Force, Kwamorombo jijini Arusha.
Mmoja wa watoto hao anayesoma darasa la 4 katika shule ya msingi 
alieleza kuwa yeye na wenzake wamekuwa wakifanyiwa mchezo mchafu katika 
kanisa hilo baada ya wachungaji hao kuwapatia shilingi 2,000.
“Siku moja nilipofika shuleni wenzangu wakaniambia niende pale 
kanisani tukapewe hela, nilipofika niliwaona wenzangu wengine 
wakifanyiwa mchezo mchafu na mimi mchungaji aliniambia niiname 
akanifanyia kitendo kibaya na kunipa shilingi 2,000/- niliumia sana,’’ 
alisema mwanafunzi mmoja.
Mwanafunzi mwingine alisema amekuwa akitoroka shuleni na wenzake na kwenda kwa watumishi hao ambapo huwaingiza katika kanisa hilo na kujifanya wanawaombea baadaye huwafanyia mchezo mbaya.
Wanafunzi hao walieleza kuwa watumishi hao huwarubuni kwa kuwaeleza 
kuwa watawasaidia kuwasomesha iwapo watakuwa wakienda kwenye kanisa hilo
 na kuwaingilia.
Mzazi mmoja wa watoto hao, Julius, mkazi wa Kwamorombo alisema mtoto wake alimweleza kwamba amekuwa akifanyiwa mchezo mbaya na watumishi hao baada ya kupewa shilingi 2,000. Alisema aligundua hilo kufuatia tabia ya mtoto wake kuchelewa kurudi nyumbani.
Naye Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema 
ambaye alifika hospitalini kuwajulia hali watoto hao alisikitishwa na 
kitendo hicho na kulitaka jeshi la polisi lifanye uchunguzi wa kina kwa 
kushirikiana na vipimo vya kidaktari ili kupata ukweli wa tukio hilo.
“Nimeongea na mkuu wa mkoa, Magesa Mulongo ambaye ameahidi 
kulifuatilia kwa kina suala hili na kujua undani wake,’’ alisema Lema.

Hata hivyo, watoto hao baadaye walihamishiwa katika Hospitali ya 
Seliani kwa ajili ya vipimo zaidi huku taarifa za awali zikithibitishwa 
na daktari wa hospitali hiyo kuwa, baadhi yao walikutwa na michubuko na 
kupanuka sehemu za siri hali inayooneshwa kuingiliwa.
Chanzo:www.baabkubwamagazine.com 

