Mke wa Rais wa Marekani,Michelle Obama, 
            
Dar es Salaam. Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush na 
mkewe,Laura wanatarajiwa kuendesha Mkutano wa Kimataifa wa wake wa 
marais wa Afrika kuzungumzia nafasi ya wanawake kuinuka kimaendeleo 
utakaofanyika Dar es Salaam, Julai 1-2 mwaka huu.
                
              
Mkutano huo ambao ni wa kwanza kufanyika nchini, 
utakwenda sambamba na ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama pia 
utajumuisha maofisa wa Serikali,viongozi wa mashirika ya kiraia na 
wasomi wa kada mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa na Wakfu wa George W. Bush 
imesema kuwa mkutano huo utakaokuwa na kauli mbiu; “Kuwekeza kwa 
wanawake kunaiinua Afrika” imewataja baadhi ya wazungumzaji kuwa ni 
pamoja na Bush mwenyewe na mkewe Laura, Mke wa Rais wa Marekani,Michelle
 Obama, Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza,Cherie Blair na 
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi 
(Unaids), Michel Sidibé.
Taarifa hiyo imesema kuwa wake hao wa marais wa 
Afrika wanatoa mchango mkubwa wa kusukuma mbele agenda za maendeleo 
katika sekta za afya na elimu hivyo kukutana kwao kutatoa fursa nyingine
 ya kujadiliana changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati ya pamoja.
“Wake za marais wanalo jukumu muhimu kuhusiana na 
uboreshwaji wa ustawi wa wanawake… wao wana nafasi kubwa ya kuinua na 
kuboresha sekta kama elimu,afya na maendeleo ya kiuchumi hivyo kukutana 
kwao ni hatua muhimu itayotoa mwanga kuhusiana na hatua zinazopaswa 
kufanywa kuwawezesha wanawake,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Baadhi ya wake za marais watakaohudhuria mkutano 
huo ni wa pamoja na Mke wa Rais wa Uganda, Janet Museveni,mke wa Rais wa
 Msumbiji, Maria da Luz Dai Guebuza, mke wa Rais wa Sierra Leone, Sia 
Nyama Koroma na mwenyeji wao Salma Kikwete.
                
              
Miongoni mwa mada zinazotarajiwa kujadiliwa wakati
 wa mkutano huo ni pamoja na kuwawezesha wanawake ujasiriamali kupitia 
mafunzo ya teknolojia,kutoa fursa na kuboresha shughuli za kilimo kwa 
wakulima wanawake na ukoaji wa maisha kwa kukabiliana na saratani ya 
ziwa