Picha hii kwa hisani ya maktaba:
 Tarehe 29 Machi 2013, mnamo saa mbili na nusu asubuhi jengo 
linalojengwa kwenye kiwanja namba 2032/73 Mtaa wa Indira Gandhi 
lilianguka kutokana na sababu ambazo bado hazijathibitishwa kitaalam na 
mamlaka husika. Shirika la Nyumba la Taifa linasikitika sana kutokana na
 kuanguka kwa jengo hilo pamoja na maafa yaliyotokana na tukio hilo la 
kusikitisha. Pia Shirika linatoa pole kwa wale wote waliofikwa na msiba 
uliotokana na ajali hii.
Mradi huu wa ubia kati ya 
NHC na M/s Ladha Construction Limited ya Jijini Dar Es Salaam ulianza 
kutekelezwa tarehe 4 Februari 2008 ambapo Shirika la Nyumba litakuwa na 
hisa asilimia 25 na mbia ana asilimia 75 mara baada ya mradi kukamilika.
 Kwa mujibu wa sera ya ubia iliyoanza kutumika mwaka 1993 na kuhuishwa 
mwaka 1995 na 2005, Shirika la Nyumba la Taifa lilikuwa likitoa ardhi 
ambayo ilikuwa ikihesabika kama asilimia 25 ya mtaji wake kwenye jengo 
husika na mbia alikuwa akipata asilimia 75.
Kwa mujibu wa mkataba
 huo mbia mwendelezaji M/s Ladha Contruction Limited kama walivyo wabia 
wengine, anapaswa kabla ya kuanza ujenzi kupata vibali kutoka kwenye 
mamlaka husika na kuwa na wataalam wa ujenzi na washauri waliokubalika 
na kuthibitishwa na mamlaka husika. Aidha, mbia huyu akishapata wataalam
 hao ndiye anayehusika kuingia nao mikataba ya kazi ya kujenga na 
kusimamia ubora wa jengo husika kwa mujibu wa sheria. Katika mradi huu 
mbia mwendelezaji aliajiri wataalamu wote waliosajiliwa na Mamlaka 
husika ambazo ni CRB, ERB, AQRB na Mansipaa husika na mamlaka 
nyinginezo. Kwa kuwa ujenzi ulikuwa bado haujakamilika, Shirika lilikuwa
 bado halijapata asilimia 25 ya umiliki wake.
Pia tunapenda 
kuufahamisha Umma kuwa, Shirika la Nyumba la Taifa, lilisimamisha utoaji
 wa miradi mipya ya ubia mwaka 2010 ili kuweza kutathimini mafanikio na 
changamoto za utekelezaji wa miradi ya ubia na hivyo kuwezesha 
kutengeneza sera mpya. Kama sehemu ya zoezi hilo, shirika pia lilifuta 
jumla ya mikataba 64 ambayo ilikuwa imesainiwa lakini haijaanza ujenzi.
Katika
 sera mpya ambayo utekelezaji wake utaanza hivi karibuni Shirika 
litahusika moja kwa moja katika kuteuwa mjenzi mtaalam (contractor), 
msimamizi mtaalam wa mradi husika (consultant) na kusimamia kikamilifu 
shughuli zote za ujenzi.
Tunapenda kuufahamisha umma kuwa taarifa
 zaidi zitatolewa baada ya vyombo husika kuwasiliana na mjenzi wa mradi 
huu. Aidha, taarifa zinaweza kupatikana moja kwa moja kutoka M/s Ladha 
Construction Limited ambaye ndiye mbia mwendelezaji aliyekuwa anasimamia
 ujenzi huu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO NA HUDUMA KWA JAMII S.L.P. 2977 Simu: 2851590 DAR ES SALAAM
Telegrams : "NYUMBA" TANZANIA
Fax 2851442