![]()  | 
| Kura zikihesabiwa kwenye kituo kilichopo Viwanja vya Kibera Social, jijini Nairobi baada ya wananchi wa Kenya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo jana. | 
Matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu nchini Kenya yanaonyesha kuwa 
Uhuru Kenyatta, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta 
anaongoza, huku akifuatiwa kwa karibu na aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi 
hiyo, Raila Odinga.
Kama alivyo Uhuru, Raila pia ni mtoto wa mmoja wa 
waasisi wa taifa la Kenya, ambaye alikuwa Makamu wa Mzee Kenyatta, 
Jaramong Oginga Odinga.
Hadi majira haya ya  saa 6.45 usiku wa kuamkia 
leo,  Uhuru ambaye ni mgombea wa TNA alikuwa amepata kura 744,648 sawa 
na asilimia 56.1 wakati Raila ambaye ni mgombea wa ODM alikuwa akifuatia
 kwa kupata kura 527, 780 sawa na asilimia 39.7.
Matokeo hayo ni kutoka katika vituo zaidi ya 5000 
kati ya 31,000 na yalikuwa yakionyeshwa moja kwa moja na Tume Huru ya 
Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kadri yalivyokuwa yanaingia.
Hata hivyo Mwenyekiti wa IEBC, Isaack Hassan 
akizungumza na vyombo vya habari jana usiku alisema matokeo hayo ni ya 
awali na kwamba matokeo kamili yangetangazwa na tume yake baada ya 
kukusanya taarifa kutoka vituo vyote vya kupigia kura.
Wagombea wengine walikuwa wameachwa mbali. Hao ni 
Musalia Mudavadi, Peter Kenneth, James Kiyiapi, Martha Karua, Mohamed 
Dida na  Paul Muite.
Waliokufa wafikia 22
Wapema watu 22 wakiwamo askari polisi tisa waliripotiwa kuuwawa baada ya kuvamiwa na kikundi cha watu zaidi ya 200 huko Mombasa na Kilifi saa chache kabla ya Wakenya kuanza kupiga kura jana.
Wapema watu 22 wakiwamo askari polisi tisa waliripotiwa kuuwawa baada ya kuvamiwa na kikundi cha watu zaidi ya 200 huko Mombasa na Kilifi saa chache kabla ya Wakenya kuanza kupiga kura jana.
Saa chache kabla ya uchaguzi huo, askari polisi 
tisa waliuawa katika mashambulizi yaliyotokea kwenye miji ya Mombasa, 
Kilifi na Kwale na kuacha wavamizi wapatao 10 na raia wa kawaida watatu 
pia wakifariki.
Baada ya vifo hivyo, serikali ilipeleka vikosi vya
 askari kutoka Mariakani Barracks kwenda kutuliza ghasia hizo wakati 
kundi lingine la askari lilitoka Nyali Barracks kwa ajili ya kuweka 
doria katika miji ya Mombasa na North Coast.
Taarifa zilizopatikana baadaye jana zilisema kuwa 
kwenye mji wa Mombasa askari polisi wanne waliuawa na watu zaidi ya 100 
waliovamia kituo cha kura cha Miritini.
Polisi pia ilithibitisha kuuawa kwa watu saba katika mapigano hayo huku na wengine kadhaa kutiwa nguvuni.
Wavamizi wengine waliuawa katika miji ya Kisauni 
na Kilifi huku polisi wanne wakiuawa Chumani na mmoja huko Chonyi huku 
watu watatu wakiuawa kwa kupigwa risasi.
