![]()  | 
| Mkuu wa Usalama na Ulinzi wa Chadema, Wilfred Lwakatare | 
Mwandishi wa gazeti la Mwananchi amemshududia jana akizungumza na 
wakili wake Nyaronyo Kicheere, huku akilalamikia hali yake kuwa si njema
 kutokana na ugonjwa wa kisukari alionao.
Alikuwa akitembea kwa kujivuta, na alidai kuwa ameshindwa kula chakula inavyotakiwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, wakili 
Kicheere alisema amehangaika sana katika kuhakikisha kuwa mteja wake 
anapata dhamana lakini imeshindikana, hali ambayo inamtia hofu kutokana 
na hali aliyomwona nayo.
“Mteja wangu ni mgonjwa wa kisukari, kwa kawaida 
hutakiwa kula chakula na kunywa maji mengi, lakini nimehangaika sana, 
leo (jana) nilikuwa na matumaini kwamba atapelekwa mahakamani ambapo 
nilijipanga kwa kuandaa watu makini wenye hati za nyumba nikiwa na imani
 kwamba angepata dhamana, lakini wamemrudisha mahabusu,” alisema 
Kicheere.
Kicheere muda mwingi alionekana kuhaha kuwasiliana
 na viongozi wa Chadema kwa simu yake ya mkononi, pamoja na kuwasiliana 
na baadhi ya wanasheria akiwamo Tundu Lissu na Peter Kibatala ambao 
walijipanga katika kuhakikisha kuwa wanapata wadhamini watakaoweza 
kumdhamini Lwakatare.
Wakili huyo alisema kuwa kinachotendeka kwa mteja wake ni kinyume cha sheria kwa kuwa ni tuhuma ndizo zimemfanya akamatwe.
Alisema mteja wake ana haki ya kupewa dhamana hasa
 kwa kuzingatia kuwa saa zaidi ya 24 zimepita na hali yake si njema, na 
kwamba kuendelea kuwa mahabusu ni kuhatarisha usalama wa afya yake.
Maofisa wa juu kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa 
Upelelelezi wa Makosa ya Jinai, waliwasili Kituo Kikuu cha Polisi jijini
 Dar es Salaam ambapo walikutana na wakili Kicheere na mtuhumiwa huyo na
 kufanya mazungumzo.
Taarifa za kuaminika zilizopatikana awali 
zilieleza kuwa juzi saa 11 jioni maofisa kadhaa wa polisi, walimchukua 
mtuhumiwa huyo na kwenda naye nyumbani kwake wakiwa na lengo la kufanya 
upekuzi kwa mara ya pili lakini juhudi zao ziligonga mwamba baada ya 
kutokuwa na kibali cha upekuzi.
“Wakili wake anawabana maofisa wa polisi akitaka 
wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria hivyo juzi hawakuweza kuingia 
ndani, pia walizuiwa na wakili huyo huyo kumhoji kwa kumrekodi kwa 
video, ambapo kulitokea hali ya majibishano ya kisheria, lakini hatimaye
 akahojiwa bila kurekodiwa,” kilieleza chanzo cha habari.
Lwakatare alikamatwa Jumatano ya wiki hii katika 
makao makuu ya chama hicho na tangu siku hiyo anaendelea kushikiliwa na 
polisi kwa mahojiano.
SOURSE: MWANANCHI
SOURSE: MWANANCHI
