WAKATI Mkutano Mkuu wa Nane wa Uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UVCCM)
ukimalizika, mmoja wa wagombea wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya
chama hicho nafasi sita Tanzania Bara, Stanley Mdoe, ametiwa mbaroni na
Polisi akibainika kuwa askari Polisi.
Askari
huyo mwenye namba F 7961 wa cheo cha Konstebo, anatoka kituo cha Polisi
Mvomero, Morogoro ambaye alibainika jana akijihusisha na siasa hata
kuingia kinyang’anyiro cha kuwania ujumbe wa NEC kupitia Vijana.
Kwa
mujibu wa habari zilizopatikana Morogoro, askari huyo alijitambulisha
kwa baadhi ya wajumbe kuwa yeye ni mtoto wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,
Joel Bendera, akijiita Stanley Bendera.
Wapambe
waliofuatana naye kutoka Morogoro wakiwa Dodoma waliarifu kuwa mgombea
huyo alikamatwa juzi jioni akiwa amevalia sare za chama hicho akiomba
kura kwa wajumbe ili wamchague kwa nafasi hiyo.
Hata
hivyo, ilielezwa na baadhi ya wanachama waliofuatana naye na wengine
wanaotambua kazi yake uaskari, waliwajulisha maofisa usalama waliokuwa
eneo hilo nao kufikisha taarifa hizo Polisi na kukamatwa.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, askari huyo alikuwa ameomba likizo isiyo na malipo, wakati wengine wakidai kuwa ameacha kazi.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile akizungumzia tukio
hilo alisema alipata taarifa ya kukamatwa kwa askari huyo Dodoma na
kwamba wakati huo alikuwa akimtafuta kwa siku mbili kwa ajili ya
shughuli za kikazi bila mafanikio.
“Sina
uhakika kama askari huyu amejiingiza katika siasa ... nimetuma askari
wengine kwenda Dodoma kufanya uchunguzi wa suala hilo,” alisema Kamanda
Shilogile na kuongeza:
“Iwapo
itabainika kuwa kweli, atachukuliwa hatua stahiki na kinidhamu
kulingana na taratibu za kijeshi. Hata hivyo siwezi kuzungumzia suala la
ugombeaji wake, sijathibitisha ukweli wake, isipokuwa hakuwa kazini kwa
siku mbili na ni utovu wa nidhamu kwa Jeshi letu kutoonekana eneo la
kazi,” alisema Kamanda Shilogile.
Kwa
mujibu wa Kamanda, sheria za nchi na Katiba kuna vifungu vinavyohusu
majeshi ya ulinzi na usalama vikitamka kuzuia na kupiga marufuku
mwanajeshi kujihusisha na siasa.
Alisema
iwapo jambo hilo litabainika, litakuwa limefanyika kinyume na kanuni na
taratibu za kazi ya uaskari. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bendera,
hakupatikana ofisini kwake wala kwa njia ya simu ya mkononi ili
kufafanua kadhia hiyo.
Hata hivyo wasaidizi wake walidai kuwa yuko nje ya nchi kwa shughuli za kikazi.