Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Prof. Haruna Lipumba  
Chama Cha
 Wananchi (CUF) kimewasimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama 
hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa 
Bara, Magdalena Sakaya.
Uamuzi 
huo umetolewa jana na Baraza Kuu la Chama hicho lililofanya mkutano wake
 visiwani Zanzibar kwa lengo la kuwajadili wanachama kadhaa wakiwemo 
vigogo hao. Sakaya amevuliwa nyadhifa zote ndani ya chama kabla ya 
kusimamishwa.
Taarifa 
kutoka ndani ya Mkutano huo zimeeleza kuwa Baraza hilo limewaadhibu 
wanachama 15 wakiwemo Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliua.
Mbali na 
vigogo hao, wengine waliopigwa rungu na Baraza Kuu la CUF ni pamoja na 
Katibu wa Baraza la Wazee, Shashi Lugeye, Thomas Malima na Naibu 
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano, Abdul Kambaya.
Aidha, 
Baraza hilo limemsimamisha uanachama Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah 
Nachuma. Hatua hii inaweka matatani ubunge wa Sakaya na Nachuma kwani 
wakifikia hatua ya kufukuzwa watakosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.
Lipumba 
na Sakaya hawakupata nafasi ya kujitetea kutokana na kutohudhuria 
mkutano huo wakati Shashi alipata nafasi ya kujitetea kutokana na uwepo 
wake lakini utetezi wake haukuzaa matunda. Katiba ya chama hicho haiwapi
 nafasi wabunge hao kukata rufaa kutokana na uamuzi wa Baraza hilo.
Uamuzi 
huo umekuja ikiwa ni siku chacha baada ya Mkutano Mkuu Maalum wa Chama 
hicho uliolenga kumchagua Mwenyekiti Mpya kuvunjika kutokana na kuwepo 
vurugu kubwa baada ya Profesa Lipumba kuingia ndani ya ukumbi huo na 
wafuasi wake wakitaka barua yake ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake 
ijadiliwe na kukubaliwa.
