Kocha Msaidizi wa timu ya Yanga Boniface Mkwasa akitoa maelekezo kwenye mazoezi ya timu ya Yanga hivi karibuni  
YANGA imeuanza mwaka 2014 kwa kasi ya aina yake ambapo makocha 
wazungu wenye hadhi zao wanahenya usiku na mchana wakisubiri simu za 
viongozi tayari kuitwa kazini kuanza kibarua kipya.
Lakini Abdallah Binkleb ambaye ni Mwenyekiti wa 
Kamati ya Mashindano na Usajili wa Wachezaji, ameithibitishia Mwanaspoti
 kwamba kabla ya Jumatano ijayo lazima watakuwa wamemchagua mzungu mmoja
 wa maana.
Binkleb alisema: “Wapo wengi sana kila siku 
wanatuma maombi lakini sisi tunataka kocha mmoja tu wa maana ambaye ni 
fundi na anayeweza kutufanyia kitu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na 
analijua soka la Afrika.
“Tumemchukua Mkwasa (Boniface, anayekuwa Kocha 
Msaidizi) ni kocha wa maana pamoja na Juma Pondamali (Kocha wa Makipa) 
wanaijua Yanga vilivyo, tuna uhakika kwamba tukishakutana tukipitia 
orodha ya mwisho na kuchagua wa kutua nchini, tusifanye makosa.”
Hata hivyo kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa 
ndani ya Yanga hakuwa na idadi kamili ya makocha walioomba kazi hiyo 
inayoachwa wazi na Ernest Brandts ambaye amepewa notisi.
Bin Kleb alisema hawezi kusema idadi kwa sasa kwa vile wamekuwa wakipokea barua pepe za maombi hayo kila baada ya muda mfupi.
MKWASA AANZA KWA MIKWARA 
Boniface Mkwasa ameiangalia timu hiyo na kutamka 
kuwa wachezaji wake hawana uwezo wa kucheza dakika 90, hivyo ataanza 
mazoezi ya aina nne kuwandaa kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu 
Tanzania Bara.
Mkwasa ametoa kauli hiyo mara baada ya mazoezi ya 
siku ya kwanza kumalizika jana Ijumaa baada ya kusaini mkataba wa miaka 
miwili kuifundisha timu hiyo akirithi mikoba ya Fred Minziro aliyekuwa 
msaidizi wa Brandts.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkwasa alisema kuwa 
timu hiyo inahitaji mabadiliko ya haraka katika kujiandaa na mzunguko wa
 pili wa ligi kutokana upungufu aliouona ambao ni;
Moja; Pumzi. Hilo ndilo la kwanza linalohitajika 
ambalo ameliona kwa wachezaji kushindwa kumudu kucheza dakika 90 jambo 
ambalo ni baya kwa timu inayojiandaa na michuano ya kimataifa.
Katika kuhakikisha analifanyia kazi hilo, tayari 
ameuomba uongozi kutafuta uwanja mkubwa kushinda ule wanaoutumia hivi 
sasa wa Bora uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Wanahamishia 
mazoezi yao Uwanja wa Tanganyika Packers ambao una eneo kubwa kwa lengo 
la kuwaongezea pumzi wachezaji hao.
                
              
                
              
                
              
                
              
                
              
                
              
                
              
                
              
                
              
Pili; Kasi. Ameona timu hiyo inacheza soka la taratibu ambalo 
yeye halitaki, anataka kuona timu inacheza kwa kasi ili kuwachosha 
wapinzani wao ndani ya uwanja.
Tatu; Pasi. Nalo ni tatizo kwani anasema wachezaji
 wanapiga pasi hovyo. Anasema ili timu icheze soka safi, lazima wapige 
pasi zitakazowafikia wenzao ndani ya uwanja na siyo kuwapelekea adui na 
kuanza kupata tabu ya kukaba.
Nne; Kumiliki mipira. Hilo nalo ni tatizo ingawa 
amesema ni karibu kwa timu zote zinazoshiriki ligi, hivyo amepanga 
kulimaliza tatizo hilo kwa Yanga.
“Ninajua ni ngumu kumaliza matatizo hayo katika 
muda huu mfupi wakati timu inajiandaa na ligi, lakini ninaamini 
nitalipunguza, jambo kubwa nahitaji ushirikiano kutoka kwa wachezaji, 
ninaomba viongozi kuhakikisha wanasimamia nidhamu ya wachezaji, pale 
wanaomba ruhusa na kupewa basi warudi kwa wakati,” alisema.
MAZOEZI MARA MBILI 
Mkwasa amebadilisha muda wa mazoezi ambapo kuanzia
 keshokutwa Jumatatu yatakuwa yakifanyika jioni tu na kadiri siku 
zinavyokwenda mazoezi ya timu hiyo yatakuwa yakifanyika mara mbili kwa 
siku yaani asubuhi na jioni.
Mkwasa alikaa kikao kirefu na wachezaji juzi 
Alhamisi jioni klabuni na aliiambia Mwanaspoti kuwa kikao hicho kilikuwa
 kwa ajili ya kuwafahamu wachezaji kabla ya kuanza kazi rasmi jana 
Ijumaa.
“Lengo langu lilikuwa kufahamiana na kupanga 
mikakati, mimi si mgeni Yanga, naamini ushirikiano kutoka kwa wachezaji 
na viongozi utasaidia timu kupata mafanikio kwenye Ligi Kuu na michuano 
ya kimataifa,” alisema Mkwasa.
Habari za ndani zinasema Yanga itasafiri kwenda 
nchi mojawapo kati Hispania, Uturuki au Ureno na inadaiwa timu inatakiwa
 kuondoka kati ya Januari 9 na 10.