TAMKO LA CHADEMA KUHUSU NJAMA ZA 
KUKICHAFUA ZINAZOFANYWA NA GENGE LA VIONGOZI WAKUU WA CCM NA VYOMBO VYA 
DOLA, LIMETOLEWA JIJINI DAR ES SALAAM LEO, MACHI 14, 2013 NA MJUMBE WA 
KAMATI KUU NA MWANASHERIA WA CHAMA, MH. MABERE NYAUCHO MARANDO
Ndugu waandishi wa habari;
LEO
 tumewaita hapa ili kuwaomba mtufikishie ujumbe kwa Watanzania, kwamba 
nikiwa mwanasheria na mtu ambaye nimepata ujuzi wa kazi za ushushu, 
nimefanya uchunguzi matukio haya ya utekaji na utesaji na kugundua mambo
 mengi mno.
Uchunguzi huu nimeufanya kabla na baada ya kukamatwa 
kwa Mkurugenzi wetu wa Ulinzi na Usalama, Willifred Muganyizi Lwakatare,
 ambaye hivi sasa anashitakiwa mahakamani kwa tuhuma za kupanga ugaidi.
Nimefanya
 hivyo kwa kuangalia maslahi mapana ya taifa langu na chama changu. 
Katika uchunguzi wangu huo, nimegundua mambo mengi ikiwamo kuwapo kwa 
genge la watu ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaopanga
 mipango hii ya kishetani na kisha kuwasingizia watu wengine.
Angalieni
 mfano huu: Unaoitwa na polisi na Mwigulu Nchemba, “mkanda wa Lwakatare”
 unadaiwa uliwasilishwa jeshi la polisi Desemba mwaka jana. Lakini jeshi
 hilo halikumkamata yoyote wala kumhoji, hadi pale Mwenyekiti wa 
Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, alipovamiwa na kuumizwa.
Aidha,
 Nchemba amedai kumiliki video ile Desemba mwaka jana, lakini rekodi 
hiyo iliwekwa kwenye mitandao ya kijamii (YouTube na Jamii Forum) baada 
ya kutekwa kwa Kibanda. Hapa mtu makini anaweza kujiuliza, hiki 
kimelenga nini?
Kwamba genge hili la kina Nchemba na wenzake, 
walipanga kumteka Kibanda, wakatimiza lengo lao hilo, baadaye wakaingia 
kwenye plani B ya kutaka kuihusisha Chadema. Wakamtumia Ludovick Joseph 
Rwezahula ambaye ni 
  
mshitakiwa wa pili katika kesi ya Lwakatare, kufanikisha mkakati wao huu wa kishetani.
Ndugu waandishi wa habari;
Huu
 ni mchezo mchafu na wahatari mno ambao kwa vyovyote vile, haupaswi 
kuvumiliwa. Kuanzia sasa nimeamua kwa dhati kabisa, kukomesha mchezo huu
 ambao unahatarisha uhai wa taifa letu.
Kwa kuanzia, kesho 
Jumatatu, nitaongoza jopo la mawakili sita wa Chadema kumtetea Bw. 
Lwakatare. Wenzangu wengine katika kesi hii, ni Profesa Abdallah Safari,
 Tundu Lissu, Edson Mbogoro, Peter Kibatara na Nyaronyo Kicheere. Huko 
mbele tutaongeza mawakili wengine, akiwamo mmoja anayewekwa na familia 
ya Lwakatare.
Ndugu waandishi wa habari;
Mnaweza kujiuliza, 
kwa nini Chadema kimechukua uamuzi huu wa kuweka kundi 
kubwa la wanasheria katika kesi hii ya Lwakatare? Jibu ni kwamba 
tumegundua kuwa kesi hii imefunguliwa kwa lengo 
maalum lakuidhoofisha Chadema na kuinusuru CCM ambayo inakabiliwa na 
dhahama ya kushindwa katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na kushamiri kwa
 makundi.
Hivyo wameamfungulia kesi Lwakatare, kwa 
lengo la kutaka kuaminisha umma kuwa Chadema ni chama cha magaidi, 
kinapanga ugaidi na hivyo kichukiwe. Hilo ndilo lengo lao. Basi!
Ndugu waandishi wa habari;
Pili,
 nitakwenda mahakamani kuwasilisha ombi maalum la kuomba amri ya 
mahakama kuagiza makampuni ya simu za mkononi kuwasilisha mahakamani 
statement za simu za watu kumi (10) ili kusaidia mahakama kutenda haki 
na jamii kujua ukweli wa mambo haya.
Watu ambao nitaomba mahakama itoe amri ya kuletwa taarifa zao simu
na
 meseji (sms) ni Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini (TISS), 
Jack Zoka, anayetumia simu Na. 255756xxxxx, Naibu Katibu Mkuu wa Chama 
Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Lameck Nchemba, anayetumia simu tano 
zikiwamo 0754 xxxxx, 0757 xxxxx, 0714 xxxxx na 0787 xxxxx na Ludovick 
Joseph Rwezahula, ambaye simu zake ni, 0715 xxxxx na 0753 xxxxx.
Mwingine
 ambaye mawasiliano yake yanahitajika, ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya 
Nchi, Emmanuel Nchimbi, anayetumia simu Na. 0754 xxxxx, Mhariri Mtendaji
 wa magazeti ya Mwananchi, Dennis Msaky anayetumia simu mbili, 0655 
xxxxx na 0764 xxxxx na Bw. Sinbad Mwagha, ambaye ni afisa wa idara ya 
usalama wa taifa, anayetumia simu 0754 xxxx.
Wengine, ni Bw. 
Shaali Ali, afisa mwinge wa usalama wa taifa anayetumia simu Na. 
0716xxxxx, Saumu K. Malungu, mwenye kutumia simu 0719 xxxxx na 0789 
xxxxx, simu mbili zinazotumiwa na mtuhumiwa mkuu wa utekaji wa Dk. 
Steven Ulimboka, Bw. Ramadhani Abeid Igondo ikiwamo 0713 xxxxx, simu za 
Bw. Ridhiwani Kikwete ambazo ni 0754 xxxxx, 0784 xxxxx, simu ya Dr. 
Steven Ulimboka, ambayo ni 0713 xxxxx, pamoja na simu zote tatu za 
Willifred Lwakatare, ambazo ni 0786 xxxxx, 0713 xxxxx na 0758 xxxxx.
Ndugu waandishi wa habari;
Mtu
 mwingine muhimu nitakayeomba mahakama itoe amri ya kutolewa kwa taarifa
 zake, ni mwandishi wa habari na mpigapicha wa magazeti ya serikali, 
Muhidini Issa Michuzi. Mwandani huyu wa Ikulu, ndiye aliyeandika ujumbe 
kwa njia ya emeili kuipongeza ofisi binafsi ya rais (OBR) na usalama wa 
taifa kwa kupata video ya Lwakatare.
Pongezi za Michuzi kwa TISS
 ndizo zinanisukuma kuiomba mahakama kuagiza kupatikana taarifa zake. 
Michuzi anaipongeza TISS kwa kuibua njama za wahalifu, lakini mimi 
ninajua TISS ikipata njama za aina hiyo haraka inapeleka ushahidi 
polisi, lakini huu wa Lwakatare ulipelekwa Youtube, badala ya kwenye 
vyombo vya sheria.
Maneno ya Michuzi kwamba ni TISS imeibua hiyo 
video yanathibitisha ushiriki wa TISS kwenye mchezo huo mchafu, na 
kwamba Chadema kinajua kuwa Michuzi alishirikiana na watu wa usalama wa 
taifa katika kazi hiyo chafu. Software za video (editing) walizotumia 
zilitoka kwake. Fedha ya kuandaa hiyo video zilitoka usalama na Ikulu. 
Tunajua kuwa wale vijana wa Ada Estate na yule jamaa anayempelekea 
kigogo wa Jamii Forum, walilalamika sana kwa mmoja wa wamiliki wa JF.
Ndugu waandishi wa habari;
Chadema kinajua
 kuwa mmoja wa watuhumiwa hawa, Mwigulu Nchemba anafanya mipango na 
baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Vodacom ili kumsaidia kufuta taarifa
 zake. Nachukua nafasi hii, kuionya kampuni hiyo kuacha kucheza mchezo 
huo kwa kuwa ni kinyume cha sheria za mamlaka ya mawasiliano (TCRA).
Tunahitaji
 mawasiliano haya kwa kuwa Mwigulu – zinaonyesha mtuhumiwa huyo akifanya
 mawasiliano mfululizo na Ludovick, yakiwamo yale ya tarehe 4 Machi 
2013. Hii ilikuwa siku moja kabla ya Kibanda kutekwa.
Ndugu waandishi wa habari;
Hawa
 niliowataja ni watu muhimu sana katika upangaji wa mkakati wa 
utengenezaji wa video ya Lwakatare na vitendo vya kihalifu vya utekwaji 
wa Kibanda na tukio la kutekwa na kisha kutupwa msutuni kwa mwenyekiti 
wa Jumuiya ya madaktari nchini, Dr. Steven Ulimboka.
Kwa mfano, 
simu ya Mwigullu Nchemba, namba 0714 xxxxx, 0756 xxxxx na 0757 xxxxx, 
zimefanya mawasiliano mara kadhaa na Ludovick Joseph, Saumu K. Malungu, 
Jack Zoka, Ali Shaali na Ramadhani Ighondo. Mawasiliano hayo yalifanyika
 katika kipindi ambacho mgomo wa madaktari ulishamiri; baadaye yakarudi 
tena kati ya 26 Desemba mwaka jana na 15 Machi mwaka huu.
Miongoni
 mwa mawasiliano ambayo tunaona yanahusika na ujambazi huu, ni yale ya 
28 Desemba, siku ambayo mkanda wa Lwakatare umerekodiwa; tarehe 4 hadi 6
 Machi 2013, siku moja kabla ya Kibanda kutekwa na yale ya usiku wa 
manane (saa 8:17) wa 13 Machi 2013, ambako mchana uliofuata Lwakatare 
alikamatwa.
Huyu Mwagha ndiye aliyekuwa anatumika kuwasiliana na
 Saumu Malungu, ambaye tulimtaja kuwa ndiye aliyekuwa amepewa kazi na 
Mwigulu na usalama wa taifa, kurubuni vijana wetu kwa fedha ili kutoa 
ushahidi wa uongo juu ya video ya Lwakatare.
Vilevile, 
mawasiliano ya Mwiguluna Mwagha, katika kipindi hicho nayo tunayahitaji.
 Kwa sababu, huyu Mwagha anayetumia simu 0754xxxxx, mbali na kuwasiliana
 na Mwigulu, ndiye aliyekuwa anawasiliana na mmoja wa waliomteka 
Ulimboka; na ndiye aliyewasiliana na Saumu kati ya 20Januari na Machi 6 
mwaka huu.
Ndugu waandishi wa habari;
Ludovick alifanya 
mawasiliano ya mwisho na Joyece Agustine, ambaye anatumia simu Na. 0717 
xxxxx, mawasiliano ambayo yalifanyika saa 5:13 usiku. Hiyo ndiyo ilikuwa
 simu yake ya mwisho usiku huo; katika siku hiyo Ludovick aliwasilisna 
na Joyce mara tisa kuanzia saa 12: 54 asubuhi.
Kwa mujibu wa 
taarifa za kwenye mtandao wa Jamii Forum, ambako video ya Lwakatare 
ilitumwa, Ludovick alikamatwa Machi 15 mwaka huu. Hata hivyo, rekodi 
katika simu yake Na. 0715 xxxxx inaoyesha 17 Machi Ludovick alifanya 
mawasiliano na Joyce Augustino. Mawasiliano hayo yalifanyika saa 8: 9 
usiku, wakati inadaiwa na polisi alishakamatwa.
Naye mhariri wa 
Mwananchi, Bw. Msaky ambaye anatajwa kutaka kutekwa na Ludovick na 
Lwakatare, amekuwa na mawasiliano kadhaa na Ludovick – mtu anayepanga 
kumteka. Ludovick na Msaky walifanya mawasiliano mfululizo kati 27 
Desema 2012, siku moja kabla ya video ya Lwakatare haijarekodiwa na 7 
Machi siku moja baada ya Kibanda kutekwa.
Msacky alitumia simu 
zake hizo mbili (0764 xxxxx na 0655 xxxxx) kuwasiliana na Ludovick, huku
 Ludovick akitumia 0753xxxxx. Mawasiliano ya 31 Desemba yalifanyika 
Ludovick akiwa Tegeta, jijini Dar es Salaam. Mawakala hawa wawili wa 
usalama wa taifa (Ludovick na Msaky), walikutana 31 Desemba 2012, katika
 hoteli ya Tamal, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Ndugu waandishi wa habari;
Baada
 ya kupitia taarifa hizi za mawasiliano ya simu za Mwigulu Nchemba, 
Ludovick Joseph, Ramadhani Ighondo na Saumu Malungu tumegundua 
yafuatayo: Kwamba, Ramadhani Ighondo, amefanya mawasiliano mara nyingi 
na Mwigulu, Mwagha na Zoka; naye Mwagha amefanya mawasiliano na Mwigulu 
na Saumu; naye Saumu amefanya mawasiliano na Mwagha, Mwiguluna Shaali 
Ali, ambaye ni afisa usalama wa taifa.
Tumegundua vilevile, 
kuwapo mawasiliano kadhaa kati ya Ludovick na Msaky; Ludovick na 
Mwigulu; Msaky na Nchimbi; Msaki na Mwagha, Samu na Mwagha na Ramadhani 
Ighondo Abeid, anayetuhumiwa kumteka Dk. Ulimboka na Mwanga na Mwigullu.
Tumegundua
 pia kuwapo mawasiliano kati ya Ulimboka na Ramadhani; Zoka na Ighondo 
na Ridhiwani na Ighondo. Mawasiliano haya yalifanywa mfululizo usiku wa 
Juni 2012 siku ambayo Dk. Ulimboka alitekwa.
Tumepata kufahamu 
pia kwamba baadhi ya watu waliotajwa na gazeti la MwanaHALISI kuwa 
waliwasiliana na Ighondo usiku wa Juni 26, mwaka 2012, wamefanya 
mawasiliano pia na Mwigulu, Mwagha na Shaali Ali.
Ndugu waandishi wa habari;
Mwagha
 ni afisa usalama wa taifa anayefanyakazi makao makuu ya idara hiyo. 
Ndiye yule anayetumika kuendesha michezo ya kuhonga wanasiasa wa CCM na 
upinzani. Ni Mwagha anayepanga wabunge na kuwapanga waongee nini kwa 
maslahi ya CCM. Ushenzi wote anaoongea Mwighulu bungeni, hupewa na 
Mwagha kwa maelekezo ya Jack Zoka.
Naye Shaali ndiye aliyekutana 
na afisa wetu wa usalama, Ahmed Sabula na mwenzake, Machi 29 mwaka huu 
katika hoteli ya See Cliff jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo kati
 ya Sabula, kijana wetu wa usalama na afisa usalama wa serikali Bw. 
Shaali alitaka Sabula akubali kutumika kwa kutoa taarifa za vikao vya 
chama, kuwasilisha kwake nyaraka za kamati kuu na kueleza mipango ya 
chama katika kesi ya Lwakatare.
Kwenye mpango huu, afisa huyo wa
 usalama wa taifa ambaye ninamfahamu vizuri, alimuahidi Sabula kiasi cha
 Sh. milioni 30 na kwamba fedha hizo angelipwa wiki iliyopita. 
Aliahidiwa pia kwamba kila nyaraka atakayopeleka atalipwa ujira.
Aidha,
 Sabula aliahidiwa kulipwa shilingi 500,000 (laki tano) kila mwezi; 
afisa wetu huyu ameripoti tukio hilo kwa viongozi wake wa chama. Yule 
mwenzake aliandaliwa kuwa shahidi wa kesi ya Lwakatare; aliambiwa 
akikubali dili hiyo atalipwa kila mwezi Sh. 500, lakini akaombwa kuwa 
mvumilivu kwa kuwa atalazimika kupotea kwa miezi kama mitano hadi sita.
Ndugu waandishi wa habari;
Kitendo
 cha Mwigulu kuwasiliana Ramadhani Ighondo, Mwigulu kuwasiliana na 
Ludovick, Saumu kuwasiliana na Mwigulu, Ighondo kuwasiliana na Ulimboka,
 Zoka kuwasiliana na Ighondo, tena katika muda uleule ambao Ighondo 
amewasiliana na Ulimboka na Saumu kuwasiliana na Mwagha, ni uthibitisho 
tosha kwamba usalama wa taifa wako nyuma ya mipango hii ya michafu ya 
kupanga utekaji na kisha kutaka kukichafua Chadema.
Aidha, 
kitendo cha Ludovick kuwasiliana Msaky; Ighondo kuwasiliana na Mwagha, 
Ridhiwani Kikwete kuwasiliana na Ighondo, tena kila baada ya Ighondo 
kuwasiliana na Ulimboka na Jack Zoka, ni uthibitisho mwingine kuwa genge
 hili la wahalifu linashirkiana na baadhi ya watu kutaka kuangamiza 
taifa.
Ni uthibitisho tosha kwamba hawa ndiyo wanaowahonga 
wanachama wa Chadema na watu wengine ili watoe ushahidi feki dhidi ya 
Lwakatare, na kwamba ni usalama wa taifa walioandaa ile video uchwara 
inayopigiwa chapuo na Mwigulu.
Ndugu waandishi wa habari;
Chama
 Cha Mapinduzi kinajua kwa hali ya sasa hakiwezi kushinda uchaguzi wa 
mwaka 2015 huku Chademaikiwa katika hali nzuri ya kisiasa tunayoiona 
sasa. Wanajua kabisa CCM imegawanyika, kundi lolote litakalopita ndani 
ya CCM, litahujumu kundi jingine. Ni kama ilivyotokea uchaguzi mdogo wa 
Arumeru Mashariki.
Ndiyo maana wanapanga kila mbinu kutaka 
kuiangamiza Chadema. Nasi tunasema katu hatutakubali 
kuonaChadema kinakufa. Tutapambana usiku na mchana. Juna na mvua. Hadi 
tushinde hila hizi.Tunawaambia wanachama wetu na wale wanaotuunga 
mkono, Chadema ni chama kikubwa. Kina mtandao kila mahali, kuanzia Ikulu
 hadi polisi; na hivyo hakitakufa au kuzorota kwa mambo ya kupikwa.
Ni
 imani yangu kwamba amri ya mahakama itawafichua wote hawa ni kuirudisha
 Tanzania katika amani yake. Ni lazima tufikike mahala watu hawa 
wafahamike mbele ya umma, tunataka wafahamu kuwa maisha ya mwanadamu 
yana thamani kuliko siasa chafu na ufisadi wanaouendeleza.
Nawashukuru kwa kunisikiliza.
Mabere Marando,
Dar es Salaam