Ndugu zangu,
Kwanza kabisa niwashukuru kwa dhati kabisa nyote 
mlionitumia salaam za kunifariji kwa njia za simu, email, facebook, 
majukwaa ya Mabadiliko, Wanabidii na JF.   
Nimefarijika sana kutambua kuwa kuna wengi wenye kunifuatilia na kunijali.
Ndugu zangu,
Kama
 alivyowataarifu kaka yangu Nyaroonyo Kichehere, ni kuwa, jana Jumamosi 
nilikuwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kuanzia saa tano asubuhi ya jana
 mpaka saa tatu usiku. Ilihusu mahojiano ya Polisi na mimi kuhusiana na 
sakata la ndugu yetu Absalom Kibanda.
Ukweli sikukamatwa mahali 
popote, bali niliitwa na Kamishna (Upelelezi) Advocate Nyombi. Alhamisi 
nikiwa Iringa, tukakubaliana na kiungwana na Kamishna Nyombi kuwa nifike
 Makao Makuu hayo ya polisi Jumamosi saa tano. Ikawa hivyo.
Hapo 
nilipokelewa na Kamishna Nyombi. Baada ya mazungumzo mafupi ndipo 
akawaita maofisa wengine watano wa Upepelezi kufanya mahojiano nami. 
Niliomba niwe na Mwanasheria, nikakubaliwa.
Nilimpigia
 simu kaka yangu Nyaroonyo, naye, kwa vile ni Wakili pia wa Kibanda 
akanisaidia kuhakikisha napata wakili mwingine. Pamoja na kuwa ilikuwa 
ni Jumamosi, ndugu yangu Nyaroonyo Kichehere alifanya alivyoweza. Ndani 
ya dakika 40 hivi alifika chumba no 704 ghorofa ya saba akiwa na Wakili 
Jacquiline Rweyongeza na Legal Officer Dickson Mbonde.
Nilimshukuru Kaka Nyaroonyo Kichehere. Na nilimuaga kwa kumwambia; “ Nenda ukaifahamishe jamii juu ya hiki kilichonitokea”.
Nachukua
 fursa hii pia kuwashukuru kwa dhati kabisa dada yangu Wakili Jacquiline
 Rweyongeza na kaka Dickson Mbonde kwa kuacha yote ya Jumamosi na kuwa 
tayari kuwa msaada kwangu. Jacquiline alimuacha nyumbani mtoto wake wa 
miezi minne kwa ajili ya suala langu. Sina namna nyingine ya kumshukuru.
 Na hakika, msaada wao niliuhitaji sana.
Nawashukuru pia kwa 
dhati kabisa, ndugu zangu Saed Kubenea, Mbaraka Islam na wengine wote 
waliokuwa na utayari wa kunisaidia pale msaada wao ulipohitajika.
Kwa
 ufupi, nimetoa maelezo yangu bila shuruti wala kutishwa. Na nimeweka 
wazi kuwa yanaweza kutumika Mahakamani kama yatahitajika au hata kama 
mimi nitahitajika, kwa namna yeyote ile.
Kesho saa mbili asubuhi nitaripoti Makao Makuu ya Polisi kupewa maelezo ya kitakachofuatia.
Kwa mara nyingine tena, nawashukuru sana kwa kuwa nami katika muda wote huu.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam