
Zitto Kabwe
Napenda kuujulisha umma kwamba tarehe tarehe 4 Oktoba, 2013 niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada 
binafsi Bungeni kufuta Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.Changamoto iliyopo ni Sheria mbadala ya vyombo vya habari baada ya Sheria ya sasa kufutwa. Hata hivyo wadau wa habari kama Baraza la Habari Tanzania wameshafanyia kazi suala hili kwa muda mrefu sana na wana mawazo kuhusu sheria mbadala.
 Nimejulishwa 
kuwa muswada wa sheria mpya ya habari tayari upo. Kwa hiyo katika 
mchakato wa kujadili muswada binafsi wa kufuta sheria ya magazeti ya 
mwaka 1976 mabadiliko yanaweza kufanywa ili kutunga sheria mpya. Hatua 
ya kwanza ni kuifuta sheria hii kandamizi ambayo kiukweli tumechukua 
muda mrefu sana na baada ya madhara makubwa kufikia hatua ya muswada wa 
kuifuta.
            
Nimeamua kutumia njia za kawaida za 
kuwasilisha muswada na kuepuka njia ya dharura ili kujenga mazingira ya 
wadau wa habari kushiriki vya kutosha katika mabadiliko yanayotakiwa. 
 Njia ya dharura ni ya haraka lakini huziba fursa za kupata maoni ya 
wadau ambao kimsingi ndio wenye sheria yenyewe haswa. Hivyo nimepeleka 
muswada leo ili uchapwe kwenye gazeti la Serikali (GN) kwa mujibu wa 
kanuni za Bunge, kisha usomwe kwa mara ya kwanza, uende kwa wadau kwa 
mjadala na marekebisho na kisha kusomwa kwa mara ya pili na kupitishwa 
na Bunge.
Ikumbukwe kuwa juhudi za kufuta sheria hii ni juhudi za wadau wa tasnia ya habari na ni juhudi walizofanya kwa muda mrefu sana. Mimi kama Mbunge ninawasilisha tu kwa sababu taratibu zetu za kuandika sheria zinataka ama Serikali, Kamati ya Bunge au Mbunge kuwasilisha muswada.
 Kwa muda mrefu tumewaangusha wana habari kwa 
kutosukuma vya kutosha mabadiliko waliyokuwa wanayapigania. Hata hivyo, 
kuna msemo wa kihindi 'asubuhi huanza pale unapoamka'. Sasa tuchukue 
hatua za kufuta sheria hii kandamizi.
Zitto Kabwe,Mb
Kigoma Kaskazini
Zitto Kabwe,Mb
Kigoma Kaskazini