![]()  | 
| Sheikh Azzan Khalid Hamdani | 
Wizara ya Afya Zanzibar imeruhusu mshtakiwa wa nne, Kiongozi Mwandamizi 
wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (Jumiki), Sheikh Azzan 
Khalid Hamdani (56), kupelekwa nje kutibiwa baada ya kukosekana tiba ya 
maradhi yanayomsumbua visiwani hapa. 
Sheikh Azzan alilazwa Hospitali ya Rufani ya Mnazi Mmoja kuanzia 
Septemba Mosi, mwaka huu baada ya kupoteza nguvu akiwa Gereza la Kiinua 
Miguu na imebainika anasumbuliwa na vijiwe kwenye figo.
Kuruhusiwa kwa Sheikh Azzan kupata tiba nje, kumethibitishwa na wakili 
wake, Salum Towfiq mbele ya Naibu Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar, 
Yesaya Kayange.
Wakili Towfiq alisema mteja wake hali yake siyo nzuri, amepata barua ya 
Wizara ya Afya Zanzibar kwamba maradhi yanayomsumbua hayatibiki Zanzibar
 na kutaka mwongozo.
Licha ya ombi hilo, Wakili Tawfiq aliwasilisha malalamiko kuwa wateja 
wake wananyanyaswa, ikiwamo kutopata nafasi ya kuwasiliana na familia 
zao kupitia simu na wanapokuwa kwenye mazingira ya Mahakama.
Alidai Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza) kimewawekea utaratibu wa 
kukutana na familia zao mara mbili kwa mwezi, huku akiomba Mahakama itoe
 mwongozo.
Pia, alidai hata wanafamilia wanapotaka kwenda mahakamani kusikiliza 
mwenendo wa kesi hukumbana na misukosuko na kushindwa kuingia ukumbini 
kutokana na kuimarishwa ulinzi na kuzuia njia za kuingia na kutoka.
Hata hivyo, Kayange alisema ombi la kwanza la matibabu ya mshtakiwa liko
 nje ya uwezo wake  na kutaka liwasilishwe Mahakama Kuu. Pia, katika 
ombi la pili alikitaka Chuo cha Mafunzo Zanzibar kuwatendea haki 
washtakiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria. Kayange aliahirisha kesi 
hiyo hadi Oktoba 7.
CHANZO:http://tinyurl.com/orpyhbf
