| Msikiti wa Ijumaa wa mjini Kyela ambao Shekhe wa msikiti huo alivamiwa na kupigwa wakati wa swala ya Idd leo asubuhi | 
WAUMINI
 wa dini ya Kiislamu waliokuwa katika ibada ya Swala ya Idd El Fitri 
katika msikiti mkuu wa Ijumaa uliopo Wilayani Kyela mkoani Mbeya jana 
walikumbwa na taharuki baada ya Shekhe wao aliyekuwa akiongoza ibada 
kuvamiwa kibla wakati akiendesha ibada na kujeruhiwa.
Tukio
 hilo la aina yake limetokea majira ya asubuhi ambapo Shekhe huyo 
aliyetambuliwa kwa jina la Nuhu Mwafilango alishambuliwa akiwa katikati 
ya sijida baada ya mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni mwanafunzi wa shule ya 
sekondari ya kutwa Kyela Ally Mwangosi kumpiga Shekhe huyo na kitu 
chenye ncha kali kichwani.
Taarifa
 kutoka msikitini hapo zinadai kuwa mara baada ya mwanafunzi huyo kupita
 upande wa Kibla na shekhe huyo na kupigwa chenye ncha kali alipiga 
ukelele wa kuomba msaada na hivyo kuibua taharuki miongoni wa waumini 
waliokuwa wakiswali msikitini hapo. KUSOMA STORI HII KWA MAREFU  BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI»
Mwenyekiti
 wa Baraza Kuu la Waislamu Wilayani Kyela Bw. Daudi Mwenda alisema kuwa 
mara baada ya Shekhe huyo kuvamiwa na kupigwa waumini walimuokoa na 
kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Bw.
 Mwenda alisema kuwa Shekhe huyo ameumizwa vibaya eneo la kichwani 
ambapo damu nyingi zilivuja mara baada ya kupigwa na kwamba mbali na 
Shekhe huyo waumini wengine wawili waliokuwa wakijaribu kumuokoa 
walijeruhiwa kwa kuchomwa na visu.
Wengine
 waliojeruhiwa katika tukio hilo ni pamoja na mweka hazina wa BAKWATA 
wilaya Ustadhi Khamis Husein aliyejeruhiwa kichwani na sikioni.
Baadhi
 ya waumini waliokuwepo katika ibada hiyo walisema kuwa tukio hilo 
lilitokea wakati waumini wote wakiwa wamesujudu ndipo waliposikia kelele
 na vurugu ambapo aliinuka mtu mmoja aliyekuwa na kitu mfano wa nondo na
 kumpiga nayo Shekhe kichwani.
Mmoja wa waumini aliyejitambulisha kwa jina la Idd Husein alisema kuwa wakati kijana huyo aliyekuwa na kitu kinachofanana na nondo liliibuka kundi la watu wengine waliomsaidia na hivyo kuibuka vurugu kubwa iliyosababisha ibada ya swala ya Idd kuvunjika.
Akizungumzia
 tukio hilo Katibu wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Shekhe Juma Killah alisema 
kuwa vurugu hizo zimetokea katika swala ya Idd na wahusika wa vurugu 
hizo ni waislamu ambao wanaipinga BAKWATA.
 ‘’Hiki
 ni kikundi cha waislamu waliotoka Jijini Dar es salaam kimekuja huku na
 kimesambaa katika wilaya zote za mkoa wa Mbeya kinashawishi watu 
kuipinga BAKWATA na  kinafanya mambo ambayo BAKWATA hatukubaliani nayo,’’alisema Shekhe Killah.
Alisema
 kuwa kikundi hicho kilikuwa kikimtuhumu Shekhe wa Wilaya kuwa ni 
mshirikina na kwamba kutokana na hali hiyo hakupaswa kuongoza ibada 
msikitini na badala yake wao ndio waliopaswa kuongoza ibada msikitini 
hapo.
Kwa
 upande wake Shekhe wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Mohamed Mwansasu alisema 
kuwa kitendo hicho kimeudhalilisha Uislamu na kwamba kilichofanywa na 
kundi hilo la watu si mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Hata hivyo Shekhe Mwansasu alienda mbali zaidi na kusema kuwa katika kikundi hicho wapo  baadhi
 ya waumini wanaodaiwa kuwa ni askari polisi ambapo inadaiwa kuwa katika
 moja ya swala ya Ijumaa wiki iliyopita imamu aliyekuwa akiswalisha 
alivutwa kanzu yake na kutakiwa kutoka eneo la kuongozea ibada ili 
kuwapisha wao waendeshe ibada hiyo.
Kamanda
 wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Athumani Diwani amekiri kutokea kwa tukio 
hilo ambapo alisema kuwa watu sita wanashikiliwa na Polisi kufuatia 
vurugu hiyo iliyotokea majira ya saa 2:30 katika msikiti mkuu wa Ijumaa 
wakati wa swala ya Idd el Fitri.
Kamanda
 Diwani alisema kuwa kundi la waislamu wanaojiita kuwa ni wenye itikadi 
kali walivamia msikitini wakati waumini wengine wakiwa wameinama 
wakisujudu na kumvaa imamu kwa kumpiga kwa mateke na ngumi huku wakiwa 
na nondo, mikasi na visu.
Alisema waumini hao walikuwa na madai kuwa hawamtaki Shekhe huyo na kwamba uwezo wake ni mdogo katika dini.
Alisema
 kuwa Shekhe huyo aliokolewa na baadhi ya waislamu ambapo aliwataja 
walioshikiliwa na polisi kuwa ni pamoja na Mashaka Kassim(30)Issa 
Juma(37),Ahmed Kassim Magogo(35) Ibrahimu Shaaban(17) ambaye ni 
mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kyela anayesoma kidato cha 
Nne,Ambokile Mwangosi,(19)mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya 
sekondari Kyela, Sadick Abdul(28).
Kamanda Diwani alisema kuwa taratibu zinafanyika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani.