WATU watatu akiwemo aliyekuwa Polisi, Edna Kadogo wamehukumumiwa kifungo
 cha miaka saba jela katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es 
Salaam baada ya kupatikana na hatia ya kula njama na kuiba Sh milioni 
330 mali ya Jeshi la Polisi.
Hakimu Gene Dudu alitoa hukumu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa na upande wa mashitaka.
Washitakiwa
 hao walikuwa wanakabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama, kughushi 
na wizi wa kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti namba 2011000015 
inayoitwa Police Retention Collection kwenye benki ya NMB Meatu.
Akisoma
 hukumu hiyo , Hakimu Dudu alisema upande wa mashitaka umethibitisha 
bila kuacha shaka mashitaka mawili dhidi ya washitakiwa watatu na 
mahakama imewaona wana hatia.
Alisema katika mashitaka ya kula 
njama watatumikia kifungo cha miaka miwili jela na wizi wa Sh milioni 
330 watatumikia kifungo cha miaka mitano jela.
Adhabu hizo 
zitakwenda pamoja ambayo ni sawa na kifungo cha miaka mitano. Mbali na 
Kadogo, washitakiwa wengine waliotiwa hatiani ni mfanyabiashara Joshua 
Aseno na Mfanyakazi wa Benki, Adelina Lwekoramu.
Baada ya kutoa 
hukumu hiyo, Hakimu Dudu alimuaru, Aseno arudishe Sh milioni 30 na 
nyingine zilizoingizwa kwenye akaunti yake kutoka katika akaunti ya 
polisi na Kadogo anatakiwa kurudishwa milioni 10.
Aidha mahakama 
imewaachia huru washitakiwa Vedastus Mafuru, Kennedy Achayo, Luciana 
Limbu, Agnes Maro, Mkika Nyasebwa, Amos Hangaya. kwa kuwa upande wa 
mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.
Kesi hiyo 
ilikuwa ikikabili washitakiwa 11 lakini Fortunatus Biseko na Deogratias 
Lumato waliachiwa huru baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu na hivyo
 wakabaki tisa