Nahodha
 wa timu ya taifa ya Tanzania, (Taifa Stars), Juma Kaseja Juma maarufu kama (Juma K. Juma)
amesema kwamba amefanya mazungumzo na wakala wa klabu ya St. Eloi 
Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini bado hajaingia 
Mkataba na klabu hiyo ya Lubumbashi.
Kaseja amesema kwamba mtu aliyejitambulisha kwake kama wakala wa Lupopo alimfuata wakafanya mazungumzo na kufikia makubalino juu ya dau la usajili, mshahara na mambo mengine ya msingi.
Hata
 hivyo, kipa huyo namba moja Tanzania amesema kwamba baada ya mazungumzo
 hayo na maafikiano, wakala huyo amepeleka majibu Lupopo ambao wakiafiki
 ndipo masuala ya Mkataba yatafuatia.
“Nimezisikia
 hizo habari, kwamba mimi tayari ni mchezaji wa Lupopo, hapana, si 
kweli. Ni kwamba tumefanya mazungumzo tu na wakala wao na tumefikia 
makubaliano, nasubiri hadi nisaini Mkataba ndipo nitajihesabu tayari ni 
mchezaji wa Lupopo,”alisema Kaseja.
Pamoja
 na Simba SC kutomuongezea Mkataba Kaseja, ameendelea kuwa kipa chaguo 
la kwanza timu ya taifa mbele ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen.
Iwapo Kaseja atafanikiwa kuingia Mkataba na Lupopo atakwenda kuwa mpinzani mkuu wa wachezaji wenzake wa Taifa Stars, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea Tout Puissant Mazembe ya Lubumbashi.
Kaseja alicheza pamoja na Samatta na kiungo Mganda wa Mazembe, Patrick Ochan katika klabu ya Simba mwaka 2010 kabla ya 2011 wachezaji hao kuuzwa DRC.
Source:Bin Zubeiry 
