Watu wawili wanahofiwa kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa 
kutokana na mlipuko wa bomu lililolipuka kwenye mkutano wa CHADEMA 
katika eneo la Soweto, kata ya Kaloleni jijini Arusha, wakati wa kufunga
 kampeni za uchaguzi wa madiwani katika maeneo ya jiji hilo.
Waliojeruhiwa
 wamekimbizwa katika hospitali za Seliani na Mount Meru ambapo baadhi ya
 watu wamejitolea vyombo binafsi vya usafiri na wengine wanashirikiana 
na Madaktari na Wauguzi wa hospitali hizo kutoa huduma ya kwanza.
Kamanda wa polisi mkoani humo, Liberatus Sabas yupo katika moja ya hospitali hizo.
Bomu
 hilo linaelezwa kuwa lilipuka kwenye mkusanyiko wa watu meta chache 
kutoka jukwa kuu, mwendo wa saa kumi na mbili na robo jioni wakati 
mkutano huo ulipokuwa umekwisha na shughuli ya kukusanya michango 
ikiendelea.
Viongozi wa juu wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Godbless Lema walikuwepo na wameendelea kuwepo kwenye eneo hilo.
Polisi
 wapo katika eneo hilo wakijitahidi kutuliza ghasia lakini inasemekana 
upo upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi wanaojaribu kuwafukuza, hali 
iliyowalazimu kupiga mabomu ya machozi na kukamata watu kadhaa wakiwemo 
viongozi wa CHADEMA. Mwandishi mmoja wa habari anaripotiwa kunyang’anywa
 kamera yake baada kwa kupiga picha, hata baada ya kujitambulisha.
Watu
 wenye hasira wanaripotiwa kuyashambulia na kuyaharibu baadhi ya magari 
ya kutoa huduma ya kwanza (ambulance) kwa kuwa yalichelewa kufika 
kuwaokoa majeruhi.
ILANI: Baadhi
 ya picha zilizopachikwa hapo huenda zikagusa  hisia ya mtizamaji, 
tafadhali ikiwa huwezi kuvumilia kuona damu usibofye kitufye cha kuelekea mbele