Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe imeifuta kesi moja 
inayowakabili viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu 
Zanzibar (Jumiki), kutokana na kuchukua muda mrefu bila ushahidi wake 
kukamilika.
                
              
Hakimu Ame Msaraka Pinja alisema jana kuwa, anaifuta kesi hiyo kwa kutumia kifungu cha 209 cha makosa ya jinai.
Washtakiwa wa kesi hiyo ambayo ilikuwa ni moja 
kati ya tatu zinazowakabili ikiwa kwenye Mahakama hiyo na nyingine 
Mahakama Kuu, walikuwa wanakabiliwa na kesi ya kuhatarisha amani kwa 
kutoa lugha kali.
Ilipotajwa mara ya mwisho, Machi 19 mwaka huu 
upande wa mashtaka ulidai kuwa, upelelezi  haujakamilika na mawakili wa 
utetezi walimwomba hakimu kuifuta kwa vile washtakiwa wako ndani muda 
mrefu.
Wakili wa washtakiwa hao, Salum Toufik na Abdallah
 Juma walimwomba hakimu kutokana na taratibu za Mahakama hususan makosa 
ya jinai, kesi inapofikia  miezi mitatu na kuendelea bila  upelelezi 
kukamilika inapaswa kufutwa.
Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Khamis Jafar 
waliomba Mahakama kuwapa muda zaidi kutokana na kuchukua kipindi kirefu 
bila upelelezi kukamilika.
Washtakiwa hao ni Masheikh Farid Hadi, Mselem Ali,
 Mussa Juma, Azza Khalid Hamdan, Suleiman Juma, Khamis Ali na Hassan 
Bakari. Washtakiwa hao bado wanakabiliwa na kesi iliyopo chini ya Hakimu
 wa Wilaya, Khamis Rashid na washtakiwa wanne wapo nje kwa dhamana, huku
 watatu wakiwa rumande kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine Mahakama 
Kuu.  Washtakiwa watatu ambao walikwenda katika kesi hiyo wakitokea 
rumande ni Masheikh Farid, Juma Suleiman na Mussa Juma.
