![]()  | 
| Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage. | 
Mkutano mkuu wa dharura wa wanachama wa Klabu ya Simba umemwondoa madarakani mwenyekiti wao Ismail Rage na kuivunja Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kwa madai ya kukiuka katiba ya klabu yao.
Awali uongozi wa Simba ulipiga marufuku mkutano 
huo usifanyike kwa sababu haukuwa halali, lakini jana wanachama wa Simba
 walifanya mkutano huo kwenye Hoteli ya Starlight jijini Dar es Salaam 
na  kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 600.
Hata hivyo, kwa mujibu wa katiba ya Simba, ni 
mwenyekiti aliye madarakani kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji ndiye
 mwenye mamlaka ya kupanga ajenda, mahali na wakati wa kufanyika kwa 
mkutano mkuu.
Mbali ya kumtimua Rage, mkutano huo pia 
ulimpendekeza aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Simba, 
Zacharia Hans Pope na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Simba, 
Rahma Al Kharoos kuongoza Kamati Maalumu ya kuiongoza Simba hadi pale 
uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utakapofanyika.
Mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Mohamed
 Wandi na katibu wake Maulid Said ulikuwa na ajenda iliyojadili mwenendo
 mbovu wa klabu ya Simba kwenye Ligi Kuu inayoendelea na kutokuwa na 
imani na viongozi wa Simba.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo uliokuwa 
na utulivu mkubwa huku ukilindwa na askari polisi wachache, Wandi 
alimlaumu Rage kwa madai kwamba amekuwa akiiendesha klabu yao bila 
kufuata katiba.
“Ibara ya 16 kipengele G inasema kutakuwa na 
mkutano kila baada ya miezi minne kujadili maendeleo ya klabu, lakini 
haujafanyika mpaka leo.
Alisema,“Ibara ya 22 ya katiba ya klabu ya Simba 
inatupa wanachama haki ya kuitisha mkutano endapo mwenyekiti na makamu 
mwenyekiti hawatakuwapo na Ibara ya 19 kifungu cha tatu inatupa mamlaka 
ya kumwandikisha na kumfukuza mwanachama.”
Baada ya kumaliza kusoma sehemu ya katiba ya klabu
 ya Simba aliyodai imekiukwa, Wandi aliwataka wanachama wenzake kuamua 
kama Rage na kamati yake ya utendaji ipewe muda zaidi au iondolewe ndipo
 wote waliponyoosha mikono juu wakitaka watimuliwe na kuunda kamati ya 
muda chini ya Hans Pope na Rahma Al Kharoos.
Hata hivyo, Hans pope alikataa kuchukua jukumu 
hilo akisema “Sijapewa taarifa yoyote juu ya uteuzi huo, hata hivyo 
siafiki suala hilo kwa vile hawajaomba hata ushauri kabla ya kufikia 
uamuzi wao.”
Juhudi za Mwananchi kuwapata viongozi wa Simba akiwamo ziligonga mwamba huku simu zao zikiita bila kupokelewa.
SOURSE: MWANANCHI
SOURSE: MWANANCHI
