
Mbunge wa jimbo la Ubungo-Chadema Mh John Mnyika-
---
Nchi 
imeingia tena katika mgawo wa umeme kinyume na ahadi iliyotolewa na 
Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo bungeni tarehe 28 
Julai 2012. 
Hali hiyo
 ni matokeo ya Serikali kutozingatia tahadhari niliyoitoa bungeni tarehe
 27 Julai 2012 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kwa nyakati 
mbalimbali kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini juu ya
 hali tete iliyotarajiwa kuwepo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika 
utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme. 
Ikiwa ni 
sehemu ya wajibu wa kibunge wa kuisimamia Serikali nawataka viongozi na 
watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Nchini 
(TANESCO) kuacha kuficha hali ya mambo na kuwaeleza ukweli wananchi 
kuhusu mgawo wa umeme uliojitokeza na hatua za haraka zinazochukuliwa 
kurekebisha hali hiyo. 
Iwapo 
Wizara na TANESCO hawatatoa matangazo ya ukweli kwa wananchi, kwa nafasi
 yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nitaeleza vyanzo vya mgawo 
wa umeme uliojitokeza ili hatua ziweze kuchukuliwa wakati huu ambapo 
wajumbe wa kamati ya nishati na madini wenye wajibu wa kuisimamia 
Serikali kwa niaba ya Bunge katika sekta hizo nyeti hawajateuliwa.
Aidha, 
pamoja na kutoa maelezo kuhusu mgawo wa umeme, Wizara ya Nishati na 
Madini na TANESCO watumie nafasi hiyo pia kueleza hatua zilizochukuliwa 
kuhusu ukaguzi wa awamu ya pili kuhusu tuhuma za ufisadi katika ununuzi 
wa vifaa na uzalishaji wa umeme wa dharura ikiwemo kuhusu mafuta mazito 
ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme. 
Ikumbukwe
 kwamba mwanzoni mwezi Agosti 2012 Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za 
Serikali (NAOT) iliunda timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalum wa 
hesabu za Shirika la Umeme (TANESCO) kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa 
fedha za umma zilitajwa bungeni na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini 
katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani tarehe 27 Julai 2012 na Waziri 
wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya hoja ya Serikali tarehe 28 
Julai 2012. 
Wizara ya
 Nishati na Madini na TANESCO waeleze pia hatua iliyofikiwa kuhusu 
uchunguzi mwingine uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma 
(PPRA) kuanzia mwezi Agosti 2012 wa mchakato wa ununuzi wa mafuta mazito
 ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme wa dharura kutokana na tuhuma 
mbalimbali zilizotolewa bungeni kuhusu ununuzi huo suala ambalo Kambi 
Rasmi ya Upinzani ilitaka pia tarehe 27 Julai 2012 liundiwe kamati teule
 ya Bunge ili uchunguzi wa kina uweze kufanyika. 
Wenu katika uwakilishi wa wananchi, 
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini 
27 Februari 2013
CHANZO CHA HABARI HII: www.dj-sek.blogspot.com