
 Mabingwa wa kombe la Kagame timu Young Africans leo imeendeleza 
wimbi lake la ushindi katika mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom 
baada ya kuichapa timu ya  African Lyon jumla ya mabao 4-0, katika 
mchezo uliofanyika jioni hii katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar 
es salaam.
Young Africans ambayo inaongoza ligi kwa kuwa na pointi
 36 na mabao 33 ya kufunga, iliingia uwanjani kwa ajili ya kusaka pointi
 3 muhimu ambazo imefanikiwa kuzipata.
Kikosi cha 
mholanzi Ernest Brandts kiliuanza mchezo kwa kasi, na katika dakika 15 
za kwanza washambuliaji wake Hamis Kiiza na Jerson Tegete walikosa 
nafasi za wazi za mabao ya mapema, kufuatia kutokua makini katika 
umaliziaji.
Jerson Tegete aliwaiunua mashabiki wa 
Yanga katika dakika ya 21 baada ya kuipatia timu yake bao la kwanza kwa 
kichwa akimalizia pasi safi iliyopigwa na mlinzi wa pembeni David 
Luhende ambaye alipanda kuongeza nguvu mashambulizi.
Yanga
 iliendela kuutawala mchezo na hasa sehemu ya kiungo, ambapo Haruna 
Niyonzima, Athumani Idd Chuji, Frank Domayo waliweza kuitawala sehemu 
hiyo ya katikati hali iliyopelekea wachezaji wa African Lyon kuutafuta 
mpira kwa tochi.
Dakika ya 42, Jerson Tegete tena 
aliipataia Young Africans bao la pili kwa staili ya peke, baada ya 
kuupiga kwa kisigino mpira wa krosi uliokuwa umepigwa na Haruna 
Niyonzima na kumfanya mlinda mlango wa African Lyon Abdul Seif na 
walinzi wake wasijue cha kufanya.
Saimon Msuva 
alitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini mipira hiyo ilipowakuta 
wafungaji hawakua katika nafasi nzuri ya umaliziaji hali iliyopelekea 
kukosa mabao mengine ya wazi katika kipindi cha kwanza. 

 Kocha
 wa African Lyon, Salum Bausi, akiwa katikati ya uwanja akiwatuliza 
wachezaji wake kukubali kupigwa penati, waliyokuwa wakiigomea, huku 
wakimzonga refa.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza Young Africans 2-0 African Lyon.
Kipindi
 cha pili kilianza kwa kasi na Yanga kuutawala mchezo hali iliyopelekea 
kujipatia penati dakika ya 48 ya mchezo, kufuatia walinzi wa African 
Lyon kuzidiwa na kiungo Haruna Niyonzima hali iliyowapelekea kumcheza 
madhambi mchezaji huyo ndani ya eneo la hatari, mwamuzi aliamuru ipigwe 
penati ambayo iilipigwa na Hamis Kiiza ambaye alikosa penati hiyo.
Kocha
 wa Yanga Ernest Brandts alifanya mabadiliko ya kuwaingiza Didier 
Kavumbagu, Said Bahanuzi, na Nizar Khalfani ambao walichukua nafasi ya 
Hamis Kiiza, Jerson Tegete na Saimon Msuva.
Mabadiliko
 hayo yalizidi kuongeza kasi ya mashabuluzi langoni mwa African Lyon 
kwani dakika ya 70, Didier Kavumbagu aliipatia Yanga bao la tatu kwa 
mkwaju wa penati kufuatia mlinzi wa African Lyon Obina Salamusasa 
kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Dakika ya 
80 Nizar Khalfani aliipatia bao la  nne kwa ustadi mzuri wa umaliziaji, 
akimalizia pasi ya Said Bahanuzi ambaye aliwazidi ujanja walinzi wa 
African Lyon na kupiga krosi hiyo iliyowapita walinzi na mlinda mlango 
Juma Abdul.
Mpaka mwisho wa mchezo Young Africans 4 - 0 African Lyon
Kocha
 mkuu wa Yanga Ernest Brndts amesema anashukuru timu yake  kupata kwa 
ushindi katika mchezo wa leo, kipindi cha kwanza washambuliaji wangu 
hawakuwa makini lakini kipindi cha pili timu ilibadilika sana hali 
iliyopelekea kuutawala mchezo kwa kipindi chote na kuongeza mabao mawili
 ya haraka.
Baada
 ya mchezo huu wa leo kikosi cha Young Africans kitaendelea na mazoezi 
yake kesho asubuhi katika uwanja wa Mabatini Kijitonyama ikiwa ni 
maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya timu ya Azam FC februari 23 
katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Young Africans:
 1.Ally Mustapha 'Barthez', 2.Juma Abdul, 3.David Luhende, 4.Nadir 
Haroub'Cannavaro', 5.Kelvin Yondani, 6.Athuman Idd 'Chuji', 7.Saimon 
Msuva/Nizar
 Khalfani, 8.Frank Domayo, 9.Jerson Tegete/Didier Kavumbagu 10.Hamis Kiiza/Sadi Bahanuzi, 11.Haruna Niyonzima
African Lyon: 1.Abdul
 Seif, 2.Yusuf Mlipili, 3.Sunday Bakari, 4.Ibrahim Job, 5.Obina 
Salamusasa, 6.Abdulehan Gulam, 7.Amani Kyata, 8.Mohamed Samata, 9.Idd 
Mbaga, 10.Bright Ike, 11.Adam Kingwande
Katika michezo mingine ya ligi hiyo iliyochezwa leo, JKT Mgambo imeifunga Oljoro JKT mabao 2-0, Kagera Sugar imeifunga Coastal Union bao 1-0, Toto African imetoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Polisi Moro na Mtibwa Sugar imetoka suluhu na Ruvu Shooting.