Serikali imeingilia kati sakata la 
uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuamuru kufutwa kwa 
katiba ya sasa ya shirikisho hilo na badala yake kuamuru itumike katiba 
ya zamani (mwaka 2006) baada ya kubaini kuwa iliyopo ina kasoro nyingi.
Katika
 taarifa yake kwa waandishi wa habari leo, Wizara ya Habari, Utamaduni, 
Vijana na Michezo imeeleza kuwa katiba ya sasa ya TFF si halali. 
Imeelezwa vilevile kuwa msajili wa vyama vya michezo aliyedaiwa 
kuipitisha katiba hiyo ameondolewa. 
Mchakato wa uchaguzi mkuu wa
 TFF umesimamishwa kutokana na mgogoro mzito uliotokana na kuenguliwa 
kiutata kwa wagombea kadhaa, wakiwamo Jamal Malinzi anayewania urais na 
Michael Wambura anayetaka kugombea nafasi ya makamu wa rais.
Kamati
 ya rufani ya TFF inayoongozwa na Iddi Mtiginjola ndiyo iliyozua balaa 
lote la sasa baada ya kuwaengua kina Malinzi na mwishowe kumuacha makamu
 wa sasa wa rais, Athumani Nyamlani abaki kuwa mgombea pekee.
Hata
 hivyo, tayari mchakato wa uchaguzi huo uliozua mabishano makali 
umeshasimamishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na maafisa wa
 chombo hicho cha juu cha mchezo wa soka duniani wameshaanza kuwasili 
kufuatilia kinachotokea nchini.
Uamuzi wa serikali wa kufuta 
katiba ya sasa na kutaka itumike ya 2006 unampa ahueni kubwa Wambura 
ambaye alishasema hadharani kuwa  ataiburuza TFF mahakamani kama 
isipoachana na katiba mpya na kufuata ya zamani; huku akitoa sababu 
kadhaa za kupinga matumizi ya katiba mpya, mojawapo ikiwa ni kupitishwa 
kwake kwa njia ya waraka wa barua pepe (e-mail) kwenda kwa wajumbe 
badala ya kufuata maelekezo ya katiba yanayotaka mabadiliko kufanywa na 
wajumbe kupitia mkutano mkuu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu 
za FIFA, ni marufuku kwa shughuli za soka kuingiliwa na serikali au 
mahakama na nchi yoyote inayokwenda kinyume na taratibu hizo hujikuta 
ikifungiwa kama ilivyowahi kutokea nchini Kenya.
