MSHAMBULIAJI wa Yanga, Said Bahanuzi 
amesema anafikiri kwa sasa amerudi kwenye fomu isipokuwa tu kocha ndiye 
anashindwa kumwamini kuanza kikosi cha kwanza.
 
Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts amekuwa akimtumia Bahanuzi kama mchezaji wa akiba tangu aliporejea uwanjani.
Bahanuzi aliyejiunga na Yanga msimu 
huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro alikuwa anasumbuliwa na maamivu ya
 nyama za paja aliyoyapata akiwa na timu ya Taifa Stars mwaka jana.
 
Katika mechi mbili za ligi ambazo nyota 
huyo ametokea benchi zikiwa zimebaki dakika 15 kabla ya mchezo 
kumalizika amefanikiwa kutoa pasi ya bao kila mechi.
Mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar 
uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Bahanuzi ndiye 
aliyetoa pasi kwa Hamis Kiiza kufunga bao la kusawazisha. Timu zote 
mbili zilifungana bao 1-1.
Pia, mchezo wa African Lyon 
uliochezwa Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Bahanuzi akitokea 
benchi alitoa pasi kwa Nizar Khalfan aliyefunga bao la tatu wakati Yanga
 ikishinda 4-0.
Mara zote anapoingia mshambuliaji 
huyo mwenye nguvu za miguu na uwezo wakufyatua mashuti makali, amekuwa 
akiichangamsha safu ya ushambuliaji ya Yanga tofauti alivyokuwa benchi.
"Kwa sasa nafikiri nimerejea kwenye 
fomu. Nafikiri kocha tu ndiye anashindwa kuniamini." alisema Bahanuzi 
mwenye bao moja kwenye ligi alilofunga kwa penalti dhidi ya Simba Oktoba
 3, mwaka jana.
"Nilikuwa nasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja. Kwa sasa nafikiri hali yangu imeimarika kama awali." alisisitiza.
Kwa upande wake Ernie Brandts 
alisema; "Siwezi kumchezesha dakika 90. Nadhani Bahanuzi ametoka kwenye 
majeruhi. Kwa hiyo nimekuwa nikimpa dakika 15 za mwisho kutizama 
maendeleo yake.
"Nafikiri ameimarika kwa mechi mechi ambazo nimemuona akicheza." 
