Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu akiwaeleza waandishi wa habari kuwa 
Chama chake kimependekeza kuwepo kwa utawala wa majimbo utakaorahisisha 
shughuli za maendeleo kwa wananchi Picha na Salhim Shao 
            
Kwa ufupi
“Pia kinga ya Rais inatakiwa kuondolewa ili kuleta 
nidhamu ya utendaji katika ofisi hii ya umma. Akifanya makosa ya jinai 
ashtakiwe kama mhalifu mwingine, hakuna sababu ya baadhi ya watu kuwa 
juu ya sheria, kila mtu awe chini ya sheria,”
MCHAKATO wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi 
yatakayosaidia katika uundwaji wa Katiba Mpya unaendelea na safari hii 
ni zamu ya makundi maalumu vikiwemo vyama vya siasa ambavyo vimeanza 
kutoa maoni yao mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mikutano hiyo kati ya Tume na wawakilishi wa vyama
 vya siasa inafanyika katika Ofisi Kuu za Tume pamoja na Ukumbi wa 
Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Vyama vyote vimepewa fursa ya  kushiriki katika 
utoaji maoni na baadhi ya mambo ambayo wameyapendekeza kuwamo katika 
Katiba Mpya ni pamoja na utawala wa majimbo na kuwapo kwa mgombea 
binafsi.
Kimsingi hoja hizi zimekuwa zikitolewa maoni mara 
nyingi na wananchi katika mikutano mbalimbali ya Tume iliyokuwa 
ikifanyika nchi nzima kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, tofauti na 
sasa ni kwamba wanasiasa wamezieleza kwa undani zaidi na kuzifafanua 
namna gani zinavyoweza kuingia katika Katiba ijayo.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) 
kimejikita zaidi katika muundo wa Muungano na utawala wa majimbo, wakati
 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejielekeza kwenye hoja ya mgombea binafsi.
Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu anasema kuwa 
chama chake kinataka kuona Katiba Mpya inakuja na mfumo mpya ambao 
utaleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali zikiwamo utawala, 
rasilimali, ulinzi wa mali za umma, haki za binadamu, uwajibikaji 
serikalini na muundo wa Jamhuri ya Muungano ambao utasaidia kuunusuru 
usivunjike.
Lissu anasema kuwa kuna kila sababu ya Katiba Mpya
 kuleta mabadiliko katika muundo wa Muungano ambao Chadema wanapendekeza
 uwe Muungano wa Shirikisho wa Serikali tatu, yaani Serikali ya Jamhuri 
ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ndogo ya 
Jamhuri ya Muungano.
“Hatuwezi kuendelea na mfumo uliopo wa Muungano 
kwani una upungufu mwingi. Ni fursa nzuri ambayo tumeipata ya 
kutengeneza Katiba Mpya ya nchi ambayo kimsingi inapaswa kuleta 
mabadiliko yatakayounusuru au kuuokoa Muungano usivunjike. Tukikosea 
tunaweza kujikuta tunatengana kama ilivyo kwa Ethiopia na Eritrea, Sudan
 na Sudan Kusini, Yugoslavia na Czechoslovakia,” anasema Lissu.
Pia anasema kwa kuwa Muungano wa Tanganyika na 
Zanzibar ni wa hiari kunatakiwa kuwe na haki ya kujitoa kwa upande 
usioridhika kuendelea kuwa kwenye Muungano.
Anasema utaratibu wa kujitoa uwe kwa njia ya kura 
ya maoni itakayopigwa na wananchi wa upande mmojawapo wa Muungano na 
ikiwa theluthi mbili ya wananchi wakikubali kujitoa basi iruhusiwe 
wajitoe kwa sababu Muungano huu haukuwa wa lazima.
Lissu anaongeza kuwa kwenye mambo ya Muungano 
wamependekeza yawemo mambo saba tu ambayo ni ulinzi na usalama, wizara 
zisizozidi 18, Bunge lisilozidi wawakilishi 300, mamlaka ya uteuzi ya 
Rais ambayo yanapaswa kupunguzwa, Rais ashtakiwe akifanya makosa ya 
jinai, pamoja na kuweka bayana suala la umilikaji wa rasilimali za nchi.
Kuhusu mamlaka ya uteuzi ya Rais anaeleza kuwa ni lazima yapunguzwe ili kuiondoa nchi kwenye mfumo wa urais wa kifalme.