HISTORIA ya wachezaji wa Yanga kulala mzungu wa nne imejirudia tena
Bukoba, baada ya kulala kwa kubanana katika kitanda kimoja kama
ilivyokuwa Mbeya, licha ya kufikia katika Hoteli ya Smart, yenye hadhi
kubwa.
Hali kama hiyo ilijitokeza wakati timu hiyo ikijiandaa kucheza na
Prisons, Mbeya, huku aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet
akianika ukweli ambao baadaye ulimponza na kufukuzwa.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wachezaji alisema, mambo ni yale yale kama ilivyokuwa Mbeya.
“Mambo
kama ya Mbeya, hoteli ni nzuri, lakini wachezaji tumelala wawili wawili
katika hoteli, pamoja na kupata huduma nzuri lakini tatizo lilikuwa ni
hilo,” alisema mmoja wa wachezaji hao.
Hata hivyo wachezaji
wanatarajiwa kurejea kwa usafiri wa basi, badala ya ndege maalumu ya
kukodi ya Kampuni ya Precision Air, iliyotumika kwenda Kagera kwa ajili
ya mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Kagera, uliochezwa
jana kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Habari zilizopatikana kutoka kwa
kiongozi mmoja, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, zinasema
wachezaji hao watarejea kwa usafiri huo baada ya mchezo wao dhidi ya
Toto African, ambao utachezwa keshokutwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Wachezaji
hao wanatarajiwa kuondoka mjini Mwanza Ijumaa, baada ya kumalizika kwa
mchezo wao dhidi ya Toto African, kwa basi maalumu walilopewa na
wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania TBL kupitia kinywaji chake cha
Kilimanjaro.
Hata hivyo, gazeti hili liliweza kuongea na mkuu wa
msafara, Mussa Katabaro, ambaye alisema anachojua yeye ni kwamba timu
yao itarejea kwa ndege kama ilivyokuja.
Wakati huo huo, uongozi
wa Kagera Sugar uliondoa mabango ya wadhamini wa Yanga, Kampuni ya Bia
Tanzania, kutokana na kuwa wenyeji wa mchezo huo.
Kagera Sugar
ambao ndio wenyeji wa uwanja huo kupitia kwa mratibu wake Mohamed
Hussein, ilikataa katu katu mabango hayo kuwekwa katika uwanja huo, kwa
kuwa wao ndio wa miliki wake.