KULIA: Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam. KUSHOTO: Dk Harrison Mwakyembe.  
Kuanzia 
sasa viongozi wote serikalini watakaopita kwenye viwanja vya ndege 
nchini, watakuwa wakikaguliwa kama abiria wengine, isipokuwa Rais, 
Makamu wake, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu na Spika wa Bunge.
Waziri  
wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema ipo tabia ya  viongozi  wenye
 madaraka, kukiuka utaratibu na kupita   katika  viwanja vya ndege  bila
 kukaguliwa.Alisema
 kutokana na hali hiyo, amewaambia watumishi  wanaofanya kazi katika 
viwanja hivyo, hususan Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere 
(JNIA) viongozi wasiokaguliwa ni Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Jaji
 Mkuu na Spika wa Bunge.
 
Alitoa 
msimamo huo wiki iliyopita  kupitia kipindi cha Jenerali on Monday, 
kinachorushwa na Televisheni ya Channel Ten. Alisema viongozi wengine 
wote, wakiwamo mabalozi na mawaziri lazima wakaguliwe.
Dk
Mwakyembe alisema aliwaambia viongozi wasiopenda kukaguliwa, wasipande ndege.
Alisema pamoja na baadhi kuona ni usumbufu, inawezekana wakajikuta wamesahau
vitu hatari, kama vile risasi na wakaenda kugundulika nje ya nchi ikawa tatizo.
Alitoa
mfano kwamba aliwahi kupigiwa simu na mmoja wa mabalozi, akilalamika kwamba vijana
wake wamemkagua uwanja wa ndege. Alisema alimjibu kwamba wanatimiza wajibu wao.
Katika
mahojiano yaliyojikita juu ya tatizo la 
dawa za kulevya  nchini, Dk
Mwakyembe alisisitiza  kwamba hatua
alizoanza kuchukua kudhibiti upitishaji dawa hizo kwenye viwanja vya ndege,
siyo moto wa kifuu wala nguvu ya soda. 
 “Ninachokifanya hapa  ni kile ambacho kinapaswa kufanywa…na hili la
dawa za kulevya katika viwanja vya ndege, nitalikomesha,” alisema. Alisisitiza
kwamba udhibiti huo ni kwa viwanja vyote vya ndege nchini.
 Dk Mwakyembe alisema,  “kwa sasa mizigo yote inayoingia katika eneo
hilo, lazima ikaguliwe, kwani huo sio mzaha, sio moto wa kifuu wala nguvu ya
soda.”
Kwa
mujibu wa Waziri, mizigo inayoingia imekuwa haikaguliwi. Alisema katika
kutekeleza ukaguzi huo wa mizigo inayoingia, imenunuliwa  mitambo kwa 
ajili hiyo.  Kuhusu wanaomeza dawa
za kulevya,  alisema wamekuwa
wakigundulika kutokana na ufuatiliaji kuanzia kwenye ndege. 
Alitoa
mfano kwamba  kwa sasa endapo abiria
atapanda ndege katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, mathalani kwenda Dubai,
akipewa chai au pombe, akakataa kunywa, 
kwa vyovyote huyo lazima akaguliwe zaidi. 
Katika
hilo, aliwaasa vijana wa Tanzania kujiepusha na hali hiyo, kwani pindi akishuka
kwenye uwanja wowote, namba yake ya kiti itashikiliwa na atakaguliwa ipasavyo,
kubaini kama amemeza dawa.
Hatua
ya Mwakyembe kuamua kuvalia njuga dawa za kulevya, inatokana na kile ambacho
kinaelezwa kuwa ni kuchafuka kwa Tanzania, kutokana na baadhi ya watanzania
kukamatwa nje ya nchi, wakisafirisha dawa hizo, wakiwa wamezipitisha uwanja wa
ndege.  Dk Mwakyembe alieleza kuwa hatua
yake ya kuvalia njuga suala hilo, inaungwa mkono na serikali kwa ujumla. Hivi
karibuni waziri huyo alifanya ziara ya ghafla 
katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere na kubaini kuwa tatizo si
vifaa vya ukaguzi, bali ni baadhi ya wafanyakazi wasio waadilifu. Msemaji Mkuu
wa Serikali ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene
alisema hivi karibuni serikali imeanzisha mkakati wa kutokomeza wimbi la dawa
za kulevya kwa kudhibiti viwanja vya ndege na sehemu mbalimbali za mipakani,
zinazotumiwa kupitisha.